Habari za leo rafiki?

Naamini uko vizuri na unaendelea kuweka juhudi kwenye kile ulichochagua kufanya kwenye maisha yako, maana hakuna namna nyingine bali kuweka juhudi na maarifa huku ukijijengea nidhamu ya hali ya juu. Kwa njia hii hakuna chochote ambacho kitakushinda.

Leo katika mazungumzo yangu mimi na wewe nataka tuguse eneo moja muhimu sana ambalo tumekuwa tukifanya makosa ya wazi. Na eneo hili tunafanya makosa mara nyingi kutokana na hisia, au kutokana na taarifa za uongo au kutokana na kuchoshwa kwetu. Na kikubwa kabisa kukosa uelewa ndio kunatuingiza kwenye makosa makubwa.

Dunia ina upacha, na tumewahi kujadili hili kwa kina sana kwenye makala za FALSAFA MPYA YA MAISHA, na tukaona jinsi ya kutumia upacha huu vizuri. Kama hukusoma makala ile isome hapa; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Upacha wa dunia na jinsi ya kuutumia kuwa na maisha bora.

Leo tutaanzia kwenye upacha huo kwa sababu kwa vyovyote vile utakuwa upande mmoja au mwingine wa hali mbili zinazotokea kwenye eneo lolote la maisha yako. na upande uliopo, utaathiri sana kile unachochagua na unaweza kupelekea wewe kufanya maamuzi ambayo siyo bora kwako.

Kila kitu ni kibovu, inategemea wewe uko upande upi. Maana kwenye chochote kibovu pia kuna kizuri na unaweza kuwa kwenye upande wa kuangalia uzuri tu au ukawa kwenye upande wa kuangalia ubaya tu, na hapa ndipo matatizo yote yanapoanzia.

Nafikiri hii imewahi kutokea kwako, au kwa mtu unayemfahamu, anaacha kazi sehemu moja kwa kuwa amepata kazi sehemu nyingine anayoona ni nzuri zaidi, lakini baada ya kwenda kule kupya anakuta mambo siyo mazuri kama alivyotegemea. Au anakuta ni mabovu kuliko hata kule alipotoka. Au mtu anaondoka kwenye mahusiano aliyopo sasa, iwe ya uchumba au ndoa na kwenda kuingia kwenye mahusiano mengine, lakini yanakuwa mabovu kuliko yale aliyoondoka.

Waswahili wanakuambia ni kuruka majivu na kukanyaga moto. Ukweli ni kwamba kila kitu ni kibovu, na uzuri ni kwamba kila kitu ni kizuri inategemea tu wewe umeamua kuweka mkazo kwenye nini.

Kila kitu unachoona ni kizuri kwa nje, huwezi kujua ndani kuna nini, mpaka utakapofika pale. Lakini naweza kukuhakikishia kwamba ndani kuna ubovu. Kila kitu unachoona ni kibaya sana kwa nje, ndani kuna uzuri. Ni wewe ndio unaamua kipi uchukue kati ya hivyo viwili.

Kitu kingine kinachofanya hata kile kizuri kuonekana kibaya zaidi ni mategemeo makubwa yanayokuwa yamewekwa na wengi. Kwa mfano mtu anapotoka kwenye kazi moja kwenda nyingine, anakuwa na mategemeo makubwa sana, hivyo hata kama atapata kawaida na alivyokuwa anapata kwenye kazi ya awali, ataona ni mbaya kulingana na matarajio yale yalivyokuwa.

Nataka uondoke na nini hapa rafiki yangu?

Ninachotaka uondoke nacho hapa ni kufikiri kwa kina kabla hujafanya maamuzi yoyote, hasa maamuzi makubwa ya maisha yako. kwenye kitu chochote unachofanya au unachokwenda kufanya jua kina ubovu wake na kina uzuri wake pia. Kabla hujafikia hatua ya kubadili kutoka moja kwenda nyingine, kaa chini na orodhesha ubora na ubovu w akila hatua unayochukua.

Kikubwa zaidi ninachotaka wewe rafiki yangu uondoke nacho ni hiki…

Baada ya kujua ubovu na uzuri, na ukaamua kuchukua hatua, chukua hatua ambayo utaisimamia hata kama haitaleta matokeo mazuri kwako kwa muda mfupi. Maana unaweza kuchukua hatua na kuona haileti matokeo mazuri na ukaiacha. Hata unapoacha na kuenda kufanya kingine bado kuna uzuri na ubovu. Hivyo fikiri kwa kina, jua ubovu na uzuri wa kila hatua unayotaka kuchukua, na amua hatua ambayo unaweza kuisimamia mpaka upate kile unachotaka.

Usikubali kuwa sehemu ya wengi ambao wanaendeshwa kwa mkumbo, ambao wanafanya maamuzi yao kwa kuangalia upande mmoja tu. Fanya maamuzi ukiwa na taarifa kamili, taarifa sahihi.

Kila la kheri rafiki yangu katika kufanya na kusimamia maamuzi bora sana kwako.

MUHIMU; Kama una mfano wa jinsi umewahi kufanya maamuzi kwa kuangalia upande mmoja na kuja kugundua kwamba haya kuwa bora tafadhali tushirikishe kwa kujibu email(kama umepokea kwenye email) au kwa kuweka maoni hapo chini kama unasomea kwenye blog. Tushirikishane ili kujifunza zaidi.

TUPO PAMOJA,

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz