Karibu mwanafalsafa mwenzangu kwenye siku hii nyingine ambapo tunakutana pamoja katika kujenga falsafa bora sana itakayoongoza maisha yetu. Kupitia falsafa hii mpya tunapata mwongozo wa maisha bora, yenye furaha na mafanikio makubwa sana.

Leo katika falsafa tutachimba ndani kuhusu furaha ya kweli kwenye maisha. Kumekuwa na upotoshaji mkubwa sana kwenye jamii zetu ha huu umepelekea watu kuishi maisha ambayo hayana furaha. Na maisha yasipokuwa ya furaha basi hayawezi kuwa bora na huwezi kupata mafanikio. Hata kama utakuwa na fedha nyingi kiasi gani, kama huna furaha maisha yatakuwa machungu sana.

Na unajua furaha ya kweli inatoka wapi?

Tulishajadili hili kwenye makala mbalimbali za AMKA MTANZANIA na KISIMA CHA MAARIFA. Na tumekuwa tunaona kwamba furaha ya kweli inatoka ndani ya mtu mwenyewe. Haitoki kwa mtu mwingine, haitokani na mali unazomiliki, bali inatokana na jinsi ulivyoridhika na maisha uliyonayo. Naweza kusema furaha inaanzia kwenye maisha yako ya kiroho, pale unapoona maisha yako yana thamani kubwa, pale unapoona maisha yako yanagusa maisha ya wengine na unapoona uwepo wako hapa duniani ni muhimu sana.

SOMA; HII NI HAKI YAKO YA KUZALIWA, USITEGEMEE KUPEWA NA WENGINE

Lakini, kama tulivyoona hapo juu, kumekuwa na upotoshwaji mkubwa sana wa furaha. Kumekuwa na upotoshwaji kwenye kuipeleka furaha mbele, kwamba nikishapata hiki ndio nitakuwa na furaha, lakini nini kinatokea unapopata kitu hiko? Unasogeza mbele zaidi, na hivyo kujikuta unaikimbiza furaha muda wote wa maisha yako. upotoshwaji mwingine mkubwa sana unaofanyika ni kuhusu furaha ya wengine, yaani kuwafurahisha wengine. Hapa ndipo tutakapojadili leo maana kuna changamoto kubwa.

Upotoshwaji kuhusu kuwafurahisha wengine.

Kwanza kabisa tulipokuwa watoto wadogo, hatukuwa tunajali kuhusu wengine, tulichokuwa tunajali ni sisi wenyewe, hivyo kama tunataka kitu tutalia mpaka tukipate. Tulikuwa tunataka furaha zetu sisi wenyewe. Kadiri tulivyokua tunakua tukaanza kujifunza kutokana na matendo ya jamii, kwamba ili baba na mama wanipende na wanipe zawadi, basi ni lazima nifanye kile ambacho kitawafanya wafurahi. Hata kama kwako hakikupi furaha, ni bora kuwafurahisha wazazi.

Hivyo mtazamo na mwelekeo ukabadilika, badala ya kufanya kile ambacho kitakupa furaha wewe, ukasukumwa kufanya kile ambacho kitawafurahisha wengine. Mambo yakaendelea hivi na lengo kuu sasa likawa ni kutaka kumfurahisha kila mtu, na hivyo kujaribu kufanya kile ambacho kinamfurahisha kila mtu. Ukawa unafanya hivyo shuleni, kwa kujaribu kufanya kile ambacho kila mtu atafurahi, hata kama wewe hufurahi.

Kadiri tulivyoendelea kukua, tukajifunza kitu kingine muhimu, kwamba licha ya kutaka kumfurahisha kila mtu, bado sio wote watakaokubaliana na wewe. Na hivyo hata ukazane vipi, kuna ambao watafurahia, na kuna ambao watachukia. Tukajifunza hili kwa uhalisia kabisa, kwenye elimu, kazi, biashara na hata maisha kwa ujumla. Unaweka juhudi ukijua ya kwamba itamsaidia kila mtu, lakini kuna ambaye anaona juhudi unazoweka hazina maana yoyote, au unajipendekeza, au una hila zako. Na mengine mengi.

Ulipofika hatua hii jamii ikakukumbusha kwamba huwezi kumfurahisha kila mtu, bali unaweza kuwafurahisha wachache. Ukakubaliana na jamii kwenye hili, na hivyo ukawapuuza wale wachache ambao hata ukifanya mazuri wanakupinga, na ukakazana kuwafurahisha wale wachache. Lakini kadiri unavyowafurahisha hawa wachache ndivyo maisha yako yanavyozidi kuwa magumu. Kwa sababu nguvu zako kubwa ni kuwafurahisha watu hawa, basi unalazimika kufanya mambo ambayo wewe mwenyewe huyafurahii. Na kwa sababu wao wanataka kufurahia zaidi, unajikuta unalazimika kufanya zaidi, na hivyo kuzidi kufanya mengi ambayo huyafurahii.

Maisha yanakwenda, wale unaotaka kuwafurahisha wanafurahi kwa muda ila baadae wanataka zaidi, huku wewe maisha yako yakiwa hayana maana kabisa kwako. Kila unapokuwa mwenyewe huoni ni jinsi gani maisha yako yalivyo muhimu kwako. Lakini kwa sababu jamii ilishakwambia wafurahishe wale wachache, basi unaona ni vyema kuyatoa maisha yako sadaka kwa sababu ya wachache. Ni vizuri kutoa maisha yako sadaka, kama kweli unayatolea sadaka kwenye kitu hasa, lakini katika kuwafurahisha wengine, sio sadaka hata kidogo. Ni mara ngapi unaona mtu anawasaidia watu kwa muda mrefu, lakini siku moja anakosea na yote mazuri aliyofanya yanasahaulika na kinachokumbukwa ni kile kibaya alichofanya? Usilalamike, ndio uhalisia wa dunia na leo tunakwenda kuweka mambo sawa.

Karibu kwenye ukweli kuhusu furaha na kuwafurahisha wengine.

Katika FALSAFA HII MPYA YA MAISHA, lengo letu kuu ni kuujua ukweli, kwa sababu wanafalsafa wengi waliopita walithibitisha ya kwamba ujue ukweli na utakuweka huru. Na hata kwenye hili la furaha na kuwafurahisha wengine, haupo huru kwa sababu hujaujua ukweli wenyewe. Na leo unakwenda kupokea uhuru wako kwani unaupata ukweli kama ulivyo. Na mara nyingi watu huwa hatukubaliani na ukweli, hasa unapokuwa unakwenda kinyume na vile tunavyoamini. Lakini hilo pia halizuii ukweli kuwa ukweli. Ukweli utabaki kuwa ukweli, iwe utakubaliana nao au la.

Ukweli kuhusu furaha na kuwafurahisha wengine ni huu, KUNA MTU MMOJA TU KWNEYE DUNIA HII AMBAYE UNAWEZA KUMFURAHISHA, NA MTU HUYO NI WEWE MWENYEWE. Hakuna mtu mwingine yeyote unayeweza kumfurahisha, kila mtu anaweza kujifurahisha mwenyewe. Hivyo achana mara moja na dhana kwamba unafanya kitu ili kuwafurahisha wengine, hakuna kitu kama hiko.

Unaweza kujifurahisha wewe mwenyewe, kwa kufanya kile ambacho unajua ni muhimu sana kwako na unajua kina mchango kwenye maisha ya wengine. Unafanya hivi kwa moyo mmoja, ukijua ndio kitu unachofurahia kufanya. Kuhusu wengine kama watafurahia au la siyo juu yako. wewe sio mhusika wa furaha zao, hivyo usipoteze muda wako kuumia na hilo.

Na uzuri wa kujifurahisha wewe mwenyewe ni kwamba unapokuwa na furaha, mahusiano yako na wengine yanakuwa bora zaidi. Na wengine pia wanakuheshimu, kwa sababu wanajua kile ambacho unafanya ndiyo muhimu kwako na unafanya kwa moyo mmoja sio kwa ajili ya kutaka kuonekana unafanya. Hapa unakuwa na furaha ya kudumu, na unakuwa na maisha bora na yenye mafanikio.

Na hata kwa kujifurahisha wewe mwenyewe, bado kuna wengi hawatakubaliana na wewe, kwa sababu hata hawajakubaliana na wao wenyewe. Hivyo hilo pia halikuhusu, wewe kazana kufanya kile kilicho bora, kile ambacho unahamasika kutoka kitandani asubuhi kwenda kufanya. Na wanaojali watajali, wasiojali hawatajali, na utakuwa na maisha bora.

Achana na harakati ambazo hazina manufaa kwa mtu yeyote, harakati kama ya kutaka kuwafurahisha wengine, wao hawatafurahi na wewe pia hutafurahi, na hata mkifurahi, furaha hiyo haidumu kwa muda mrefu, na hivyo ni kupoteza muda wa kila mtu. Chagua kuishi maisha, ambayo unajua ndiyo maisha unayotaka kuishi, maisha yenye maana kwako na wengine pia. Na kila siku kazana kuwa bora zaidi. Hapa ndipo unapotengeneza maisha bora na yenye mafanikio.

ANGALIZO; Katika kuamua kujifurahisha mwenyewe, usitafute njia za mkato, kwa sababu unaweza kujishawishi kwamba kunywa pombe ni kujifurahisha ila hujifurahishi, unajaribu tu kujidanganya, na kutengeneza matatizo makubwa zaidi. Kwa kifupi kama hujasoma makala za nyuma za falsafa hii mpya ya maisha, usifanye maamuzi yoyote kutokana na ulichojifunza leo, unahitaji kuwa na msingi sahihi kabla hujafanya maamuzi. Msingi sahihi utaleta maamuzi bora na yatakayokufanya uwe na maisha bora.

Nakutakia kila la kheri katika kutengeneza furaha ya kweli kwako na hivyo kuboresha maisha yako na yale ya wanaokuzunguka pia.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz