Ukilinganisha na vitu ambavyo tunatakiwa kujua, tunavyojua mkapa sasa ni vichache sana. Yaani ni sehemu ndogo sana ambayo kila mmoja wetu mpaka sasa anajua.

Ukiangalia kuhusu maisha, ambayo ndiyo biashara inayomhusu kila mmoja wetu, tunajua kidogo sana, bado kuna mengi ambayo ni muhimu lakini bado hatujayajua.

Tatizo sio kujua kidogo, bali tatizo ni kile kidogo ambacho tunakijua. Hiki kimekuwa chanzo cha sisi kupotea na kutokutaka kujifunza vipya zaidi.

Kile kidogo ambacho tunajua ndio kinatupoteza. Kwa sababu tunapenda kufanya kile ambacho tunajua, kile ambacho tuna uhakika nacho, kile ambacho tumezoea kufanya.

Kwa kupenda kufanya kile tunachojua, tunakataa kujifunza njia mpya ambazo zingeweza kuwa bora zaidi. Tunakataa kupokea uelewa unaoenda tofauti na tunavyoamini na hivyo kung’ang’ania kile tulichozoea kufanya.

Ni muhimu sana, kama unataka kweli kuwa na maisha bora na yenye mafanikio makubwa, ukajua ya kwamba chochote unachojua sasa ni kidogo sana na unahitaji kujifunza zaidi na kufanya kwa njia tofauti zaidi. Ifungue akili yako na usikubali kukataa kitu kwa sababu hukijui au hujazoea kufanya, chagua kuwa mwanafunzi wa maisha na jifunze kila siku na kuboresha kila siku.

Unachojua leo kinaweza kisikusaidie kesho, dunia inabailika kwa kasi sana, unahitaji kubadilika na wewe pia. Kama bado hujasoma kitabu; JINSI YA KUFAIDIKA NA MABADILIKO YANAYOTOKEA bonyeza hayo maandishi kupata kitabu hiko kizuri.

SOMA; Jambo Moja La Kukumbuka Kuhusu Mabadiliko.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba ninachojua kinaweza kunikwamisha kujua zaidi. Hasa pale ninapokuwa nimekizoea sana na hivyo kutokukubali kile kinachokwenda kinyume na nilivyozoea na kuamini. Kuanzia sasa nimechagua kuwa mwanafunzi wa maisha, nitajifunza kila siku kupitia kila kitu, na sitosita kufanya mambo mapya yenye tija zaidi.

NENO LA LEO.

“Life moves forward. The old leaves wither, die and fall away, and the new growth extends forward into the light.” – Bryant McGill

Maisha yanasonga mbele. Majani ya zamani yananyauka, kufa na kudondoka, na majani mapya yanaota na kukua kuelekea kwenye mwanga.

Usikubali kubaki nyuma, kuanguka na kupotea kabisa. Hakikisha kila siku unakua na kusonga mbele zaidi. Dunia inabadilika kila siku.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.