Hadithi inakwenda kwamba mtu mmoja alikwenda kwa Socrates na kutaka kumwambia alichosikia kuhusu rafiki yake. Socrates alikuwa mwanafalsafa aliyeheshimika sana enzi hizo za utawala wa kigiriki. Socrates alimwambia mtu yule, kabla hujaniambia chochote kuhusu rafiki yangu, naomba kwanza nikupe jaribio la machujio matatu, kuhusu habari unazotaka kuniambia.

Chujio la kwanza je hiki unachotaka kuniambia kuhusu rafiki yangu, una uhakika ni ukweli? Mtu yule alimjibu sina hakika kama ni kweli, nimesikia tu. Socrates akamwambia hivyo huna hakika na habari unayotaka kuniambia, twende chujio la pili, je unachotaka kuniambia kuhusu rafiki yangu ni kitu kizuri? Mtu yule alimjibu hapana, siyo kitu kizuri. Socrates alimwambia kwa hiyo unataka kuniambia kitu kibaya kuhusu rafiki yangu, ambacho hujui kama ni cha kweli. Twende kwenye chujio la tatu, je habari hiyo unayotaka kuniambia kuhusu rafiki yangu itakwenda kuwa na msaada wowote kwangu? Akamjibu hapana. Basi Socrates alimaliza kwa kumwambia, kama unachotaka kuniambia siyo kweli, siyo kizuri na siyo muhimu kwangu, kwa nini nikisikilize?

Kama ukiweza kuweka chujio la aina hii kwenye kila kitu ambacho watu wanataka kukuambia, utajiepusha na mengi na utaokoa muda wako wa thamani. Kwa sababu mambo mengi unayoambiwa, kuanzia habari, ni ya uongo au yamewekwa chumvi sana, yaani yamekuzwa kuliko uhalisia.

Tumia jaribio hili la machujio matatu kuchuja kila kitu kabla hakijaingia kwenye akili yako. usikubali kushiriki kwenye majungu a umbeya, au kuwa mtu wa kusambaza habari ambazo huna uhakika nazo. Kama umesikia tu kitu, amini ni uongo mpaka pale utakapodhibitisha mwenyewe. Kwa kufanya hivi utajiepusha na matatizo mengi kwenye maisha yako.

SOMA; KIPAUMBELE; Jinsi Ya Kuweka Kipaumbele Kwenye Maisha Yako.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba sio kila kitu ninachosikia ni cha kweli, na pia sio kila kitu ninachosikia ni kizuri na pia sio kila ninachosikia kina msaada kwangu. Kuanzia sasa nitapima kitu kabla ya kukubali kusikia kwa kutumia machujio matatu, JE NI KWELI? JE NI KIZURI? Na JE KINA MSAADA KWANGU? Kama majibu ni hapana, sina muda wa kupoteza.

NENO LA LEO.

Gossip is a very dangerous tool. We should be more wary of the gossiper, and not the gossip they’re trying to relay to you. John Lydon

Umbeya ni silaha hatari sana. Ni muhimu sana kuwaepuka wambeya kuliko hata umbeya wanaosambaza.

Kabla hujakubali kusikiliza chochote jiulize, JE NI KWELI, JE NI KIZURI na JE NI MUHIMU KWANGU? Kama majibu ni hapana basi huo ni umbeya, uepuke haraka sana.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.