Wewe hapo ulipo, bila ya kujali umri wako, bila ya kujali kabila lako, bila ya kujali umeanzia wapi, unaweza kufikia mafanikio makubwa sana kwenye maisha yako.
Ndiyo namaanisha wewe ambaye unasoma hapa sasa hivi, sahau kuhusu yote uliyowahi kuambiwa na wazazi, ndugu jamaa na marafiki, sahau kuhusu yote uliyoambiwa ulipofeli shuleni, kwamba kwa kufeli shule basi maisha yako hayawezi kuwa mazuri tena.
Sahau hadithi ambazo umekuwa unajipa, kwamba kwa sababu umetokea familia masikini basi hutaweza kufikia mafanikio makubwa. leo hii tutakwenda kujifunza kwa pamoja, hatua kwa hatua kanuni ya uhakika ya wewe kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako, bila ya kujali upo wapi au umetokea wapi.
Je upo tayari kwa kujifunza? Je upo tayari kuchukua hatua ili maisha yako yawe bora? Kama ndiyo naomba uniahidi kitu kimoja, kwamba baada ya hapa utakwenda kufanya kitu. Maana mafanikio yako hayatakuja kwa kujua tu, bali kwa kufanya. Je utafanya? Kama ndiyo basi karibu tuendelee kujifunza. Kama haupo tayari kufanya kitu kwenye maisha yako unaweza kuishia hapa maana hata ukiendelea hakuna kikubwa utakachonufaika nacho.

http://www.amkamtanzania.com/p/kuwa-tajiri.html

 
Hakuna hata mtu mmoja ambaye anataka kuwa na maisha mabovu, kwamba siku yake ya leo iwe mbaya kuliko ilivyokuwa jana. Kila mmoja wetu anataka kuwa bora zaidi kadiri siku zinavyokwenda. Iwe ni kwenye kazi, biashara na hata maisha ya kawaida. Lakini tupo kwenye jamii ambayo ni watu wachache sana wenye maisha bora na wengine wanazisukuma tu siku. Je kwa nini kuna tofauti hii?
Kuna hatua nne muhimu ambazo kwa kuzifuata utafanya maisha yako kuwa bora sana na hatimaye utafikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako. tutajadili hatua hizo hapa na jinsi ya kuzitumia kwenye maisha yako.
HATUA YA KWANZA; Jua ni wapi unataka kwenda au unataka kuwa nani.
Hii ni hatua ya kwanza na muhimu sana kwenye kila kitu unachotaka kufanya au unachotaka kuwa kwenye maisha yako. tumekuwa tunajadili hili mara kwa mara kwenye makala nyingine.
Ni lazima uwe na ndoto kubwa sana, ndoto ambayo inakusukuma, ndoto ya jinsi maisha yako unataka yawe, miaka mitano ijayo, kumi ijayo na hata ishirini ijayo.
Fanya ndoto hii iwe kubwa kiasi kwamba wengine wanaona haiwezekani, lakini iwe ni muhimu sana kwako kiasi kwamba kila siku na kila wakati unaifikiria ndoto hiyo.
Ukishakuwa na ndoto hii ndipo unapoweza kuweka malengo na mipango mbalimbali ya kuifikia ndoto hii. Lakini huwezi kukwepa hatua hii ya kwanza, ni lazima uwe na picha kabisa kwenye mawazo yako na jinsi unavyotaka kuwa. Kama ni biashara jione ukisimamia biashara kubwa, kama ni kazi jione ukiwa mkurugenzi wa kampuni kubwa.
Swali muhimu la kujiuliza na kujijibu hapa; je ni ipi ndoto yako kubwa? Iandike kwenye kijitabu chako cha kuandika mambo yako muhimu na kila siku ifikirie ndoto hii.
HATUA YA PILI; Jua pale ulipo sasa.
Huwezi kwenda popote bila ya kutokea hapo ulipo, hivyo ni muhimu sana wewe kujua kwa sasa upo wapi.
Kuanzia sasa chukua umiliki wa maisha yako, amua kwamba wewe ndiye kiongozi mkuu wa maisha yako, wewe ndiye wa kulaumiwa na kulalamikiwa kama mambo hayatakwenda kama ulivyopanga. Amua kwamba hakuna mtu mwingine mwenye jukumu la kufanya maisha yako kuwa bora ila wewe mwenyewe.
Na pia jua kulalamika au kulaumu wengine ni kupoteza muda wako na kutafuta sababu ya kutoroka matatizo yako. kuwa mmiliki wa chochote unachofanya au kusema, ukikosea kubali makosa yako na jifunze. Kama kuna kitu hujui jifunze haraka sana.
Unahitaji kwenda mbali zaidi ya hapo ulipo sasa, ni muhimu kujua ulipo na unaanzaje kufanya safari yako ya uhakika ya mafanikio.
Swali muhimu la kujiuliza na kujijibu; je kwa sasa ni nani mmiliki wa maisha yangu? Ni nani mwenye jukumu la kufikisha maisha yangu kwenye mafanikio makubwa? je nimekuwa nalaumu au kumlalamikia nani? Andika majibu yako kwenye kijitabu chako.
HATUA YA TATU; Jua unahitaji kufanya nini ili kufika pale unapotaka kufika.
Umeshajua ni nini unataka na umeshajua ni wapi ulipo kwa sasa. Kama ni maandalizi ya mafanikio hii ni asilimia moja tu ya kufikia mafanikio yako. asilimia 99 iliyobaki itakuja baadae.
Katika asilimia hii moja pia kuna kitu kingine muhimu sana unatakiwa kujikua. Na kitu hiki ni kujua ni nini unatakiwa kufanya ili kufika pale unapotazamia kufika. Jua ni hatua zipi unazotakiwa kuchukua ili kutoka hapo ulipo sasa na kwenda mbali zaidi.
Hapa ndipo mahali muhimu sana kwani ndiyo unafanya maamuzi ya nini unakwenda kufanya na maisha yako. hapa huna tena haja ya kuangalia wengine wanafanya nini au wanasema nini. Wewe unajua ni nini unachotaka na unakifikiaje.
Swali muhimu la kujiuliza na kujijibu; je ni hatua zipi unahitaji kuchukua ili kufikia ndoto yako kubwa kwenye maisha? Andika jibu kwenye kijitabu chako.
HATUA YA NNE; FANYA.
Hii ndiyo hatua ya mwisho, na hiki ndicho utakachofanya kwa maisha yako yote yaliyosalia hapa duniani. KUFANYA. Hapa ndipo asilimia 99 ya mafanikio yako yote imelala.
Unaweza kuwa na ndoto kubwa sana, unaweza kujua ni wapi ulipo na unaweza kuwa unajua vizuri sana ni nini unatakiwa kufanya. Ila kama hutachukua hatua, kama hutafanya kitu, hakuna kitakachobadilika kwenye maisha yako. ni lazima ufanye kitu, uchukue hatua kila siku kwenye maisha yako na maisha yako yatakuwa bora sana.
Kwa kuwa unajua kila ambacho ni muhimu, hakuna namna nyingine zaidi ya kufanya. Na kama ukifanya kitu na hukupata majibu uliyotarajia, jifunze na boresha zaidi. Isifike wakati na ukaona huhitaji tena kufanya, hapo utakuwa umeamua kujipoteza wewe mwenyewe.
Fanya, fanya, fanya. Chukua hatua kila siku ya kufanya maisha yako kuwa bora zaidi. Iwe ni kwenye biashara yako, iwe ni kwenye kazi yako, iwe ni kwenye mahusiano yako na wengine, fanya kitu, kila siku ambacho kitakusogeza karibu na ndoto yako kubwa.
Unakumbuka uliniahidi nini mwanzoni kabla hatujaanza kujadili mambo haya manne? Uliniahidi kwamba utafanya kitu, kitu chochote. Basi nakuomba sana wewe kama rafiki yangu, fanya kitu, fanya chochote. Hata kama hukubaliani na kile nilichokuambia ufanye, basi angalau fanya kitu kingine, fanya kitu, usiendelee kubaki kama ulivyo sasa, halafu utegemee kwamba maisha yako yatakuwa bora. Huko ni kujidanganya na kupoteza muda wako.
Jua ni nini unataka, jua ni wapi ulipo sasa, jua ni kipi cha kufanya ili kufika unakotaka kufika na muhimu zaidi ANZAKUFANYA. Hizi ni hatua nne muhimu zitakazokufikisha kwenye mafanikio makubwa kwa uhakika.
Nakutakia kila la kheri kwenye safari hii ya mafanikio uliyochagua. Siyo rahisi lakini inawezekana. Kama unahitaji kuambatana na wengine wanaosaka mafanikio kama wewe, karibu ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA na kupitia kundi la wasap utajifunza mengi sana kuhusu mafanikio. Kujiunga tuma ujumbe kwa wasap kwenda namba 0717396253. Karibu sana.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz