Kama ambavyo tumewahi kujifunza, hakuna ushindani ambao ni mbaya kwenye biashara kama ushindani wa bei. Huu ni ushindani mbovu sana na mara nyingi huwa nauita mbio za kuzimu. Yaani kama mnashindana kwa vigezo vya bei, kwa kuwa mara nyingi mnashindana kushusha bei, basi mwisho wa siku wote mnaishia kuwa na huduma mbovu sana na kupoteza wateja wote.

SOMA; BIASHARA LEO; Hili ndio tatizo la kushindana kwa bei na linavyokumaliza.

Katika makala hii ya BIASHARA LEO tutaangalia hatua zipi uchukue pale unapojikuta kwenye ushindani wa bei. Na haya hapa ni maoni aliyotuandikia msomaji mwenzetu juu ya hili;

Katika kipengele hiki ninajifunza mengi sana tena sana tu ila sema changamoto inayonikuta ni upangaji wa bei, hapa ninapo fanyia biashara kumekuwa na changamoto hii sana kwangu na ni mfanyabiashara mmoja tu ndiye anayenisumbua sana na kuleta upinzani mkubwa kwenye suala hili la bei.. Japo huduma zake haziko vizuri ila anapunguza sana… Kiujumla kwa suala la huduma bado hayupo vizuri ila suala la bei ndio shida… Nimejifunza mengi kuhusu biashara
Jinsi ya kupanga bei
Jinsi ya kutoa huduma bora
Kuliko wengine. Yote haya nimejifunza kupitia sehemu hii ya kisima cha maarifa
Ila naomba msaada japo ufafanuzi zaidi…. Pengine hata kwa asilimia… Kwa uzoefu wako kocha watu wanapanga bei kutoka ile waliyonunulia kwa asilimia gani jinsi utafiti wako ulivyoufanya. – Helanane.

Kama ambavyo mwenzetu amesema hapo juu, mshindani wake anashusha bei, lakini huduma zake siyo nzuri. Na hili ndilo tunalolitegemea popote ambapo bei inatumika kama zana ya ushindani. Unaposhusha bei, na hasa unaposhusha ili kumzidi mshindani wako, ni lazima utatoa huduma mbovu.

Kikubwa cha kufanya hapa ni wewe uchague, je unataka kuingia kwenye huo mtego na wewe ushushe bei, au unataka kuboresha huduma zako zaidi.

Ukishusha bei na kufika chini yake, huenda ukapata wateja kutoka kwake, ila pia huduma zako zitakuwa chini na kuna wateja ambao utawapoteza.

Kikubwa ninachokushauri ni kuuza bidhaa au huduma zako kwa bei ambayo wale wateja uliowalenga wanaweza kuimudu na wewe unapata faida. Halafu peleka nguvu zako zote kwenye kufanya huduma zako kuwa bora zaidi. Watu siku zote wanapenda kilicho bora, hivyo usiogope kwamba utakosa wateja.

Soda kwenye kibanda unauzwa mia tano, na soda hiyo hiyo kwenye hoteli kubwa inauzwa elfu tatu. Na watu bado wanakunywa soda kwenye mahoteli makubwa na hawalalamikii bei. Hivyo tatizo kubwa sana siyo bei, bali mteja anapata nini. Na usitake kupata wateja wote, pata wale ambao wanaendana na biashara yako.

SOMA; BIASHARA LEO; Ingia Kwenye Biashara Yenye Ushindani Lakini Usishindane.

Na kingine muhimu nataka nikuambie leo ni hiki, hakuna wateja wasumbufu kama wateja wanaokimbilia bei rahisi. Wanalipa kidogo lakini watakusumbua sana, na unaweza kuona maisha yako ya biashara ni magumu sana.

Chagua unataka wateja wa aina gani, wawekee bei wanayoimudu na boresha huduma zako. Mwenzako hata akigawa bure, bado wewe utapata wateja bora.

Jinsi ya kukokotoa bei ya bidhaa zako.

Kama unafanya biashara ya bidhaa, katika ngazi ya reja reja basi unaweza kukokotoa bei ya bidhaa ya kuuzia bidhaa hizo kwa kuzingatia yafuatayo;

1. Bei uliyonunulia kwa jumla, au kama umezalisha gharama za uzalishaji.

2. Gharama za kufikisha bidhaa kwa mteja, iwe ni dukani au unampelekea kwake.

3. Faida unayotaka kupata wewe kutokana na bidhaa utakayouza. Mara nyingi hii unaweza kuanza na asilimia 30.

Kupata bei ya bidhaa jumlisha gharama za kununua jumla au za kuzalisha na gharama za kuifikisha bidhaa kwa mteja, hapo unaweka gharama zote. Kisha jibu unalopata zidisha kwa asilimia 30. Kisha jumlisha jibu hili kwenye lile jibu la awali. Hivyo utakapouza bidhaa yako moja utakuwa umepata faida hiyo ya asilimia 30.

SOMA; BIASHARA LEO; Jambo Moja Muhimu La Kuzingatia Kwenye Upangaji Wa Bei.

Tumia mbinu hii ya bei kuhakikisha unaendelea kutoa huduma bora sana na unajenga mahusiano mazuri na wateja wako.

Kila la kheri.

MUHIMU; Kama una swali, maoni au changamoto yoyote ya kibiashara, weka kwenye maoni hapo chini na tutajadiliana zaidi na kama itahitajika nitaandaa makala ya kuhusu jambo hilo kwenye makala zijazo.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz