Habari za wakati huu rafiki?

Naamini uko vizuri sana na unaendelea kuyafanya maisha yako kuwa bora kila siku. Hongera sana kwa hili kwa sababu hakuna namna nyingine ya kuishi maisha ya furaha kama hayawi bora. Hivyo jukumu lako la kila siku ni kuhakikisha unakuwa na maisha bora zaidi.

Karibu tena kwenye mazungumzo yetu haya ya leo kati yangu na wewe rafiki yangu, ambapo tunashirikishana yale muhimu kwenye safari yetu ya mafanikio. Leo nataka tukumbushane jambo moja muhimu sana ambalo wengi huwa tunalisahau na linatugharimu sana baadaye.

Kuna watu ambao wanatuzunguka kwenye maisha yetu, na katika watu hawa kuna ambao wapo juu yetu, kuna ambao wako sawa na sisi na kuna ambao wapo chini yetu. Na ngazi hizi zinaweza kuwa kutokana na kazi, au kutokana na hadhi au kigezo kingine chochote kinachotumia kupima madaraja haya ya watu.

Mara nyingi mahusiano yetu na wale walioko juu yetu huwa tunayajenga vizuri, kwa sababu tunategemea kupata mengi kutoka kwao. Hivyo hapa tunakuwa wema sana, tunakuwa na heshima zaidi na kujiweka kwenye hali ambayo watu hawa wataona sisi ni bora kwao.

Kwa wale ambao tuko nao sawa, mahusiano yanaweza kuwa mazuri lakini hayafikii ya wale ambao wako juu yetu. Kumbuka hapa tunajadili jinsi wewe unavyoyachukulia yale mahusiano, jinsi unavyoyapa kipaumbele. Kwa wale wa ngazi yako unachukulia kawaida.

Sasa tatizo kubwa lipo kwa wale ambao wako chini yako, hapa ndipo mahusiano mabaya sana yalipo. Hapa ndipo wengi wanachukulia kwa urahisi sana na kuona kwa kuwa wako juu basi hawana haja ya kujali sana wale wa chini. Kwa kuwa wanawaona kama watu ambao wao ndio wanahitaji kutengeneza mahusiano bora kwao na sio namna nyingine.

Hapa ndipo ambapo tunakosea sana kwenye maisha yetu. Wewe ni mtu mmoja, iweje uishi kama kinyonga. Kwamba akiwepo fulani utakuwa mwema na mwenye heshima, kwa kuwa ni mtu wa juu yako. ila akiwepo mwingine hasa wa chini basi wema unaondoka na heshima haipo tena.

Jinsi unavyowachukulia wale ambao wako chini yako ina ishara kubwa sana jinsi maisha yako yalivyo na kama utakuwa na maisha bora.

Huwezi kuwa na maisha bora kama unaona walioko chini yako siyo wa muhimu kwako kama walivyo wa juu yako. kila mtu ni muhimu sana kwako na kila mtu ana mchango mkubwa sana kwenye mafanikio yako.

Mpe kila mtu uzito sawa, mpe kila mtu heshima sana na kuwa mwema kwa kila mtu, hata wale ambao huhitaji kuwa wema kwao. Na utaona ni jinsi gani maisha yako yatakavyobadilika na kuwa bora zaidi.

Na hili ni kwenye maeneo yote ya maisha yako, iwe ni kazi, biashara, maisha ya familia na kwingineko.

Nafikiri ulishawahi kujikuta kwenye hali hii, au umeshawahi kumwona mtu ameingia kwenye hali hii; unakutana na mtu ambaye alikuwa muhimu, lakini hukuwa umejua, na hivyo kumchukulia poa kama ilivyo kawaida yako, baadaye unagundua ni mtu muhimu sana na unaanza kuomba radhi, sikujua kama ni wewe.