Habari rafiki yangu?

Unaendeleaje na harakati za kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi?

Nina hakika uko vizuri na licha ya changamoto na vikwazo ulivyopitia, bado hujakata tamaa, unaendelea kuweka juhudi kwa sababu unajua ni kitu gani unataka kwenye maisha yako na unajua kuwa utakipata.

Lakini pia huenda umejaribu na kukutana na changamoto kisha ukaona huwezi, au haiwezekani na kuona kwa sasa utaacha kwanza na utakuja kufanya tena baadaye ukiwa umeshajipanga vizuri.

Leo nataka tujadili kiutu uzima zaidi, tuambiane ukweli halisi, yaani nyeupe tuiite nyeupe na nyeusi tuuite nyeusi.

Lakini kabla hatujaingia kwenye ukweli wenyewe, naomba nitoe tahadhari, kama hujajiandaa kuusikia ukweli utakuumiza, na utachukia, na utajisikia vibaya. Hivyo kama haupo tayari kusikia ukweli ni vyema tu ukaishia hapa, ili usije ukaumia na yale utakayoyasikia.

Kama umeshakuwa tayari kuupokea ukweli basi karibu tushirikishane hapa na uondoke ukijua kipi muhimu na ukachukue hatua sahihi.

UKWELI NAMBA MOJA..

HII GAME NI NGUMU, NGUMU, NGUMU, NGUMU.

Nimerudia mara nyingi? Nataka tu uelewe na kila siku unapoamka ujikumbushe hilo. Haya mambo siyo marahisi hata kidogo. Ni magumu mno, yaani magumu, na hivyo kama hujajitoa kweli, utaona kama maisha ni utumwa.

Mambo ni magumu kwa kuanza na wewe binafsi. kuna tabia ambazo tayari ulishajijengea huko nyuma, tabia za uvivu, tabia za uzembe, tabia za kutafuta ‘short cut’ na nyingine nyingi. Zote hizi zilikuwa zinakupa moyo kwamba mambo ni rahisi na siku yako bado tu, lakini hakuna matokeo mazuri uliyowahi kuyapata.

Sasa kama umechagua safari hii ya kuwa bora kwa kuweka juhudi na maarifa, inabidi uende kinyume kabisa na yale yote uliyokuwa umezoea kufanya.

Ulikuwa umezoea kulala mpaka usingizi uishe wenyewe, hilo unahitaji kulisahau.

Ulikuwa umezoea kukutana na watu mnapiga soga, mnaongea, mnabishana, bila ya kujali ni muda gani. Mpaka mtakapochoka au kusikia njaa ndio kila mtu aondoke, hili nalo huwezi kuendelea nalo.

Ulikuwa umezoea kujifariji kwamba wale waliokuzidi hela wana namna wanafanya, njia ambazo sio za kawaida, ndiyo maana wao wako mbali na wewe umebaki nyuma. Na kujidanganya kwamba wewe ndiyo mtakatifu zaidi, huku ukiwa hujui hata robo ya ukweli wa maisha ya wale wenzako. Hili unatakiwa kulisahau kabisa.

Ulizoea kufanya kazi kama ambavyo wengine wanafanya, hujisukumi kwenda zaidi, kwa maisha mapya hili ni sumu.

Ulizoea kushinda kwenye mitandao ya kijamii muda mwingi, kusoma kila gazeti, japo kupata habari za juu tu. Kuangalia taarifa za habari na tamthilia kwenye tv. Kwa maisha mapya hii ni sumu ya kuepuka.

Sasa huo ni ugumu unaoletwa na wewe binafsi, bado ugumu unaoletwa na wale wanaokuzunguka.

Watakukatisha tamaa, watakuambia umebadilika, watakuambia unajitenga, watakuambia huwezi, watakuambia unachanganyikiwa, watakuambia kila neno wanalojisikia kukuambia.

Na ukweli mwingine ninaotaka kukupenyezea hapa ni huu; wanaokuzunguka mara zote wako sahihi kuliko wewe. Kile unachofanya wewe siyo, kile wanachofanya wao ndio sahihi na wewe unatakiwa ufanye ili uwe sawa na wao. Hakuna mahali pagumu kama hapo.

UKWELI NAMBA MBILI;

UTASHINDWA KWA ASILIMIA 99.99..

Sitanii, siongezi chumvi, nakushirikisha tu kile ninachokiona.

Mara nyingi watu huwasiliana na mimi, wakiwa wanataka kufanya maamuzi makubwa kwenye maisha yao. Na huwa nawasikiliza vizuri na kuwahoji kama kweli wamejitoa kufanya maamuzi hayo makubwa na kama wamefikiria kwa kina madhara ya maamuzi hayo.

Na mara nyingi huwa nawapa muda, wake wakitafakari kwanza, waandike chini faida na hasara za maamuzi wanayokwenda kufanya, kisha wakimaliza tuwasiliane na kujadili kila faida na kila hasara. Kuna ambao huwa wanafanya zoezi hilo na wengine wengi huwa hawafanyi, wanaona wapo tayari kwa maamuzi. Tatizo linakuja pale wanapofanya maamuzi, wanakutana na hali ngumu kuliko walivyotegemea, na hapa wanashindwa kabisa kuendelea. Na mwishowe kurudi kule kwa mwanzo.

Ukweli ninaotaka kukupa hapa ni kwamba nafasi za kushindwa ni nyingi kuliko za kushinda.

Na sababu ziko wazi, tumezieleza hapo juu. Kuna sababu zako wewe, na kuna sababu za wale wanaokuzunguka.

Yaani kila hatua utakayojaribu kupiga, utakutana na ugumu mkubwa sana kwenye maisha yako, kama hujatafakari kwa kina na kutegemea hali kama hii, hutafika mbali, utashindwa na utakuwa nabii mzuri wa kuwaambia wengine wasijaribu kabisa kuchukua hatua kama uliyochukua wewe.

UKWELI NAMBA TATU;

HISIA NDIYO ZINAVURUGA KILA KITU.

Hisia na kufikiri ni vitu ambavyo haviwezi kwenda pamoja. Hisia zinapokuwa juu, uwezo wa kufikiria unakuwa chini.

Hisia zinavuruga kila kitu, umeweka mipango yako vizuri umeshaweka juhudi kiasi kikubwa halafu kinatokea kitu ambacho kinaumiza hisia zako, unakimbilia kufanya maamuzi ambayo ni mabovu sana kwako na yanavuruga kila kitu.

Jitahidi sana sana sana kuzidhibiti hisia zako, na sisemi uzidhibiti kwa kuzizuia, hapana huwezi kuzizuia. Kama una furaha onesha furaha, kama una huzuni ni ruhusa kuwa na huzuni na kama una hasira una haki ya kukasirika.

Lakini, nirudie tena, LAKINI, usifanye maamuzi yoyote ukiwa na hisia. Usijaribu kabisa. Wacha hisia ziondoke kwanza kisha weka jambo mezani, andika faida na hasara, chambua hasara moja moja kisha fanya maamuzi ukijua ni kipi hasa umechagua kufanya.

Mara zote kumbuka hisia zinaweza kuvuruga kazi kubwa uliyoifanya kwa muda mrefu.

GAME NI NGUMU,

UTASHINDWA KWA ASILIMIA 99.99

HISIA ZITAVURUGA KILA KITU.

Tuanze na hayo kwa leo, yatafakari vizuri, na yaweke kwenye silaha zako za kuhakikisha unafika pale unapotaka kufika.

Unapochagua hii safari elewa kabisa umeingia kwenye vita kubwa, ambayo nafasi za kushindwa ni kubwa kuliko kushinda. Na ujue ya kwamba unaweza kushinda, lakini siyo kirahisi.

Nakutakia kila la kheri katika safari hii uliyochagua, na nina hakika kama hutaishia njiani, tutakutana kwenye kilele cha ubora. Sio leo, siyo kesho, siyo mwezi, ujao, na huenda siyo mwaka ujao. Lakini lazima tutakutana, kama tu hutaishia njiani.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz