Habari za leo rafiki?

Naamini uko vizuri sana, mimi pia niko vizuri sana na naendelea kuweka juhudi kuhakikisha maisha yangu na yako wewe rafiki yangu yanaendelea kuwa bora sana. Nina hakika na kwa upande wako unaendelea kuweka juhudi, hongera sana kwa hilo.

Leo katika mazungumzo yetu haya nataka kugusia swala moja ambalo kila mtu amekuwa akipigia kelele, na kwa uelewa na uzoefu wangu, wengi wamedanganywa kwenye hili. Je na wewe unaweza kuwa mmoja wa hawa waliodanganywa? Twende pamoja kulijua hilo.

Kama unavyoelewa falsafa yangu na falsafa ya AMKA CONSULTANTS kwa ujumla, ni mtu kushika hatamu ya maisha yako. hakuna kulalamika, hakuna kutafuta sababu, badala yake ni kuchukua hatua, kuona ni kipi unaweza kufanya na ukaanza kufanya, kuona ni wapi unaweza kubadili na ukabadili. Hiki ndio tunachosimamia na kama umekuwa rafiki yangu na kuwa unasoma haya basi ni muhimu usimamie hiko.

Hivyo basi nimekuwa nikiwashauri marafiki zangu wote tuachane kabisa na haya mambo ya lawama au kulalamika. Lakini wale wasioelewa wamekuwa wakiendelea kukataa kwamba ni muhimu tuilalamikie serikali kwa sababu ina jukumu la kufanya mazingira yawe mazuri kwetu. Na mimi nawaambia ni kweli, lakini je ukishalalamika ni kipi kinabadilika kwako? Hakuna, unazidi kubaki kuwa mlalamikaji na unashindwa kuchukua hatua.

Japokuwa hii ni moja ya sehemu tunazojidanganya, lakini sio dhumuni langu la maongezi yetu ya leo.

Dhumuni la maongezi ya leo linatokana na hili.

Baada ya watu kuchukua falsafa hii ya kuchukua hatua, kwa kuamua kuacha kulalamika na kufanya kile wanachoweza, wanashindwa, wanakutana na changamoto na hapo wanakata wanaacha.

Hivyo ukimfuata kwa wakati mwingine kwamba chukua hatua anakuambia nitachukuaje hatua wakati mwanzo nilichukua na mambo yakaenda vibaya? Nilianzisha biashara na nimepata hasara kubwa sana, sina tena hata pa kuanzia. Au nimefanya kilimo lakini mvua hazikunyesha hivyo nimepata hasara kubwa. Au nimelima na kuvuna lakini sijapata soko.

Hivyo hitimisho ni kwamba sifanyi tena, kwa sababu mambo ni magumu kuliko nilivyotegemea. Au kwa sababu sina pa kuanzia tena.

Sasa hapa ndipo ninapokuja na swali langu, ni nani aliyekudanganya? Ni nani alikudanganya kwamba mambo yatakwenda kama mstari ulionyooka? Ni nani alikuahidi kwamba mambo yatakuwa rahisi na utapata kile unachotaka bila ya shinda yoyote? Kama kuna mtu alikuahidi hivyo, alikudanganya.

Nimekuwa nakusisitiza mara zote rafiki yangu ya kwamba kitu chochote chenye thamani kubwa basi pia kina changamoto kubwa. Na ndiyo maana kinakuwa na thamani kwa sababu wengi wanashindwa na ni wachache pekee wanaoweza kukomaa. Na kile chenye thamani ndogo huwa kinakuwa rahisi.

Hivyo unapoanza kufanya jambo lolote kubwa, jua kabisa kuna giza nene lipo mbele yako, jua ya kwama kuna wakati mgumu sana upo mbele yako, na jiandae kwa mambo hayo.

Japo utakuwa umejiandaa vya kutosha, lakini kuna mengi bado huwezi kuyajua mpaka pale utakapoingia uwanjani kucheza.

Kuwa na wazo zuri la biashara na ukawa na mtaji wa kuanza biashara hiyo haikupi uhakika kwamba siku ya kuanza biashara yako wateja watajipanga kugombania bidhaa au huduma zako. Una kazi nyingine kubwa ya kutengeneza wateja ambao watakuwa waaminifu kwenye biashara yako, hii siyo kazi ya siku moja, inahitaji muda.

Japo unajua kuhusu kilimo fulani na umepata eneo la kulima na una mtaji wa kuwekeza kwenye kilimo hiko, haikupi uhakika kwamba mawingu yote yatajikusanya karibu na shamba lako ili yakunyeshee mvua unayohitaji. Na wala haikupi uhakika kwamba ukishavuna basi wanunuzi watajipanga kuja kugombania mazao yako. Unahitaji kuweka kazi ya ziada kuhakikisha unapata mazao na pia kuhakikisha unapata soko la uhakika. Na mwanzoni mambo yatakuwa magumu.

Hivyo rafiki yangu mpenzi, usikubali tena kudanganywa, na wala usijidanganye wewe mwenyewe. Chochote kikubwa unachokwenda kufanya, jua utakutana na changamoto na hivyo jiandae kupambana na changamoto hizo. Au kama utakubali kurudi kwenye kundi kubwa la wasiofanikiwa, kubaliana na changamoto hizo na rudi kulalamika kwamba umejaribu lakini umeshindwa au hujawezeshwa, au chochote kitakachokupa ahueni.

Ninachotaka kukusisitiza rafiki yangu ni kwamba GAME NI NGUMU, na ni wagumu pekee wanaodumu. Ninaamini wewe ni mgumu, na ndiyo maana mpaka sasa tupo pamoja hapa.

Haya sasa hebu AMKA na uendelee kuweka juhudi, usikubali kurudishwa nyuma na chochote.

Nakuaminia.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani.

makirita@kisimachamaarifa.co.tz