Kama kuna kitu ambacho tunapambana nacho kwenye dunia ya sasa, basi ni uzalishaji wa mtu binafsi. kwa dunia ya sasa tumekuwa na mambo mengi sana ya kufanya lakini muda ni ule ule ambao ni masaa 24 kwa siku. Bila ya kuwa na mfumo mzuri wa ufanyaji wa kazi zako, unaweza kuona siku imekwisha lakini huoni ni kipi hasa ulichozalisha.
Ni changamoto hii iliyomfanya mwandishi Leo Babauta kuandika kijitabu kidogo alichokiita ZEN TO DONE. Kwenye kijitabu hiki Leo ametushirikisha mfumo rahisi wa kuweza kuongeza uzalishaji kwenye kazi zetu za kila siku.
Kumekuwa a mifumo mingi sana ya matumizi bora ya muda na kuongeza uzalishaji, lakini mifumo hii imekuwa na mapungufu kwa sababu imekuwa haigusi eneo moja muhimu sana ambalo ni tabia ya mtu. Katika mfumo huu ambao Leo anatushirikisha, unakwenda kuanzia kwenye kubadili tabia ambao ndio msingi muhimu sana katika kuongeza uzalishaji wako.
Karibu tujifunze kwa pamoja mambo muhimu kati ya mengi niliyojifunza kwenye kijitabu hiki.
Tabia kumi unazohitaji kujijengea ili kuongeza uzalishaji wako.
1. Kusanya mawazo yako yote. Kila unapokuwa kuwa na kijitabu kidogo ambacho unaweza kuandika kila wazo linalokujia kwenye akili yako. kwa kufanya hivi utaweza kuyatunza mawazo yako yasipotee, maana tunasahau haraka. Pia utapunguza mzigo kwenye akili yako na hivyo kufikiria zaidi jukumu lililopo mbele yako.
2. Fanya mchakato wa majukumu yako. kwa yale majukumu ambayo unahitaji kufanya, unahitaji kuyawekea mchakato, jua ni yapi utayafanya mara moja, yapi utawapa watu wengine wafanye na yapi ambayo utaachana nayo kabisa. Katika mchakato huu unaangalia umuhimu wa jukumu.
3. Weka mpango wa wiki na siku. Kila wiki kuna na mambo muhimu ambayo unataka kuyakamilisha kwenye wiki hiyo, zoezi hili lifanye kabla ya kuianza wiki yako. na kila siku kuwa na majukumu matatu muhimu utakayoyakamilisha siku hiyo, yapange majukumu haya kabla ya kulala.
4. Fanya jukumu moja kwa wakati, epuka usumbufu. Moja ya vitu vinavyopunguza uzalishaji ni usumbufu, hasa pale mtu anapofanya kazi na huku anafuatilia mambo kwenye mitandao. Pia kingine ni kujaribu kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja. Huku ni kupoteza muda na kupunguza uzalishaji.
5. Tengeneza mfumo rahisi wa kufuatilia mwenendo wako kila siku. Na hapa unaweza kutumia kijitabu chako kuorodhesha majukumu yako ya siku husika na kila unapokamilisha jukumu unaweka alama ya vema. Hii itakuonesha kama unakwenda sawa au la.
6. Kuwa na mpangilio mzuri wa siku yako na hata eneo lako la kazi. Pangilia majukumu yako vizuri, anza na yale ambayo ni muhimu na magumu na maliza na yale ambayo ni rahisi. Pia eneo lako la kazi liwe limepangiliwa vizuri, kila kitu kikae sehemu yake. Kufanya kazi kwenye eneo ambalo liko hovyo kunapunguza uzalishaji wako kwa sababu ukitaka kitu itakuchukua muda kukipata.
7. Fanya mapitio ya siku yako na wiki yako pia. Kila mwisho wa siku, kabla ya kupangilia siku inayofuata na kulala, pitia siku yako inayokwisha. Angalia kijitabu chako, ni majukumu yapi umekamilisha na yapi yamekushinda. Fanya hivyo pia kwenye wiki yako, mwisho wa wiki fanya tathmini ya wiki yako. kwa njia hii utajua ni wapi uko vizuri na wapi bado unahitaji kuweka juhudi.
8. Rahisisha siku yako na majukumu yako pia. Usitake kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja, au kutekeleza jukumu kubwa ndani ya muda mfupi. Kama kuna kitu unataka kukifanya, kigawe kwenye mafungu madogo madogo na anza kuyatekeleza.
9. Kuwa na utaratibu wako wa kufanya mambo ambao utautumia kila siku. Sisi binadamu ni viumbe wa tabia, tunatengeneza tabia ili ziturahisishie ufanyaji wetu wa mambo. Katika kazi zako za kila siku, jitengenezee utaratibu ambao utakuwa tabia kwako. Kwa mfano kila ukiamka unafanya kitu fulani, au kila ukifika sehemu yako ya kazi unaanza na jukumu fulani. Ukishazoea hii inakuwa sehemu ya maisha yako.
10. Jua kile unachopenda kufanya. Njia ya uhakika ya kuwa na uzalishaji mkubwa sana kwenye kazi zako, ni kufanya kile ambacho unapenda kufanya. Kwa sababu unapofanya unachopenda, unakuwa na shauku kubwa sana ya kufanya kitu hiko kwa juhudi kubwa. Kwa njia hii utakuwa na uzalishaji mkubwa sana.
Njia nane za kuweka kujijengea tabia yoyote unayotaka.
Kama ambavyo tumeona, unahitaji kujijenga tabia hizo kumi ambazo zitaongeza uzalishaji wako. Lakini kujenga tabia siyo kitu rahisi, hapa kuna njia nane ambazo Leo anatushirikisha, kwa njia hizi utaweza kujijengea tabia yoyote unayotaka.
11. Jitoe kujijengea tabia hiyo. Amua kwamba unataka kujenga tabia fulani na jitoe kwa kuwaambia watu kwamba unajijengea tabia hiyo, au unaachana na tabia ambayo hupendi. Waambie watu ili wawe walinzi wako, utakaporudi nyuma wakukumbushe.
12. Weka kwenye vitendo. Kusema tu kwamba unataka kubadili tabia ni rahisi, lakini maneno hayatabadili tabia, bali vitendo. Jijengee utaratibu wa kufanya kitu kwa siku 30 kila siku. Kila siku kwa siku 30 fanya kitu kinachokujengea tabia unayotaka kujenga. Kama ni kupangilia siku yako, basi hakikisha kila siku unapangilia siku yako kwa siku 30, ikitokea siku umeshindwa usiache, bali anza tena. Ukitimiza siku 30, utakuwa mbali sana.
13. Kuwa na hamasa. Ni vizuri ukawa na kitu kinachokuhamasisha wewe kujijengea tabia hiyo. Kwa sababu njia hiyo haitakuwa rahisi, kuna wakati utakaribia kukata tamaa, unapokuwa na kitu kinachokuhamasisha inakuwa rahisi kwako kuendelea.
14. Kuwa na njia ya kujifuatilia. Kuwa na njia ya kujifuatilia kila siku, kila siku uweze kupima umekwenda kiasi gani katika tabia yako mpya unayojijengea. Hii itakupa hamasa zaidi na kukukumbusha pale unapoanza kurudi nyuma.
15. Kuwa na watu wanaokuunga mkono. Kuwa na watu ambao wanakuunga mkono kwa tabia unaojenga au nao pia wanajenga tabia hiyo. Unaweza kujiunga na kikundi cha watu ambao wanafanya kile ambacho wewe unafanya. Kwa kuwa na watu wa aina hii watakuhamasisha kuendelea zaidi hata pale unapokaribia kukata tamaa.
16. Jipe zawadi. Unapofikia vile vigezo ambavyo umejiwekea jipe zawadi. Na zawadi hii siyo lazima iwe kubwa, bali kitu chochote kitakachokufanya uone juhudi ulizoweka ni nzuri.
17. Kuwa na umakini. Ni vigumu sana kuweza kubadili tabia nyingi kwa wakati mmoja, hivyo chagua kujenga au kubadili tabia moja tu kwa wakati, na chagua kufanya hivyo kwa siku 30. Kufanya kitu kimoja kwa siku 30 ni lazima kitakuwa tabia yako mpya.
18. Kuwa na mtizamo chanya. Kama utajiambia kwamba unaweza kujijengea tabia hiyo utaweza, kama utajiambia huwezi basi utashindwa. Kuwa na mtizamo chanya na ona inawezekana.
19. Njia ya uhakika ya kuongeza uzalishaji wako bila hata ya kuhitaji hamasa kubwa ni kufanya kile ambacho unakipenda. Na unaweza kujua kile unachopenda kwa kuangalia ni vitu gani hasa unapendelea kufuatilia kwenye maisha yako. ni vitu gani ambavyo unapenda kuvisoma sana na ni vitu gani ambavyo ukifanya kila mtu anakusifia kwamba umefanya vizuri. Angalia ni jinsi gani watu wanaweza kukulipa kwa kufanya vitu hivyo.
20. Katika kujijengea tabia ya kuongeza uzalishaji wako, unahitaji kuwa mvumilivu na king’ang’anizi. Hakuna kitu rahisi, utajaribu na kushindwa, lakini usikate tamaa, amka tena. Endelea kuweka juhudi na hakuna kitakachoshindikana.
21. Kama kazi au biashara unayofanya sasa haitokani na kile unachopenda kufanya, anza kutafuta kile unachopenda kufanya na anza kukifanya kwa pembeni. Usiache kazi au biashara yako kwa pamoja, badala yake tumia mbinu hizi za kuongeza uzalishaji kuweza kufanya kazi yako ya sasa na hiyo mpya. Ukifika wakati umeshaweka misingi mizuri ndiyo unaweza kuacha kazi yako na kufanya kile unachopenda kuwa sehemu kuu ya kipato chako.
Ongeza uzalishaji wako kwa kuanza kubadili tabia zako, jijenge tabia zitakazokuwezesha kuweka juhudi na kupata matokeo bora. Epuka usumbufu hasa wa simu na mitandao ya kijamii. Tenga muda wa kufanya kazi kwa umakini, hata kama ni mfupi, utazalisha zaidi kuliko kufanya kazi huku unasumbuliwa na simu au wengine.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Asante sana kwa uchambuzi huu wa kitabu.
Hakika tupo Pamoja.
LikeLike
Karibu sana Mahule.
LikeLike
Naomba uchambuzi wa vitabu vifuatavyo
1- The business of the 21st century
2- Secrets millionaire mind
LikeLike