Kama ambavyo nimekuwa nasisitiza mara nyingi, ushindani wa moja kwa moja kwenye biashara, ndiyo mchezo mbaya kuliko yote unaoweza kufanya kwenye biashara yako, kwa sababu utakupoteza haraka sana.
Mfanyabiashara mwenzetu aliandika maoni kutaka kujua ni viashiria gani mfanyabiashara anaweza kuwa navyo pale anapokuwa ameingia kwenye mashindano ya kibiashara.Aliandika maoni yake baada ya kusoma makala hii; Kitu Kimoja Unachoweza Kumpoteza Nacho Mshindani Wako Wa Biashara.
Haya hapa ndiyo maoni ya msomaji na mfanyabiashara mwenzetu;
Shukrani sana kwa makala hiyo kuhusu kumshinda mshindani wako.
Samahani, Siku zote umekuwa unasisitiza kuwa ni vema unapoingia kwenye biashara usishindane sasa ningependa unisaidie ni viashiria gani mfanyabiashara anaweza kuwa navyo na kudhihirisha kuwa anashindana katika biashara. Naomba unisaidie baadhi ya viashiria vinavyonyesha mtu anashindana katika biashara.
Shukrani, Peter.
Kwanza kabisa naomba nitoe ufafanuzi, sisemi usishindane, bali ninachosema ni usishindane moja kwa moja. Yaani usifanye kitu kwa sababu wengine wanafanya na kuishia pale, badala yake kazana kuwa bora kila siku. Hii ndiyo njia bora sana ya kushindana kwenye biashara yoyote utakayoifanya.
Sasa nikushirikishe viashiria vya mtu anayeshindana kwenye biashara.
1. Kufanya maamuzi ya kibiashara kwa sababu wengine nao wamefanya, na kuishia pale. Maana yake hapa ni unaangalia wenzako wamefanya nini na wewe unaiga, na hufikiri kufanya kwa ubora zaidi, unaishia pale walipoishia wao. Na hivyo hakuna kinachokutofautisha, badala yake unaumia.
2. Kupunguza bei kwa sababu wengine nao wamepunguza, na huishii hapo, wanapopunguza tena na wewe unapunguza zaidi. Mpaka wote mnaanza kuumia kwa bei ndogo.
3. Kukosa mpango wa ukuzaji wa biashara yako, na badala yake maamuzi yako yanatokana na kile ambacho wafanyabiashara wenzako wanafanya. Hapa huna mpango wowote unaotekeleza, ila ukiona wenzako wamefanya kitu fulani na wewe unafanya.
4. Kuingia kwenye biashara yoyote kwa sababu tu umeambiwa inalipa. Na wewe hujaijua kwa undani, badala yake unaangalia ni faida kiasi gani unapata, na faidia inapopungua unahamia biashara nyingine inayolipa, au unafanya kile wengine wanafanya.
5. Kuwaambia wateja wako mambo mabaya kuhusu wale wanaofanya biashara kama yako. Hapa unaamua kueneza sifa mbaya za wafanyabiashara wenzako kwa wateja wako ili wasiende kununua kwao. Na hili linakurudi kwa sababu watakwenda kujaribu na wakigundua ni uongo wanakukimbia.
Hivi ni viashiria vikuu kwamba upo kwenye ushindani wa moja kwa moja wa kibiashara na hatari ni kwamba ushindani huu hautakuacha salama.
Fanya maamuzi sahihi, weka ubora kwenye biashara yako kila siku, na utaikuza zaidi. Ushindani wa moja kwa moja utakuumiza kichwa na kuua biashara yako.
MUHIMU; Kama una swali, maoni au changamoto yoyote ya kibiashara, weka kwenye maoni hapo chini na tutajadiliana zaidi na kama itahitajika nitaandaa makala ya kuhusu jambo hilo kwenye makala zijazo.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,