Habari za leo rafiki?

Karibu tena kwenye kipengele chetu cha falsafa mpya ya maisha ambapo kwa pamoja tunakwenda kujifunza mambo muhimu kuhusu maisha ili kuweza kuyafanya maisha yetu kuwa bora, ya furaha na yenye mafanikio makubwa. maisha ndiyo kitu pekee ambacho hakuna atakayekikwepa, tutayaishi mpaka pale tutakapoacha maisha haya.

Leo tunakwenda kuangalia eneo moja muhimu sana la maisha yetu, ambalo limekuwa linatuzuia kuishi maisha bora na kuyafurahia maisha yetu. Na eneo hili ni ubinafsi wa maisha. Elewa vizuri hapa hatujadili kuhusu ubinafsi ule wa kawaida kwamba mtu ana ubinafsi na mali au vitu vingine, bali hapa tunaongelea kuwa na ubinafsi na maisha yako au ya wengine. Tutakwenda kujifunza kwa undani na kujua hatua za kuchukua.

Kabla hatujaingia ndani na kuangalia kuhusu ubinafsi wa maisha, tukumbushane hili ya kwamba binadamu ndio viumbe pekee tunaoishi huku tukiwa tunajua ya kwamba siku moja tutakufa. Yaani pamoja na yote tunayofanya lakini siku moja tutakufa, na hata wale wanaotuzunguka pia watakufa. Lakini pamoja na kujua hili, bado tunachagua kuishi maisha bora kwetu na kwa wanaotuzunguka.

Pamoja na kujua kwamba siku moja tutakufa, kuna siri moja ambayo hakuna anayeijua. Na siri hii ni siku gani hasa tutakufa, labda kwa wale ambao wanaamua kukatisha maisha yao ndiyo wanaweza kujua. Lakini wengine hatuwezi kujua kwa hakika ni siku gani tutakufa. Kwa kutokujua ni siku gani tutakufa tumekuwa tukiona kwamba muda wetu wa kuwepo hapa duniani bado ni mwingi sana. Na hapa ndipo ubinafsi wa maisha unapoanzia na kutuzuia kuwa na maisha bora.

Ubinafsi wa maisha ni nini?

Ubinafsi wa maisha ni ile hali ambayo mtu anaipata kwa kufikiri kwamba maisha yake yeye au ya watu wa muhimu kwake hayapaswi kuisha. Hapa ni pale ambapo mtu anaona yeye au mtu wa karibu kwake hastahili kufa. Licha ya kujua kwamba kila mtu atakufa, lakini kifo kinapokuwa kinakuhusu wewe au mtu unayempenda unaona kifo hakistahili.

Kwa ubinafsi huu wa maisha tunaumizwa sana na vifo vya wale ambao ni wa karibu kwetu. Na pale inapotokea kwamba hali zetu siyo nzuri na hivyo tukaona kuna uwezekano wa kufa, ubinafsi huu unatufanya tuumie zaidi na hivyo kufanya hali kuzidi kuwa mbaya.

Ubinafsi huu unawafanya watu kukata tamaa na maisha kabisa pale ambapo watu wa karibu kwao wanapofariki dunia. Wengine wanachukua maamuzi ambayo yanavuruga kabisa maisha yao ya baadaye.

Ni kweli ya kwamba kifo chochote kinaumiza, lakini tulitegemea nini? Kwamba watu waishi milele? Na pia kifo cha mtu ambaye bado umri wake ni mdogo kinaumiza zaidi. Lakini kuumia huku hakupaswi kutuzuia sisi kuendelea kuwa na maisha bora.

Unawezaje kuondokana na ubinafsi huu wa maisha?

Ili tuweze kuwa na maisha bora, ili tuweze kuyafurahia maisha ni lazima tuweze kuondokana na ubinafsi huu wa maisha. Hapa kuna njia unazoweza kutumia kuondokana na ubinafsi huu;

1. Ishi kila siku kama ndiyo siku yako ya mwisho hapa duniani.

Kila siku unayoishi, na kila kitu unachofanya, kifanye kama ndiyo mara yako ya mwisho kufanya. Fanya kama hutapata tena nafasi ya kufanya, fanya kama leo ndiyo mwisho wa maisha yako. Kwamba jua litakapozama leo, basi hutakuwepo tena hapa duniani. Kwa njia hii unahakikisha umefanya kadiri ya uwezo wako, umefanya kile ambacho umepanga kufanya na umeishi maisha ambayo watu watayakumbuka na kujifunza kupitia wewe.

Na hapa haimaanishi kwamba uishi hovyo kwa sababu ndiyo siku ya mwisho, wala haimaanishi utapanye mali hovyo kwa sababu unachukulia ni siku ya mwisho, bali weka juhudi kubwa ukijua hii ndiyo alama pekee unayokwenda kuiacha. Kama kuna mtu hujawasiliana naye muda mrefu basi wasiliana naye, kama kuna mtu umekosana naye basi patana naye, kama kuna mtu ulimkosea basi muombe msamaha.

Kwa njia hii utaishi maisha ambayo ni mazuri sana kwako na kwa wanaokuzunguka. Pia utaacha tabia ya kuahirisha mambo kitu ambacho kitakuwezesha kufikia mafanikio makubwa sana.

2. Kila unayekutana naye, chukulia kwamba hiyo ndiyo siku yake ya mwisho hapa duniani.

Kila mtu unayekutana naye kwenye siku yako, chukulia kwamba una siri moja kubwa sana kuhusu wao. Kwamba hii ndiyo siku yao ya mwisho hapa duniani, kwamba baada ya jua kuzama leo hutapata tena nafasi ya kukutana naye akiwa hai. Hivyo tumia muda unaoupata kuhakikisha unamfaidi vizuri, kama kuna kitu unataka kujifunza kwake basi jifunze leo. kama kuna kitu ulitaka kumwambia basi mwambie leo. Leo inaweza kuwa ndiyo siku ya mwisho kweli, hivyo usibaki na kitu halafu ukaja kusema ningejua.

Unapopata nafasi ya kukutana na mtu, au kuongea na mtu hakikisha umetumia muda huo vizuri kwa sababu unaweza usiupate tena.

3. Dunia haitabiriki.

Pamoja na malengo na mipango mizuri tunayojiwekea, ni lazima tujue ya kwamba dunia haitabiriki. Tunaweza kupanga mambo yetu vizuri lakini yakatokea mambo mengine na yakavuruga kila kitu. Tunaweza kuwa na mategemeo makubwa kwenye kitu fulani na mategemeo yale yakazimwa kabisa.

Hivyo ili kuepuka kukata tamaa na kuumizwa sana pale mambo tofauti na tulivyopanga yanapotokea, tuweke nafasi ya dunia kuleta mambo tofauti na tulivyotegemea. Kwa njia hii unajiandaa kupokea chochote kinachokuja na kuwa tayari kuboresha zaidi.

Kwa kuhitimisha, ili kuondokana na ubinafsi wa maisha, ni lazima tujiandae kwa wakati wowote kuondoka kwenye dunia hii. Na pia kwa wale ambao ni wa karibu kwetu, ni lazima tukubali kwamba watatuacha muda wowote. Kwa hali hii tunaweza kutumia vizuri muda wetu na ule wa wale ambao ni wa karibu yetu. Lakini pia hii haimaanishi tuishi maisha ya hovyo, bali tuendelee kuboresha maisha yetu kila siku.

Nakutakia kila la kheri katika kuboresha maisha yako zaidi kila siku.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz