Moja ya bahati kubwa ambayo kizazi hiki tumeipata ni kuishi kwenye zama ambazo kuna zana nyingi sana za kuweza kufanya kazi zetu. Na kila siku inakuja zana mpya ambayo inaweza kufanya kazi zetu kuwa bora zaidi.

Lakini pia bahati hii imekuwa kikwazo kwa watu wengi kuweza kufanya makubwa. Hii ni kwa sababu uwepo wa zana na njia nyingi mpya, unamfanya mtu ashindwe kuweka juhudi na kusingizia njia anayotumia ndiyo mbovu.

Inapotokea mtu amepanga kufanya kitu na akakifanya lakini hakupata matokeo aliyoyategemea, sehemu ya kwanza kukimbilia ni kufikiria kwamba njia aliyotumia ndiyo imemletea matokeo hayo ambayo siyo mazuri. Na kwa sababu kuna njia nyingine nyingi mpya, basi hufikiria mara nyingine atatumia njia mpya.

Na kweli wakati mwingine anatumia njia mpya, lakini pia anashindwa kupata alichotaka, na kwa sababu njia au zana zipo nyingi, anafikiria tena kutumia nyingine mpya.

Ukweli ni kwamba unaposhindwa kufikia kile unachotaka, sababu ya kwanza siyo njia au zana uliyotumia, sababu ya kwanza ni wewe mwenyewe. Ndiyo wewe mwenyewe, na kama usipoanzia hapo, utajaribu kila kitu kipya lakini utaishia kupata majibu mabaya.

Jua kwamba wewe mwenyewe unahitaji kuweka juhudi kubwa, jua kwamba wewe mwenyewe unahitaji kuweka ubunifu wa kipekee, jua kwamba wewe mwenyewe unahitaji kuwa king’ang’anizi mpaka utakapopata kile unachotaka. Na hapo ndipo njia yoyote inaweza kukusaidia.

Huwa tunafikiri kutumia njia mpya au zana mpya kunapunguza juhudi tunazotakiwa kuweka. Lakini huo sio ukweli, juhudi hazitakiwi kupungua, njia mpya inachofanya ni kuongeza uzalishaji, lakini juhudi lazima uweke kama mwanzo, juhudi kubwa sana.

Usiendelee tena kupotezewa muda kwa upya.

SOMA; Hii Ndio sababu halisi kwa nini biashara nyingi zinashindwa.

TAMKO LANGU;Nimejua ya kwamba licha ya kuwepo kwa njia na zana nyingi mpya za kufanya kazi zangu, bado juhudi zangu kubwa zinahitajika. Kutegemea upya pekee na kusahau juhudi zangu kutanipelekea kushindwa kufikia kile ninachotaka. Nitaendelea kuweka juhudi kubwa na sitosingizia kukosa njia au zana mpya kama sababu ya mimi kushindwa kufikia nilichopanga.

NENO LA LEO.

Ninety-nine percent of the failures come from people who have the habit of making excuses. George Washington Carver

Asilimia tisini na tisa ya kushindwa inatoka kwa watu ambao wanatabia ya kutafuta sababu.

Usiwe mtu wa kutafuta sababu, kuwa mtu wa kufanya mambo na yaonekane.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.