Ukimbusu mtu mwenye mafua, na wewe utapata mafua, au kama wewe una mafua, ukimbusu mtu ambaye hana mafua atayapata. Mafua yanaambukizwa kwa njia hiyo, na magonjwa mengine pia.
Lakini siyo magonjwa pekee yanayoambukizwa kwa kuwa karibu, kuna kitu kingine chenye nguvu sana ambacho pia huwa kinaambukizwa kwa ukaribu. Kitu hiko ni tabia.
Tabia zinaambukizwa, na zinaambukizwa kwa nguvu na kasi kubwa sana. Tabia yoyote uliyonayo, jua ya kwamba umekuwa unaiambukiza kwa watu wengine wanaokuzunguka. Swali ni je unawaambukiza kitu kizuri? Na kwa upande wa pili na wewe pia unaambukizwa tabia za wale ambao wanakuzunguka kwa muda mrefu. Swali ni je unaambukizwa kitu kizuri?
Ni vyema kukaa chini na kutafakari unachowaambukiza wengine na hata kile ambacho wengine wanakuambukiza, maana hivi vina michango mikubwa sana kwenye maisha yako na ya wengine pia.
Kitu kingine muhimu sana ambacho kinaambukizwa ni mtazamo. Na huu ndiyo una nguvu sana ya uambukizwaji, kama ni mafua basi haya ni ya ndege.
Umewahi kuamka siku uko na hamasa nzuri ya kufanya makubwa, umeshajipanga kuweka ubora, halafu unakutana na mtu anaanza malalamiko yake na lawama kwa wengine mpaka anamaliza unakuta na wewe umeshachoka na unashindwa kuendelea na ratiba zako? Hapo jua umeambukizwa mtazamo hasi.
Mtazamo unaambukizwa, iwe hasi au chanya, ule unaopewa nafasi unaambukizwa kwa wengine. Kama wewe ni msimamizi wa kazi na kuna watu wanafanya kazi chini yako, jaribu kujenga utaratibu wa kufanya kazi zako kwa hamasa, bila ya kulalamika au kulaumu, utashangaa baada ya muda kila aliye chini yako anafanya kwa hamasa. Lakini jaribu kufanya kwa kujivuta na kulaumu, utaona kila aliye chini yako anafanya hivyo. Hii inakwenda pia kwenye familia na hata maisha ya kawaida ya kila siku.
Tabia na mtizamo vinaambukizwa, je wewe unawaambukiza wengine nini, na je wao wanakuambukiza nini? Tafakari kwa kina kicha chukua hatua.
SOMA; Kabla Hujakazana Kubadili Tabia, Badili Hiki Kwanza….
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba nimekuwa nawaambukiza wengine tabia zangu na mitazamo yangu. Na wengine nao wamekuwa wakiniambukiza tabia zao na mitazamo yao. Kuanzia sasa nitakuwa makini na tabia ninazoambukiza wengine na zile wanazoniambukiza pia. Nitahakikisha naambukiza na kuambukizwa mambo chanya pekee.
NENO LA LEO.
Tabia na mtizamo vinaambukizwa kama ugonjwa wa kuambukiza. Unazipata tabia hizi kutoka kwa wengine na unazisambaza kwa wengine. Kuwa makini na watu wanaokuzunguka, usikubali kuambukizwa au kuambukiza wengine tabia ni mitizamo ambayo ni hasi.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.