Ukuaji wa biashara yako unategemea idadi ya wateja unaowafikia. Kadiri unavyowafikia watu wengi zaidi wenye uhitaji wa kile unachotoa, ndivyo inavyokuweka kwenye nafasi kubwa ya kufanya nao biashara.
Sasa hapa kuna maswali muhimu unayotakiwa kujiuliza ili uweze kuikuza biashara yako.
Swali la kwanza; kama umeweza kutengeneza faida kwenye eneo la sasa unalofanyia je ni maeneo gani mengine kama hayo ambapo unaweza kufanya biashara hiyo na kupata faida?
Kwa kuwa umeshayajua vizuri mazingira uliyopo sasa, je kuna mazingira mengine kama hayo ambapo unaweza kuifanya biashara hiyo na ukapata faida? Swali hili litakufanya ufikirie zaidi ya pale ulipo sasa na kuziona fursa zaidi.
Swali la pili; kama unaweza kufanya faida kwenye muamala mmoja je ni miamala mingapi kama hiyo unaweza kuifanya kwenye biashara yako? Swali hili linakuwezesha kujua huduma zaidi unazoweza kuwapatia wateja wako. Bila ya kujiuliza hivi unaweza kuwa unaacha fedha nyingi ambazo wateja wako wanaenda kupata huduma sehemu nyingine, ambazo hata wewe ungeweza kuwapatia.
Usifike wakati ukachoka kujiuliza njia mbalimbali za kuikuza biashara yako.
Kila la kheri.