Kitu Kimoja Unachopuuza Ambacho Kinagharimu Mafanikio Yako Kwenye Jambo Lolote Unalofanya.

Habari za leo rafiki?
Neno ni mafanikio, maana hiki ndio kipimo pekee kama unaishi au unasukuma siku. Na hapa sijasema mafanikio ni nini, maana kuna wengi wakisikia mafanikio moja kwa moja mawazo yanakwenda kwenye vitu. Lakini mafanikio ni makubwa kuliko vitu, ni mfumo wa maisha ambao mtu unachagua kuishi. Kwa kupigania vile ambavyo ni muhimu kwako. Kwa kusimamia kile ambacho unaamini ndiyo sahihi hata kama kila mtu anakipinga, na baadaye kunufaika sana.
Kitu kimoja kuhusu safari hii ya mafanikio ni kwamba ni safari ngumu kuliko zote hapa duniani. Kwa sababu tumezungukwa na watu wengi ambao hawayatafuti mafanikio, na hivyo kuona wale wanaotafuta mafanikio kama hawapo sahihi.

 
Pamoja na changamoto hii ya wengine, kuna changamoto kubwa ya mafanikio ambayo tunaitengeneza sisi wenyewe, na tunatengeneza changamoto hii kwa kupuuza kitu kimoja muhimu sana kwetu ili tuweze kufikia mafanikio. Leo kupitia makala hii tutaangalia kitu hiki muhimu ambacho tumekuwa tunakipuuza na hatua za sisi kuchukua ili kujihakikishia mafanikio kwenye jambo lolote ambalo tunafanya kwenye maisha yetu.
Kabla hatujaingia kwenye kitu hiki muhimu ambacho umekuwa unakipuuza, hebu tuangalie mifano hii ambayo tumekuwa tunakutana nayo kwenye maisha yetu ya kila siku;
Unakuta mtu amepanga kujenga nyumba kubwa ambayo huenda itamgharimu zaidi ya milioni 30, lakini mtu huyu anaona ni gharama sana kwake kulipia milioni moja ili apewe ramani ya kitaalamu ya kujenga nyumba yake hiyo. Badala yake anatafuta ramani ya bei rahisi, au hata ya kuiga ambayo haimpatii majibu bora kwake. Yaani mtu yupo tayari kutumia milioni 30 kujenga, lakini hayupo tayari kuwekeza milioni moja kupata msaada wa kitaalamu kwenye ujenzi wake.
SOMA; Mambo Matatu (3) Ya Kuzingatia Ili Kupata Ushauri Bora Utakaokuwezesha Kufikia Mafanikio Makubwa.
Unakuta mtu anapanga kuingia kwenye biashara, labda anapanga kuanza na mtaji wa milioni moja, au tano au kumi au ishirini. Lakini mtu huyu hayupo tayari kutoa elfu kumi ili kununua kitabu ambacho kitampa mwongozo kwenye kile anachokwenda kufanya. Au hayupo tayari kulipia elfu hamsini apate ushauri bora kwake kufanyia kazi. Au anaona kulipia laki moja na kuhudhuria semina ni gharama kubwa kwake. Anaamua kufanya mwenyewe kwa mazoea na mwishowe anafanya makosa ambayo angeweza kuyaepuka kama angefanya uwekezaji kidogo tu kwenye msaada wa kitaalamu, iwe ni kwa kusoma kitabu, au kupewa ushauri wa kitaalamu, au kuhudhuria semina.
Kwa mifano hiyo miwili naamini umeanza kuipata picha ya kitu gani tunakwenda kujadili leo.
Kitu kimoja ambacho watu wengi wamekuwa wakipuuza na kinawagharimu kwenye mafanikio ni kuwekeza kwenye msaada wa kitaalamu. Wengi huchukulia ni kitu kisicho na thamani na hivyo kuona wanaweza kupata tu bure. Kwa mtazamo huu hukosa msaada bora na hivyo kujikuta wanafanya makosa makubwa sana ambayo yanawagharimu kwa kiasi kikubwa.
Kama kuna mahali popote ambapo unataka kuwekeza fedha au muda wako, kabla ya kufanya hivyo nakushauri sana uwekeze kwenye msaada wa kitaalamu. Iwe ni kwa kutafuta vitabu vinavyohusiana na kile unachokwenda kufanya, au iwe ni kwa kulipia ushauri, au kuhudhuria semina au kupata mafunzo.
Kwa vyovyote vile hakikisha umewekeza kwenye msaada huu wa kitaalamu, ambao utakupa ujuzi kwa kile unachokwenda kufanya. Hakuna ujuzi ambao unakwenda bure, na hakuna ujuzi ambao utakuacha kama ulivyokuwa awali.
Kuna makosa mengi sana ambayo yameshafanywa na wengine, huhitaji kurudia tena makosa haya ndiyo ujifunze, badala yake unaweza kujifunza makosa hayo kwa msaada wa kitaalamu utakaoupata. Una mambo mengi sana unayohitaji kufanya, usipoteze muda huo kufanya majaribio ya vitu ambavyo ungeweza kujifunza kwa wengine ndani ya muda mfupi.
Weka kipaumbele kwenye kupata msaada wa kitaalamu, na huu utakuwa uwekezaji bora sana kwenye maisha haya ya mafanikio ambayo umeyachagua. Usioteze muda wako na fedha zako kupambana na mambo ambayo ungeweza kuelekezwa vyema na ukanufaika sana.
SOMA; Zimebaki Siku Chache Kujiunga Na Semina Ya Utoaji Wa Huduma Bora Kwa Wateja.
Zingatia sana msaada wa kitaalamu kwa jambo lolote unalofanya kwenye maisha yako, iwe ni kazi, biashara, kilimo, ufugaji na mengine mengi. Kuna mengi ambayo huyajui, ambayo kwa msaada wa kitaalamu utaweza kuyaelewa na kuyatumia vizuri kwenye safari yako ya mafanikio.
Nakutakia kila la kheri katika kufanyia kazi hili muhimu sana ulilojifunza leo, mara zote jikumbushe juu ya hili, hasa pale unapoanza kufanya kitu kipya. Na pia kwenye kile unachofanya sasa, mara kwa mara pata msaada wa kitaalamu, utakusaidia kupambana na changamoto mbalimbali unazopitia na hivyo kuweza kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako.
TUPO PAMOJA,
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
MUHIMU; Rafiki nakukumbusha ya kwamba zimebaki siku chache sana za kujiunga na semina itakayoendeshwa kwa njia ya mtandao kuhusu UTOAJI WA HUDUMA BORA SANA KWA WATEJA. Ni semina ambayo hupaswi kuikosa, itakupa maarifa muhimu ya kufikia mafanikio kwenye kile unachofanya sasa. Kushiriki semina hii tuma ujumbe kwa wasap kwenye namba 0717396253, ujumbe uwe na majina yako kamili na maneno SEMINA HUDUMA KWA WATEJA. Kumbuka ujumbe huo unautuma kwa njia ya wasap pekee, na kama huna wasap utume kwenye email amakirita@gmail.com KARIBU SANA.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: