Kabla ya kujiuliza kama jibu ulilopewa kwa swali ulilouliza ni sahihi au la, anza kujiuliza kama swali lenyewe lilikuwa sahihi.
Kwa sababu jibu unalopata linategemea na swali ulilouliza. Kama swali lipo sahihi basi utapata jibu sahihi, lakini kama swali siyo sahihi, unategemea kupata jibu gani?
Leo tunajadili hili kwa sababu tumekuwa tunauliza maswali ambayo siyo sahihi halafu tunaishia kulalamikia majibu ambayo tunayapata. Au tunapata majibu lakini hayatupatii kile ambacho tunategemea.
Mfano wa maswali ambayo tunakosea kuuliza na hivyo kupata majibu ambayo siyo sahihi.
- Nipate nini ili niwe na furaha?
Ukijiuliza swali kama hili utapata majibu mengi sana, lakini chochote utakachokipata kitakupa furaha ya muda mfupi sana, baada ya hapo utaendelea kuona kuna kitu kinakosekana kwenye maisha yako. furaha haitokani na kile unachopata, bali inatokana na vile unavyokuwa.
Hivyo swali sahihi hapo ni niweje ili niwe na furaha, au niishi maisha gani ili niwe na furaha, ni rahisi kupata majibu mazuri kwa swali hili.
- Nifanye nini ili niwe tajiri?
Hili ni swali jingine ambalo watu wengi wamekuwa wanakosea kuuliza na hivyo kupata majibu mengi ambayo siyo sahihi. Ukijiuliza ufanye nini ili uwe tajiri, utapata majibu mengi sana, kuna kuiba, kuna kudhulumu, kuna kufanya kazi kwa juhudi sana. Lakini njia nyingi zinaweza zisikufikishe kwenye lengo lako.
Hapa swali sahihi linaweza kuwa ninawezaje kuwasaidia watu wengi zaidi wenye matatizo na wao wakaniwezesha kufikia utajiri? Hili ni swali sahihi zaidi kwa sababu linakufanya uwafikirie wengine, uwasaidie kwa kile ambacho wana shida nacho na wao wakulipe halafu uwe tajiri.
Maswali ni mengi sana kwenye kila eneo la maisha yetu, hakikisha unauliza swali sahihi ili kupata majibu sahihi.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba jibu ninalopata linategemea sana swali ambalo mimi nimeuliza. Kama nikiuliza swali sahihi nitapata majibu sahihi. Lakini kama nitauliza swali ambalo siyo sahihi, hata majibu hayatakuwa sahihi. Kuanzia sasa nitakuwa naweka umakini kwa jinsi ninavyouliza maswali yangu, nitakuwa naangalia ni jinsi swali ninalouliza linakuwa na manufaa kwa wengine na siyo kwangu tu.
NENO LA LEO.
Kabla hujahoji kama jibu ulilopata ni sahihi au siyo sahihi, jiulize je swali ulilouliza ni sahihi? Kwa sababu jibu unalipata linatokana na swali ulilouliza, kama ukiuliza swali sahihi utapata jibu sahihi, na kinyume chake.
Badala ya kuuliza unawezaje kuwa tajiri, uliza unawezaje kuwasaidia watu wengi zaidi na wakakufikisha kwenye utajiri.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.