Biashara haijakamilika kama mtu hajanunua kitu. Mambo yote unayofanya kwenye biashara yako ni kwa ajili ya kukamilisha kitu hiki muhimu sana, ambacho ni kumuuzia mteja wako kile ambacho unauza. Pale mteja anaporidhika na kutoa fedha yake ili apate bidhaa au huduma unayotoa ndio biashara inakuwa imekamilika.

Katika maeneo mengi muhimu ya biashara, hili ni moja ya maeneo magumu sana. Ni rahisi mteja kusema nitanunua, ila kulipia kweli ili anunue, hiyo ni habari nyingine. Unahitaji kuwa na mbinu bora za uuzaji kwenye biashara yako. Na hata wale unaowaajiri kwenye kitengo cha mauzo kwenye biashara yako, hasa meneja mauzo kuna sifa ambazo wakiwa nazo wanaweza kufanikisha uuzaji zaidi.

Karibu leo tujifunze tabia ambazo zitakuwezesha wewe kuwa muuzaji bora. Jifunze tabia hizi na anza kujijengea zile ambazo huna. Na pale unapoajiri watu kwenye biashara yako hasa kwenye kitengo cha mauzo, angalia wenye tabia hizi na wape kipaumbele.

Kujali maslahi ya mteja.

Kuna watu ambao huwa wanajali maslahi yao wenyewe tu, wao wanachotaka ni kuuza na hawajali kama mteja atanufaika au la. Watu hawa hupata mauzo mwanzoni lakini baadaye wanashindwa kupata mauzo zaidi kwa sababu wateja hawanufaiki. Ili kuwa muuzaji bora ambaye utajenga uhusiano mzuri na wa kudumu na wateja wako, mara zote jali maslahi ya mteja wako. Ijue shida ya mteja wako na mpatie kile ambacho kitamtatulia shida yake. Na kama huna au huwezi kumtimizia anachohitaji ni vyema ukamwambia ukweli. Mteja atakuamini na wakati mwingine atakuja tena kwako. Ila kama utalazimisha kumuuzia kile ulichonacho huku ukijua hakitamsaidia, unaharibu mahusiano na mteja huyo na hatokuja tena kwenye biashara yako.

Kujiamini na kuamini unachouza.

Ili uweze kumfanya mteja aamini kweli kile unachotaka kumuuzia ni bora kwake, ni lazima wewe mwenyewe ujiamini. Unahitaji kujiamini na hivyo kuweza kujieleza vizuri na kuielezea bidhaa yako kwa mteja wako, huku ukigusia yale maeneo ambayo mteja wako atanufaika nayo kwa kutumia bidhaa hiyo ambayo wewe unataka kumuuzia. Pia unahitaji kuiamini ile bidhaa unayouza, na hapa uwe na uhakika ya kwamba kile unachosema bidhaa hiyo inafanya, basi ifanye kweli. Kama ni kitu ambacho unaweza kukitumia basi kitumie na wape wateja ushuhuda wa jinsi ambavyo bidhaa hiyo imekusaidia wewe mwenyewe binafsi. Kwa njia hii wateja watakuamini na kununua kile ambacho unakiuza.

Kutokulazimisha.

Zamani wauzaji walikuwa wanauza kama vile wanamlazimisha mtu kununua kitu. Kama hujui tabia za watu ni kwamba mtu akigundua analazimishwa kufanya kitu, atakataa hata kama mwanzoni alikuwa anataka. Angalia staili yako ya kushawishi wateja wanunue isionekane kama unawalazimisha. Badala yake wape elimu na ushauri kuhusu kile unachouza wewe na jinsi ambavyo kinaweza kuwasaidia wao kwa matatizo au changamoto walizonao. Mtu anapojua kwamba kuna kitu kinaweza kumwondolea shida aliyonayo, yeye mwenyewe atasukumwa kununua na siyo mpaka alazimishwe. Ili usiwe mlazimishaji unahitaji kujua vitu viwili kwa undani, bidhaa unayouza wewe na matatizo ya mteja wako ambayo bidhaa yako inayatatua.

Uvumilivu.

Siyo mara zote utaongea na wateja na wakasema ndiyo nanunua, wengine watakataa kununua, wengine watasema nitakutafuta. Ukweli ni kwamba utakutana na wengi ambao hawatakubali kununua kile ambacho wewe unauza. Hili halipaswi kukukatisha tamaa, badala yake inabidi iwe hamasa kwako kuboresha zaidi na kuongea na wengi zaidi. Unahitaji kuwa mvumilivu kama unataka kuwa muuzaji bora. Pale mtu anapokuambia hapana sinunui, usiumie, badala yake mwulize kwa nini, huenda akakupa jibu ambalo litakusaidia kuboresha zaidi biashara yako.

Usikivu.

Hii ni tabia muhimu sana kwenye uuzaji. Kama ambavyo tumeona, moja ya vitu unavyohitaji kujua kwa undani ni matatizo aliyonayo mteja wako ambayo biashara yako inatatua. Utayajua matatizo hayo kama utakuwa msikivu, na kusikiliza kwa makini kile ambacho mteja anaongea. Kwa kuwa msikilizaji utanufaika na mengi sana. Na siyo tu kusikiliza kwa masikio, bali pia kutumia macho kusoma tabia za mteja, ambazo pia zitakupa uelewa zaidi wa mteja. Usikivu ni tabia ambayo itakuwezesha kuwa muuzaji bora kwa kujua vyema kuhusu wateja wako.

Jifanyie tathmini na uone ni tabia zipi kati ya hizo ambazo tayari unazo na zipi ambazo huna. Baada ya tathmini hiyo chukua uamuzi wa kujijengea tabia ambazo huna. Kwa mfano kama siyo msikivu, basi anza kujijengea tabia ya usikivu. Mtu anapoongea weka mawazo yako yote kwenye kumsikiliza, usifikirie unamjibu nini na wala usimkatishe, badala yake msikilize vizuri, elewa na kisha mpe majibu sahihi kwake. Mauzo ni nguzo muhimu ya biashara yako, hakikisha unaiboresha nguzo hii kwa kuwa muuzaji bora, au kutengeneza timu bora ya uuzaji.