Inawezekana hapo ulipo ukawa huna kazi ama unakazi ambayo unaona haikuingizii kipato cha kutosha. Inawezekana pia kutokana na sababu hizo ukawa una shauku kubwa ya kutaka kuanzisha biashara ambayo itakulipa. Na inawezekana tena umekuwa ukijiuliza maswali mengi ufanye nini au ufanye bishara gani ambayo kwako itakuingizia pesa nyingi na kwa muda mfupi.
Hayo ni baadhi ya maswali machache kati ya mengi ambayo naamini umekuwa ukijiuliza sana kutaka kujua, ni biashara gani ambayo inaweza kuwa ya manufaa kwako zaidi. Naamini pia kwa maswali hayo umekuwa ukitafuta kama mwongozo wa kukusaidia kufanikiwa kibiashara pale utakapoanza. Kama nia na lengo lako ni hilo uko sawa. Nimesema hivyo nikiwa na maana kwamba, biashara yoyote utakayoianza ili iweze kufanikiwa ni lazima ujue kwanza mambo ya msingi ya kukusaidia kufanikiwa.
Watu wengi kutokana na kutokujua mambo hayo mapema au kukosa mwongozo huo sahihi hujikuta kila wanapoanza biashara huwa ni watu wa kushindwa sana. Leo hii utakuta mtu huyo yupo kwenye biashara hii au kesho ile ilimradi tu yupo yupo na ukichunguza, hakuna mafanikio makubwa anayokuwa anayapata. Tatizo kubwa linalopelekea hali hiyo ni kule kwa wao kutokujua mambo ya msingi yatakayowapa mafanikio, hasa pale unapoanza biashara.
Leo kwa kusoma makala haya, utajifunza mambo haya muhimu yakukusaidia kuanza bashara yako kwa mafanikio makubwa. Bila shaka yoyote, kwa kujua mambo haya yatakusiadia kufanya biashara yako kwa ushindi . Ile hofu ya kusema kwamba naweza nikashindwa kwa namna moja au nyingine naweza sema utakuwa umeipunguza kwa kiasi kikbwa. Najua unajiuliza tena mambo hayo ni yepi ya kuyajua kabla ya kuanza kufanya biashara? Toa shaka na twende pamoja sasa kujifunza.
1. Pata uzoefu.
Kabla hujaanza kufanya biashara unayotaka kufanya kitu cha kwanza unachotakiwa utambue ni lazima upate au ujenge uzoefu kwenye biashara hiyo. Nikiwa na maana kwamba biashara unayoiendea kuifanya ni lazima uijue ndani nje kwa sehemu kubwa sana . Bila kuwa na uzoefu angalau kidogo sio rahisi sana kuweza kufanikiwa kwa biashara inayotaka kuifanya au kuiendea. Ni lazima utaanguka tu ikiwa utaingia kichwa kichwa bila kuijua biashara hiyo vizuri.
Kwa mafano unataka kuanzisha duka la vipodozi, pata uzoefu kwa kuwatembelea watu wenye maduka yenye vipodozi . Lakini hiyo isiishie hapo utatakiwa pia uwaulize maswali ya kutosha ili kujijua biashara hiyo vizuri. Pia kama unataka kufanya kilimo cha aina fulani ni lazima sana kuwatembelea wataalamu wa kilimo hicho ili kujifunza. Kwa kufanya hivyo utajenga uzoefu na itakusaidia kuanza biashara yako kwa mafanikio makubwa.
Anza biashara yako kwa mafanikio.
2. Jiwekee malengo ya kibiashara.
Kabla hujaanza biashara yako ni vyema ukatambua malengo uliyonayo kwenye hiyo biashara. Ni lazima ujiulize unataka kufika wapi kwenye hiyo biashara? Unataka kuwa mfanyabiahara mdogo wa kawaida? Au unataka kuwa mfanyabiashra mkubwa. kwa kujiuliza maswali kama hayo na mengineyo mazito yatakufanya ufanye biashara yako kwa ukomavu mkubwa.
Kwa kuwa utakuwa umeshajua malengo yako ya kibiashara ni wapi unapotakiwa kufika, endelea kuwekeza nguvu zako nyingi huko. Tambua ni baada ya mwaka mmoja au miwili utakuwa wapi. Kwa kujiwekea mahesabu kama hayo itakusaidia sana kuweza kufanya biashara yako kwa ushindi kwa sababu ya kuweka juhudi nyingi bila kuchoka. Kwa juhudi hizo utajikuta umekuwa mshindi.
3. Tengeneza mtandao wako.
Kabla hujaanza biashara ni lazima ujue mtandao vizuri utakaoweza kukusaidia kufanikiwa. Ukijijengea ‘netwek’ yako nzuri ya kibiashara itakupa mafanikio makubwa na itakuwa ni njia bora ya kisasa ambayo umeichagua kuitumia kukuza biashara. Lakini hata hivyo si njia tu ya kisasa pia wengi hawaitumii, nikiwa na maana hawana mtandao.
Kwa mfano, unapokuwa na mtandao wako mzuri, mara nyingi mtandao wako huo unakusaidia kuifanya biashara yako kuwa juu hata katika kipindi soko linapokuwa limeshuka au baya kabisa. wale watu ambao upo nao kwenye mtandao mmoja ndio itakuwa chanzo cha kukuza na kutangaza iashara yako vizuri. Angalia biashara za mitandao au ‘netwek marketing’ nyingi zinafanya vizuri kwa sababu ya mtandao walioweka waanzilishi wake.
4. Wajue washindani wako vizuri.
Ni vyema kabla hujaanza biashara yako, weka mikakati ya kuwajua washindani wako na pia elewa jinsi ya kukabiliana nao. Kitendo cha kuwajua washindani wako kitakusaidia sana kujipanga vizuri kwa ajili ya kutoa huduma bora na hata kuweza kumudu soko kwa uhakika. Lakini ikiwa utaingia kwenye biashara bila kujua wapinzani wako itakusumbua kidogo kufanikiwa.
Kumbuka kwamba kabla hujaanza biashara yako ni lazima upate uzoefu, uwe na malengo mazuri ya kibiashara, jiwekee mtandao na bila kusahau ni lazima kuwajua washindani wako. Kwa kuyajua mambo haya manne kwa vyovyote ni lazima utakuwa mshindi kwenye biashara yako.
Kwa makala nyingine za mafanikio tembelea DIRA YAMAFANIKIO kwa kuboresha na kuimarisha yako.
Nikutakie kila la kheri na endelea kujifunza kupitia AMKA MTANZANIA kila siku.
Ni wako rafiki,

Imani Ngwangwalu,
Simu;-0713 048035,

Blog;dirayamafanikio.blogspot.com