Kwenye dunia tunayoishi sasa, kila unachofanya, kusema au kuandika, kuna watu wanakurekodi.
Unahitaji kulijua hili na kuwa makini sana kwa sababu ulichosema au kuandika kinaweza kutumika kama ushahidi dhidi yako.
Hakuna wakati ambao inalipa kuwa mwadilifu kama zama hizi, maana kila kitu kipo wazi kabisa. Unaweza kufanya kitu ukijua ni siri au umejificha, lakini utashangaa siku kipo hadharani.
Kuhakikisha unakuwa salama, usifanye, usiseme wala usiandike jambo lolote ambalo usingekuwa tayari kufanya kama ingekuwa linaripotiwa kwenye kurasa za mbele za magazeti.
Mitandao ya kijamii imerahisisha sana kuwashirikisha wengine mawazo yetu na hata hisia zetu, lakini kila unachoandika kinahifadhiwa na wengine na kinaweza kutumika dhidi yako.
Mawasiliano ya simu yamerahisisha sana kuwasiliana, lakini pia unapoongea na mtu anaweza kukurekodi na kutumia ulichosema dhidi yako.
Hata unapokutana na mtu katika mazungumzo ya kawaida tu, anaweza kuchagua kukurekodi, na huwezi kujua ni wakati gani mtu anafanya hivyo.
Njia salama ni kuchukulia kama kila unachofanya watu wanakurekodi, na hivyo kuepuka kufanya yale ambayo usingependa wengine wayasikie au wayaone kwamba ni wewe umefanya.
Kuwa mwaminifu na kuwa mwadilifu kwenye kila unachofanya, dunia nzima inakuangalia, haijalishi unafanya kwa kificho kiasi gani.
SOMA; Hivi Ndivyo Mitandao Ya Kijamii Inavyoharibu Akili Yako, Kuwa Makini.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba dunia inanirekodi kwa kila inachofanya, kuandika au kusema. Najua hakuna tena siri kwenye dunia ya sasa, teknolojia imerahisisha sana zoezi la kurekodi. Kuanzia sasa nitafanya mambo yangu kama vile kila mtu anaangalia na kwa njia hii nitaepuka kufanya mambo ambayo yanaweza kutumika dhidi yangu hapo baadaye.
NENO LA LEO.
Kwenye kila kitu unachofanya, unachosema au unachoandika, dunia nzima inakuona. Hakuna tena siri kwenye dunia hii ya utandawazi na teknolojia.
Kila unachofanya, chukulia kwamba watu wanakurekodi na wanaweza kutumia dhidi yako, na hivyo fanya mambo yako kwa uaminifu na uadilifu. Hakuna tena siri, kila unachofanya kitawafikia wengine.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.