Jana tarehe 01/05/2016 ilikuwa siku ya wafanyakazi duniani. Wafanyakazi kila kona ya dunia walikuwa wakiadhimisha siku yao na kuonesha michango yao kwenye ukuaji wa uchumi na changamoto zao pia.
Kuna mengi ya kujadili kwenye siku hii ya wafanyakazi, kuanzia chimbuko lake na harakati ambazo wafanyakazi wamepitia mpaka kufikia kuanzishwa kwa vyama vya wafanyakazi. Lakini hapa hatutajadili hayo, bali tutajadili upande ambao wengi huwa hawauangalii, ambao ni ukweli unaoumiza, na kama ilivyo tabia yetu binadamu kama ukweli unaumiza basi hatutaki kabisa kuujadili.
Kwa kuwa lengo langu ni kukushirikisha wewe maarifa ambayo yatakuwezesha kuwa bora zaidi na kuweza kufikia mafanikio kwenye maisha, sina budi bali kukueleza ukweli na kama utakuumiza ni vizuri ili uweze kuchukua hatua.
Kabla hatujaangalia mambo haya kumi ya ukweli ambayo yanaumiza, ni vyema tukakumbushana ya kwamba mambo yamebadilika sana kwa sasa, nafasi za kazi zimekuwa chache huku wanaozitaka wakiwa wengi. Hii imefanya ile thamani ya kazi iliyokuwepo mwanzo kushuka sana kwa sasa. Na pia ni vyema tukatambua ya kwamba licha ya kuwepo kwa changamoto kwenye ajira, bado wafanyakazi wana mchango mkubwa sana kwenye ukuaji wa uchumi na hata kwa sisi wananchi kupata mahitaji yetu.

 
Mambo kumi ya ukweli ambayo waajiriwa hawapendi kuyasikia;
1. Mshahara haujawahi kutosha na hatakuja kutosha.
Nafikiri hili liko wazi kwa kila mmoja japo hatupendi kulisikia mara kwa mara. Ukiangalia kila sehemu ya kazi, mwenye mshahara mdogo na mwenye mshahara mkubwa, inapofika mwisho wa mwezi wote wana kilio kimoja, hawana fedha na wanasubiri mshahara utoke. Kadiri mshahara unavyoongezeka ndivyo mahitaji nayo yanaongezeka. Hali hii imekuwa inawafanya waajiriwa kuishi maisha ya mzunguko wa kukopa, kupokea mshahara na kulipa madeni halafu kuanza tena kukopa.
SOMA; Sababu Tatu(3) Zinazokuzui Kufanikiwa Kwenye Kazi Unayofanya.
2. Mfanyakazi ndiye mtu pekee ambaye hawezi kukwepa kodi.
Mwajiriwa anakatwa kodi kabla hata hajapokea mshahara wake, hivyo hakuna njia yoyote ambayo anaweza kuitumia kukwepa kulipa kodi. Kwa wafanyabiashara, wana njia nyingi za halali kabisa za kukwepa kodi, kadiri biashara yake inavyokwenda, anaweza kuwa na sababu nyingi zinazopelekea yeye kukatwa kodi ndogo kulingana na mahesabu yake. Lakini kwa mfanyakazi, unalipa kodi ile ile bila ya kujali matumizi yako yameongezeka au yamepungua.
3. Unaadhibiwa kwa kuwa na kipato kikubwa.
Kadiri mshahara wako unavyoongezeka ndivyo kodi yako inavyozidi kuwa kubwa. Mwenye mshahara kidogo anakatwa kodi kidogo, mwenye mshahara mkubwa anakatwa kodi kubwa, na yule ambaye mshahara wake ni mkubwa zaidi, anakatwa kodi kubwa zaidi kwenye ile ziada ya kipato chake. Inaumiza sana hii.
4. Mwajiri wako hakupendi.
Hili unaweza usilielewe vizuri lakini ni ukweli unaoumiza. Mwajiri wako hakupendi kama unavyofikiri anakupenda, anakutumia katika kukamilisha ndoto zake. Na ndiyo nakubaliana na wewe kwamba mnasaidiana, lakini subiri siku ambayo mwajiri wako anapata hasara, anachofanya ni kukupunguza wewe mfanyakazi. Kama angekuwa anakupenda, mngekuwa pamoja kwenye shida na raha, ila hakupendi, anakutaka wakati unamtengenezea faida tu.
5. Maamuzi ya mtu mmoja yanaweza kuharibu kabisa maisha yako.
Ni ukweli unaoumiza na kusikitisha ya kwamba unapokuwa kwenye ajira huna udhibiti wa moja kwa moja kwenye maamuzi ya kazi yako. na maamuzi ya mtu mmoja, ambaye ni bosi wako, yanaweza kuharibu kabisa maisha yako, hasa pale unapoitegemea kazi yako kuendesha maisha yako.
SOMA; Hii Ndio Kazi Inayolipa Sana Ambayo Hata Wewe Unaweza Kuifanya.
6. Huwezi kufikia uhuru wa kifedha kwa kutegemea ajira pekee.
Kwa kutegemea ajira pekee kama chanzo chako cha kipato, huwezi kufikia uhuru wa kifedha. Na uhuru wa kifedha ina maana kwamba hufanyi tena kazi ili kupata fedha ya kuendesha maisha. Kwenye ajira unaishi mwezi kwa mwezi. Unahitaji jitihada za ziada kujitengenezea uhuru wa kifedha.
7. Ukuaji wa teknolojia unatafuna ajira nyingi.
Sijui kama unajua, ila huko duniani kwa sasa watu wanaumiza akili kutengeneza maroboti ambayo yataweza kufanya kila kitu. Kuanzia kufanya upasuaji wa miili ya binadamu, kucheza michezo, kuburudisha na kuzalisha. Sasa hivi makampuni mengi yanatengeneza magari yanayojiendesha yenyewe. Najua utasema ni muda mpaka haya yafike huku kwetu, lakini kumbuka kuna watu walisema kompyuta zitachukua muda kufika, na sasa zipo hapa na zimechukua ajira za watu wengi.
8. Daraja la kati limekufa.
Zamani wafanyakazi wengi walikuwa wanaishi kwenye daraja la kati katika madaraja ya kimaisha. Ila kwa sasa daraja la kati limeshapotea kabisa, limebaki daraja la chini ambapo kuna masikini wasiokuwa na uhakika na mwezi unaofuata na kuna daraja la juu la matajiri ambao wana uhuru wa kifedha. Kama unategemea ajira pekee, utaendelea kubaki daraja la chini, ambapo unaishi mkono kwenda mdomoni, yaani kula kile unachopata na kuanza kutafuta tena.
SOMA; Je Watanzania Tunaiweza HAPA KAZI TU? Haya Hapa Ni Mabadiliko Ya Wewe Kufanya Kwenye Kazi Zako.
9. Majungu yatakuzidishia msongo wa mawazo.
Kama kuna sehemu ambayo imejaa majungu basi ni kwenye ajira, hasa kwenye hizi nchi zetu ambazo bado watu wengi ni masikini. Kwa maisha kuwa magumu wafanyakazi wanaanza kuona wabaya wao ni wafanyakazi wenzao na hivyo mchezo wa majungu unaanza. Majungu haya yamekuwa yanawaumiza wengi na kuwaletea msongo wa mawazo.
10. Unapostaafu unakaribisha kifo.
Tafiti nyingi zinaonesha ya kwamba watu wengi wamekuwa wakifariki miaka mitano baada ya kustaafu kazi zao. Na hili linachangiwa na mabadiliko makubwa ya kimaisha ambayo mtu anayapitia kwenye kipindi kifupi. Kwanza watu wanapostaafu, ule mshahara waliokuwa wanategemea unakauka. Na hatari zaidi inatokana na mafao ambayo mstaafu anapata, kwa kukosa maandalizi bora anafanya makosa kwenye uwekezaji na hivyo kupoteza fedha zote, hili huchangia wengi kupoteza maisha mapema.
Ufanye nini kama wewe ni mwajiriwa?
nimekukumbusha hayo mambo 10 siyo kwa ajili ya kukuumiza au kukubeza, bali kwa ajili ya kukukumbusha hatua muhimu za kuchukua. Na wala sikuambii uache kazi leo kwa sababu inakuumiza, bali nataka nikupe mpango mzuri kwako kununua uhuru wako. Nimeanika kitabu kinaitwa BIASHARA NDANI YA AJIRA. Kitabu hiki kimejadili kwa kina jinsi unavyoweza kuanza na kukuza biashara yako ukiwa bado umeajiriwa. Pia kuna mifano ya biashara unazoweza kufanya na uwekezaji muhimu kwako kufanya. Endelea kutembelea AMKA MTANZANIA  na utapata taarifa kitabu hiki kitakapoanza kupatikana.

TUPO PAMOJA,
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz