Tangu zamani kumekuwa na njia kuu mbili za kutengeneza au kurekebisha tabia. Njia hizi ni za kisaikolojia na zimekuwa zinaleta majibu mazuri lakini pia zisipotumiwa vizuri zinaleta majibu mabaya.

Njia hizo mbili ni Tuzo/zawadi na Adhabu.

Tuzo/zawadi;

Hapa mtu anatuzwa au kupewa zawadi kwa kitu kizuri alichokifanya. Mtu anatambuliwa kwa kitu kizuri na kikubwa ambacho amefanya. Lengo la tuzo ni kutengeneza tabia nzuri. Yule anayeipata na wengine wanahamasika kuwa na ile tabia ambayo imepelekea mtu kupewa tuzo.

Adhabu;

Hii hutolewa pale mtu anapofanya kitu ambacho siyo kizuri au hakikubaliki. Hapa mtu anaadhibiwa kwa kwenda kinyume na taratibu ambazo zipo kwenye eneo fulani. Lengo la adhabu ni kurekebisha tabia mbaya. Yule anayeadhibiwa na wengine waone kwamba kufanya kitu ambacho hakikubaliki ni kitu kibaya na hivyo kuepuka kufanya.

Changamoto;

Changamoto kwenye tuzo na adhabu inakuja pale vitu hivi vinatolewa kwa asiyestahili au kwa mtu aliyetumia njia ambazo siyo sawa kwake kupata vitu hivyo.

Changamoto ya tuzo ni pale ambapo mtu asiyestahili anapewa, au mtu anatumia njia zisizo nzuri kupata tuzo. Hapa ujumbe unaoenda kwa wengine ni tofauti na wao watakazana kutumia njia isiyo sahihi ili nao wapate tuzo.

Changamoto ya adhabu ni pale mtu anapotumia njia zisizo sahihi kuepuka adhabu ya kosa ambalo amefanya. Hapa wengine wanapata ujumbe kwamba wanaweza kufanya kosa lakini wakaepuka adhabu. Au ikitokea adhabu imetolewa kwa asiyestahili, inaharibu kabisa kile ambacho kinatakiwa kujengwa.

Bila ya kuwa makini, tuzo na adhabu vinaweza kuharibu mfumo mzima wa kutengeneza tabia njema na bora kwa jamii zetu. Hii ni kuanzia kwenye familia yako, kwenye biashara yako na kwenye kazi yako. kuwa makini unapotoa tuzo au adhabu, hakikisha unatoa ujumbe sahihi na wengine wanajifunza njia sahihi.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; Why Motivating People Doesn’t Work And What Does. (Sayansi Mpya Ya Hamasa Na Uongozi)

TAMKO LANGU;

Najua ya kwamba tuzo na adhabu ni njia nzuri za kujenga na kurekebisha tabia. Nimejua ya kwamba kutokuwa makini kwenye utoaji wa vitu hivi viwili kunaweza kuharibu sana kuliko kunavyojenga. Nitakuwa makini katika utoaji wa tuzo na adhabu kwenye familia, kazi na hata biashara zangu ili kuweza kujenga tabia bora za kufanya maisha kuwa bora zaidi.

NENO LA LEO.

Tuzo na Adhabu ni njia mbili ambazo zimekuwa zinatumia kutengeneza na kurekebisha tabia. Wanaofanya vizuri wanatuzwa au kupewa zawadi na wanaofanya vibaya wanaadhibiwa.

Iwapo njia hizi mbili hazitatumika vizuri zinaharibu zaidi kuliko zinavyotakiwa kujenga. Hakikisha Tuzo inatolewa kwa tabia inayostahili na mfano unaofaa kuigwa na adhabu inatolewa kwa kosa linalostahili na wengine waepuke kosa hilo.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.