Mbinu Saba(7) Za Kuongeza Ushawishi Wako Kwa Wengine Na Kupata Chochote Unachotaka.

Chochote unachotaka kwenye maisha yako, unakipata kutoka kwa wengine. Ndivyo dunia ilivyo na ndivyo itakavyoendelea kuwa. Hii ina maana kwamba mafanikio yako utayapata kupitia watu wengine. Hivyo mahusiano yako na wengine ni muhimu sana kwa mafanikio yako.
Kama unafanya biashara, wateja wako ni watu wengine, kama umeajiriwa bosi wako ni mtu mwingine, kama umeajiri wafanyakazi wako ni watu wengine. Na hata kwenye familia unakutana na watu wengine, ambao mnahitaji kuweza kwenda pamoja.
Moja ya vitu vigumu kwenye maisha ni kuweza kuenda vizuri na watu wengine. Ni changamoto kubwa sana kuweza kuwashawishi watu kufanya kile ambacho unataka wafanye. Na hivyo unahitaji kuwa na mbinu bora za kuweza kuwashawishi wengine ili wafanye kile ambacho unajua ni muhimu kwao na kwako pia.
Kupitia makala hii tutajifunza mbinu saba unazoweza kutumia kuongeza ushawishi wako kwa wengine na kupata chochote unachotaka. Lakini kabla hatujaanza kuangalia mbinu hizi elewa wazi kwamba hapa hatujifunzi jinsi ya kuwaendesha wengine, kuwafanya watupe kile tunachotaka bila ya kujali wao wananufaikaje. Hizi ni mbinu ambazo zitawanufaisha wengine na kukunufaisha wewe pia.

 
Zifuatazo ni mbinu saba za kuongeza ushawishi wako kwa wengine na kupata chochote unachotaka.
 
1. Jali kuhusu maslahi ya wengine.
 
Japokuwa wewe unataka kupata unachotaka, bado hutaweza kukipata kwa kulazimisha au kuwaendesha wengine. Njia muhimu ya kuwashawishi ni kujali kuhusu maslahi yao. Unapojali maslahi ya wengine, na hivyo kufanya mambo ambayo yatawakuwa yanawanufaisha wao, watashawishika kufanya kile ambacho unawataka wafanye.
Kujali huku kuhusu maslahi ya wengine kusiwe ni kwa muda tu, kwa sababu watu wanaweza kulisoma hilo. Inabidi kuwe halisi, yawe ni maisha ambayo umechagua kuishi na utajenga mahusiano bora na wengine.
SOMA; Huu Ndiyo Umuhimu Wa Kuwa Na Shukrani Kwenye Maisha Yako.
 
2. Tabasamu.
 
Hiki ni kitu kidogo ambacho kinaweza kuleta mabadiliko makubwa sana kwenye maisha yako na ya wengine. Sura yenye tabasamu inawavutia wengi kuliko sura isiyokuwa na tabasamu. Unapotabasamu watu wanajiona salama kuwa na wewe na kukuchukulia kama rafiki. Tabasamu lako linaongeza ushawishi wako kwa wengine. Kuna sababu kwa nini sheria muhimu ya wafanyakazi wanaohusika na huduma kwa wateja wanatakiwa kutabasamu hata kama wanaongea kwa simu. Tabasamu linajulikana na linaongeza ushawishi.
 
3. Kumbuka majina ya watu na yatumie.
 
Hakuna kitu ambacho mtu anapenda kusikia kama jina lake. Unapokumbuka jina la mtu na kulitumia mtu anajisikia vizuri na kukuchukulia wewe kama mtu unayejali sana kuhusu yeye. Unapoongea na mtu tumia majina yake kamili na kwa usahihi, atakusikiliza vizuri na atashawishika kufanya kile ambacho unataka afanye, ambacho pia ni muhimu kwake.
 
4. Kuwa msikilizaji mzuri.
 
Sikiliza. Hii ni mbinu bora ambayo itaongeza ushawishi wako kwa kiasi kikubwa sana. Watu wanapenda sana pale ambapo wanasikilizwa. Hivi unajua sasa hivi hakuna watu wanaosikiliza kabisa, kila mtu anataka aongee na kama haongei anafikiria atajibu nini. Unapoacha hayo na kuamua kusikiliza kwa umakini, kwanza yule anayeongea atajisikia vizuri na pia utasikia mambo ambayo yatakusaidia kuongeza ushawishi wako. Watu wanasema mambo mengi, wanatoa maumivu yao, ukiwa makini kusikiliza utapata mengi yatakayokusaidia katika kuongea ushawishi wako.
 
5. Wahamasishe wengine kuongea kuhusu wao.
 
Hakuna kitu watu wanapenda kama kujieleza wao binafsi, kusema ni mambo gani wamefanikisha kufanya, ni jinsi gani wamefanya vizuri na hata mafanikio yao. Wahamasishe watu kujizungumzia wao wenyewe, na unaweza kufanya hivi kwa kuwauliza kuhusu mafanikio yao au vitu wanavyovipenda. Halafu ukawasikiliza kwa makini. Wanakuchukulia wewe kama rafiki muhimu kwao na watakubaliana na wewe kwa kile unachotaka wafanye.
 
6. Ongea kwa maslahi ya wengine.
 
Unapopata nafasi ya kuongea, usiongee kuhusu wewe au kuhusu kile unachofanya, bali ongea kwa maslahi ya yule unayetaka kumshawishi. Kama unataka kumuuzia mtu kitu, usianze kumwambia kitu hiko kimeshindaje vitu vingine, bali mweleze ni jinsi gani kitu hiko kitamsaidia yeye kuwa na maisha bora au kuondokana na changamoto alizonazo yeye. Mtu anaposikia kitu kinachomhusu yeye binafsi, anakuwa makini zaidi na atachukua hatua.
 
7. Mfanye mtu mwingine ajisikie wa muhimu, na fanya kwa uaminifu.
 
Kila mtu anataka kuonekana ni wa muhimu, na hivyo kama ukiweza kumfanya mtu akajiona yeye ni wa muhimu, atashawishika kufanya kile unachomtaka yeye afanye. Chukua mfano kwenye kauli kama kwetu mteja ni mfalme, ni kauli ndogo sana lakini mtu anapoisikia anapata picha kwamba pale atajaliwa na kuonekana wa muhimu kama alivyo mfalme. Tafuta njia za kumfanya mtu ajione yeye ni wa muhimu, na usifanye hivi kwa kuigiza, bali fanya kwa uhalisia.
Mbinu hizi sana siyo za kutumia moja na kuacha nyingine, bali ni za kutumia kwa pamoja. Yaani zitumie zote kwa pamoja na utakuwa na ushawishi mkubwa sana. Unapojali maslahi ya wengine, ukatabasamu, na kuwasikiliza kwa makini wanapoongea, ukatumia majina yao na kuongea kwa maslahi yao huku ukiwafanya kuwa wa muhimu, watashawishika kuchukua ile hatua ambayo unataka wachukue.
Fanyia kazi mbinu hizi sana na utaongeza ushawishi wako kwa wengine na kuimarisha mahusiano yako.
TUPO PAMOJA.
Rafiki na kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: