Uhuru ni moja ya mahitaji muhimu sana kwenye maisha yetu. Ili maisha yawe bora, na uweze kuyafurahia, ni lazima uwe na uhuru. Na uhuru siyo tu kutokuendeshwa na wengine, bali unahitaji kuwa huru hata kwako wewe mwenyewe pia.
Unaweza kupata uhuru kutoka kwa wengine lakini ukajinyima uhuru wewe mwenyewe. Ndiyo maana leo nataka ujiulize swali hili, je upo huru kiasi gani?
Kwa binadamu huru, anatakiwa kujitosheleza kwa maisha yale aliyonayo, na kutokutegemea kitu fulani pekee kwenye maisha. Ni lazima awe huru kubadilika kadiri mambo yanavyobadilika.
Kama unasema siwezi kuishi bila ya kitu fulani, au mtu fulani, haupo huru. Kwa sababu umeshayafanya maisha yako yategemee kitu kingine au watu wengine. Tatizo la kutegemea vitu hivi vingine ni kwamba huwezi kuwa na uhakika navyo, watu watakuangusha, vitu havitatokea kama ulivyotegemea, lakini wewe utabaki kuwa wewe.
Ili kuwa huru unahitaji kujitosheleza mwenyewe, vile ulivyo. Na kujua chochote unachotegemea kinaweza kuondoka muda wowote na hivyo usijiweke kwenye hali ambayo maisha yako yatashindwa kwenda bila ya kitu fulani au mtu fulani.
Kujipima uko huru kiasi gani, chagua kuishi japo kwa kipindi bila ya kutegemea kile ambacho unasema huwezi kuishi bila ya kitu hiko. Fikiria vile vitu ambavyo unapenda kufanya sana na umeshaona kama ni sehemu ya maisha yako, na chagua kutokufanya au kutokuwa navyo kwa muda. Utaona ni jinsi gani maisha yanavyoweza kwenda licha ya kuwa una nini au umekosa nini.
Yafanye maisha yako kuwa huru, usiegemee chochote ambacho ni cha kupita.
SOMA; Hivi Ndivyo Waajiriwa Wanavyopoteza Uhuru Wao Wenyewe, Na Jinsi Ya Kuudai Tena.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba uhuru wa maisha yangu ni pale ambapo sitegemei kitu cha nje ndiyo maisha yangu yaweze kwenda. Kwa sababu najua vitu vya nje vipo kwa wakati tu, siyo vya kudumu. Nitavitumia wakati vipo lakini sitakubali maisha yangu yaharibike kwa sababu nakosa vitu vya nje. Uhuru wa maisha yangu ninao mimi mwenyewe, sikubali kuuza kwa wengine au kwa vitu vingine.
NENO LA LEO.
Uhuru wa kweli ni pale unapoweza kuishi kwa chochote kile unachopata au kukutana nacho. Pale ambapo huwezi kushindwa kuishi kwa sababu umekosa kitu fulani au mtu fulani.
Ukitaka kuishi maisha ya uhuru, ambayo yana furaha na mafanikio, maisha yako yasitegemee moja kwa moja kitu fulani au mtu fulani. Kuwa tayari kuishi bila ya kile unachokipenda sana na maisha yako hayatafungwa na chochote.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.