Tunapokuwa wenyewe na kupata nafasi ya kufikiria maisha yetu, huwa tunafikiria vile vitu ambavyo tunavitaka lakini bado hatujavitapa. Tunafikiria kwa kina jinsi gani maisha yetu yatakuwa bora kama tutapata vitu hivyo ambavyo hatuna.

Lakini tunasahau ya kwamba kuna vitu ambavyo tunavyo sasa, ambavyo tunavichukulia kwa ukawaida, lakini kama vikiondoka tutavikosa sana. Tunasahau kufikiria vitu hivi ambavyo tayari tunavyo na kufurahia jinsi ambavyo vinafanya maisha yetu kuwa bora jinsi yalivyo sasa.

Kwa njia hii tunaishi maisha ambayo kila mara tunaangalia ni kipi hatuna. Kwa sababu hata tunapopata tunachotafuta, bado tunaona kuna vingine ambavyo bado tunahitaji kupata.

Kuweza kuishi maisha bora na ya furaha, tunahitaji kuona mchango wa vile ambavyo tunavyo sasa. Kuona ni jinsi gani vinaboresha maisha yetu na kujua kama hatutakuwa navyo maisha yetu hayatakuwa kama yalivyo sasa.

SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Kinachotuzuia Kuishi Maisha Ya Furaha.

TAMKO LANGU;

Nimekuwa natumia muda wangu kufikiria vile vitu ninavyotaka ambavyo kwa sasa sina. Kwa njia hii nimekuwa nasahau kwamba kuna vitu ambavyo ninavyo sasa na kama vikiondoka maisha yangu hayatakuwa kama yalivyo sasa. Kuanzia sasa nitakuwa natafakari vitu nilivyonavyo na mchango ambao vimetoa kwenye maisha yangu. Kwa njia hii nitayafurahia maisha yangu bila ya kujali nakosa nini.

NENO LA LEO.

Mara nyingi huwa tunafikiria vile vitu ambavyo tunavitaka ila kwa sasa hatuna. Tunasahau kwamba kuna vitu ambavyo kwa sasa tunavyo, ambavyo kama tutavikosa maisha yetu hayatakuwa kama yalivyo sasa.

Ili kuweza kuona ubora wa maisha na kuyafurahia, ni lazima uweze kuvithamini vile ambavyo unavyo sasa na kuona mchango wake kwenye maisha yako.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.