Ujue ukweli nao utakuweka huru…
Hii ni falsafa ambayo imekuwepo tangu zamani, na ni falsafa nzuri sana kwa kuwa na maisha bora na ya mafanikio. Lakini kwa bahati mbaya sana wengi tunashindwa kuitumia na hivyo kushindwa kuwa na maisha bora.
Wote tunajua ya kwamba uhuru ndiyo kitu muhimu sana kwenye maisha yetu. Na siyo uhuru kutoka kwa wengine pekee, bali uhuru kutoka kwetu wenyewe pia. Watu wengi wamejifunga na mambo ambayo yanawanyima uhuru, na hii yote inatokana na kutokuujua ukweli.
Karibu mwanafalsafa mwenzangu katika kipengele hiki cha FALSAFA MPYA YA MAISHA ambapo tunaijenga upya falsafa ya kuwa na maisha bora yenye furaha na mafanikio makubwa. Leo tutakwenda kuangalia kikwazo cha ukweli, nini kinatuzuia kuujua ukweli ili tuweze kuwa huru.
Ukweli ni nini?
Kabla hatujaangalia kinachotuzuia kuujua ukweli, ni vyema tukaangalia ukweli ni nini. Na hakuna kitu kigumu kueleza kama ukweli, kwa sababu mara nyingi watu tumekuwa tukichanganya ukweli na maoni.
Kwa lugha rahisi tunaweza kusema kwamba ukweli ninile hali inayoendana na uhalisia wa asili. Kile ambacho kinaendana na jambo jinsi lilivyo ndiyo ukweli. Ukweli haubadiliki iwe ni kwa watu au kwa mazingira. Ukweli unabaki vile ulivyo iwe watu wanakubaliana nao au hawakubaliani nao.
Kwa maana hii ya ukweli ni vigumu sana kwa wengi kuweza kufikia ukweli. Tunaweza kusema ya kwamba vitu vingi tunavyofikiri sasa ni vya kweli, siyo kweli. Na kadiri muda unavyokwenda ndivyo tunavyozidi kuujua ukweli.
Kwa mfano zamani watu waliamini kwamba jua linaizunguka dunia, na huu ndiyo ulikuwa ukweli, na aliyekwenda kinyume na hilo alipata adhabu kali sana, hata ya kifo. Lakini baadaye kadiri uelewa wa watu ulivyoongezeka, iligundulika ya kwamba dunia ndiyo inalizunguka jua. Na huu ndiyo ukawa ukweli. Ukiangalia kwenye hali hii siyo kwamba ukweli umebadilika, bali uelewa umeongezeka.
Hata tukiangalia mila zote potofu ambazo tumekuwa tunazipinga na nyingine zimeshatokomezwa kabisa, kipindi ambapo mila hizo zilikuwa zinafanyika, zilionekana ndiyo ukweli, na hivyo kila mtu kufanya. Lakini kadiri uelewa wa watu ulivyoongezeka ikaonekana kwamba siyo kweli.
Maoni ya watu yamekuwa wakichanganywa na ukweli, hasa watu hao wanapokuwa ni watu wanaochukuliwa kuwa na mamlaka fulani.
Falsafa ya ijue kweli nayo itakuweka huru, ni falsafa ambayo inakuhitaji wewe uwe mtu wa kujifunza wakati wowote kwenye maisha yako, kwa sababu kile ambacho unafikiri sasa ni kweli, huenda kesho ukapata ushahidi kwamba siyo kweli. Na kwa jinsi dunia inavyokwenda kasi sasa, vitu vingi unavyoshikilia kama ukweli vinaweza kuwa siyo kweli.
Pamoja na mabadiliko haya makubwa yanayoufunua ukweli, bado wengi wanakataa ukweli huu na kuendelea kushikilia yale ambayo yameshapitwa na wakati.
Ni kipi hasa kinatuzuia kuujua ukweli?
Kuna kikwazo kikubwa ambacho kimekuwa kinatuzuia kuujua ukweli na hivyo kutuzuia kuwa na maisha bora. Kikwazo hiki kinaanza na sisi wenyewe kwa jinsi ambavyo tunachukulia mambo yetu. Kikwazo hiki ni UBAGUZI.
Sisi binadamu tuna tabia ya kubagua, na tunabagua kwakuchagua kile ambacho tunataka na kuacha kile ambacho hatukitaki. Tunapojifunza vitu, kwa kusikia au kusoma, tunatafuta vile ambavyo vinaendana na kile tunachoamini na kuacha vile ambavyo vinapingana na kile tunachoamini.
kwa mfano kama kuna vyama viwili vya siasa, chama A na chama B. Kama wewe ni mfuasi wa chama A utakuwa unakubaliana na kile ambacho chama A kinasimamia. Na utakapokutana na mtu anayeongea kuhusu chama A utamwona ndiye mtu anayejitambua sana na kuchukua kila anachokisema. Lakini ukikutana na mtu anayeongea kusifia chama B utaona kama ni mtu aliyepotoka na asiyejua ni nini anachosimamia. Kwa njia hii utaacha kumsikiliza hata kama kuna mambo mazuri atakayokuwa nayaongea.
Hivi ndivyo ilivyo kwenye maeneo mengi ya maisha yetu, hasa yale ambayo tunachanganya hisia zetu kama siasa, dini na hata mapenzi.
Tunachagua kusikiliza na kujifunza kile ambacho tayari kinaendana na kile tunachoamini sisi. Na hivyo kuendelea kujua kile ambacho tunajua. Hali hii imekuwa inawazuia wengi kuujua ukweli, hasa pale kile wanachoamini kinapokuwa siyo kweli. Tunapenda kuchukulia kile tunachojua na kuamini kama ndiyo uhakika na kile ambacho hatukiamini kuwa ndiyo uongo. Lakini kama ambavyo tumeona kwenye mifano ya zamani, vingi ambavyo tunaamini siyo kweli.
Tufanyeje ili tuweze kuujua ukweli?
Tilia mashaka kwenye kila jambo. Ndiyo kuwa na shaka kwa kila jambo, na hoji zaidi. Usikubali kupokea kila kitu kwa sababu tu kinaendana na kile unachoamini, badala yake hoji zaidi. Hoji kujua uhalali, hoji kuona kama kile unachoamini kinaendana na uhalisia wa maisha. Usiwe na ubaguzi, badala yake kuwa kati kati, usipokee kila kitu kama kilivyo, na usipinge kila kitu kwa sababu hakiendani na vile unavyoamini.
Pia kuwa tayari kujifunza vile ambavyo ni tofauti na unachoamini wewe. Jua ya kwamba kwenye kila kitu kuna jambo unaweza kujifunza. Jua ya kwamba hata kama kitu hakionekani sahihi, kuna kitu unaweza kujifunza.
Kuwa tayari kubadilika wakati wowote, na pale mazingira yanapoonesha kwamba mabadiliko ni lazima, usiendelee kung’ang’ana na kile ulichozoea kufanya. Hata kama kile unachoamini sasa ndiyo kilikusaidia huko nyuma, haimaanishi kitaendelea kukusaidia. Nyakati zinabadilika na uelewa mpya unapokuja kuna mapya mengi yanajulikana. Jifunze mara zote na kuwa tayari kubadilika. Kwa kasi hii ambayo dunia inakwenda, kutokubadilika ni kuchagua kurudi nyuma.
Usijipe uhakika wa jambo lolote, kwa sababu hakuna jambo lolote ambalo ni la uhakika. Unapojipa uhakika unachagua kuacha mengine yote na hivyo kuacha kujifunza na kushindwa kuujua ukweli. Mara zote kuwa wazi kujifunza, kuwa tayari kuona vitu kwa jinsi vilivyo na ndipo uamue ni hatua gani unaweza kuchukua.
Mwisho kabisa usikubali kuwa shabiki. Shabiki ni mtu ambaye anafuata kitu kwa sababu wengine wanafuata. Hajachimba kwa ndani na kujua kwa nini anafuata kitu fulani, kwa sababu kila mtu anafuata na yeye anaona ni salama kufuata. Wewe kaa chini na ufanye tathmini kwa kila unachofuata au kuamini, na jiulize kwa nini unakifuata. Kwa nini uchague kitu hiko na sio vingine ambavyo wengine wanafuata au kuamini. Na hapa utapata ufahamu wa ndani, ambao utakuwezesha kuchukua hatua pale mambo yanapobadilika.
Ujue ukweli nao utakuweka huru, hii ni falsafa ambayo itaendelea kuishi. Wale wasioujua ukweli ndio wanaodanganywa na kutapeliwa, wale wasiojua ukweli ndio wanaoburuzwa. Kama unataka uhuru wa maisha yako, ambao utakuwezesha kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako, basi ujue ukweli.
Nakutakia kila la kheri katika kuujua ukweli, hili ni jukumu la kila siku.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz