Kwenye tafiti za kisayansi, kama kwenye kila tukio kuna kitu fulani, basi kitu hiko ndiyo kinachangia kutokea kwa tukio hilo. Kwa mfano kama imetokea kwenye eneo fulani watu wameanza kuharisha ghafla, na kila anayeharisha akipimwa anaonekana kuwa na vijidudu vya aina fulani, basi kuna uwezekano mkubwa vijidudu vile ndiyo vimepelekea watu hao kuharisha.

Unakumbuka nimekuwa nakuambia mara nyingi ya kwamba kwenye safari hii ya mafanikio unahitaji kujifunza kutoka kwa wengine. Unahitaji kujifunza kutoka kwa wale ambao wameshafanikiwa. Lakini pia watu hawa ni wachache na wengine hawapo tayari kukuonesha ni jinsi gani wamefanikiwa. Na nikakushauri njia nzuri ni kuangalia wale walioshindwa wanapenda kufanya nini na wewe usifanye. Kwa kutumia njia za kisayansi, kama walioshindwa wote wanapenda kufanya kitu fulani, kuna uwezekano mkubwa kitu hiko ndiyo kinawapelekea kushindwa.

Leo tunaangalia kitu kimoja ambacho watu wote walioshindwa wanacho. Ukijua kitu hiki na kukiepuka unajiondoa kwenye nafasi ya kushindwa.

Kila mtu aliyeshindwa ana sababu. Tena sababu nzuri sana kwa nini ameshindwa. Na mara nyingi sababu hizo ni za nje, jinsi gani watu wengine wamewazuia wao kuweza kufanikiwa. Wana kila sababu wazazi, ndugu, serikali, mwajiri, uchumi, hali ya hewa na sababu nyingine nyingi. Sababu hizi zinawaridhisha na hawajisumbui kuweka juhudi kubwa na hivyo kushindwa kufikia mafanikio makubwa.

Kwa upande wa pili, wale wanaofanikiwa hawana sababu hizo, na siyo kwa sababu hawapitii mambo hayo, ila kwa sababu wanachagua kuachana nayo. Wanachagua kuchukua hatua na hii inawawezesha kupata kile wanachokitaka.

Acha sasa kutafuta sababu kwa nini huwezi au utashindwa, na badala yake chukua hatua kuboresha maisha yako na kufika kule unakotaka kufika.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; THE 50TH LAW (Mbinu Za Kuondokana Na Hofu)

TAMKO LANGU;

Ninajua ya kwamba watu wote walioshindwa wana sababu nyingi kwa nini wameshindwa, na sababu hizo ni nzuri kwao kulingana na mtazamo wao. Mimi sitaki kuwa mshindwa, nataka kushinda na hivyo sitakuwa mtu wa sababu. Nitakuwa mtu wa kuchukua hatua mara zote.

NENO LA LEO.

Watu wote walioshindwa wana kitu kimoja ambacho wanakipenda; SABABU.

Watu hawa wana sababu kwa nini wameshindwa kufanikiwa, na mara nyingi sababu hizi ni za nje.

Kama unataka kufanikiwa, usikubali kuwa mtu wa sababu, badala yake kuwa mtu wa kuchukua hatua.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.