Mazungumzo Muhimu Yanayoweza Kubadili Maisha Yako Kabisa.

Habari za wakati huu rafiki yangu?
Ni imani yangu kwamba uko vizuri na unaendelea kuweka juhudi ili kuweza kufikia malengo yako uliyojiwekea kwa mwaka huu. Hili ndilo jambo la msingi sana kwako kufanya, endelea kuweka juhudi na hakuna kitakachoweza kukuzuia wewe kupata kile unachotaka.
Kuna kitu kimoja muhimu sana ambacho watu wengi huwa hawakielewi mapema. Kwa kushindwa kuelewa kitu hiki watu wamekuwa wanajikuta wakihangaika na mambo ambayo hayawezi kuwafikisha kule wanakotaka kufika. Kitu hiki ni chanzo kikuu cha mabadiliko kwenye maisha. Unafikiri mabadiliko ya kweli kwenye maisha yako yanatoka wapi? Yanatoka ndani yako au nje yako? umewahi kufikiria kwamba kama watu wangekuelewa basi ungefikia mafanikio? Au kufikiria kama mwajiri wako angekuwa mwelewa basi ungefika unakotaka? Kama na wewe umeshawahi kufikiria kama hivyo unajipoteza njia.
 

KUPATA KITABU HIKI BONYEZA KWENYE PICHA AU MAANDISHI HAYA


Watu wengi wamekuwa wakifikiri kwamba mabadiliko kwenye maisha yao yatakuja pale ambapo mazingira yao yatakapobadilika. Pale mwajiri, wateja, ndugu na hata uchumi utakapokuwa vizuri basi na wao watakuwa vizuri. Lakini ukweli ni kwamba hakuna mtu mwenye nguvu yoyote ya kubadili vitu hivi vya nje. Badala yake kila mmoja wetu ana nguvu ya kuibadili yeye mwenyewe. Hivyo mabadiliko ya kweli kwenye maisha yanaanza na mtu mwenyewe. Yanaanzia pale mtu anapojua ya kwamba anataka kubadili maisha yake na anachukua hatua kwa kuanzia ndani yake. Hata kama mazingira ya nje ni magumu kiasi gani, nia ya mabadiliko ikishaanzia ndani, hakuna kinachoweza kuizuia.

Leo tunakwenda kuangalia mazungumzo muhimu sana yanayoweza kubadili maisha yako kabisa. Wote tunajua nguvu ya mazungumzo mbalimbali ambayo tumekuwa tunafanya kwenye maisha yako. Unaweza kuomba ushauri na katika mazungumzo hayo ya ushauri ukajifunza mambo mengi sana. Unaweza kuhudhuria semina na kupitia mazungumzo hayo ya semina ukajifunza mengi na kuweza kubadili maisha yako. Lakini haya yote ni mazungumzo ya nje, ambayo nguvu yake haiwezi kufikia mazungumzo tutakayokwenda kuyajadili leo kupitia makala hii.
Mazungumzo muhimu yanayoweza kubadili maisha yako ni yale mazungumzo yako ya ndani. Yale mazungumzo unayofanya na wewe mwenyewe ni mazungumzo ambayo yana nguvu kubwa sana kwenye maisha yako.
Kabla hatujaenda mbele kwanza tukubaliane jambo hili moja muhimu, kila mtu ana mazungumzo na nafsi yake. Na siyo lazima yawe mazungumzo ambayo unaongea kwa sauti, bali katika mawazo yako kunakuwa na mazungumzo yanayoendelea mara zote. Wakati mwingine kunakuwa na ubishi mkali sana hasa pale unapohitaji kufanya maamuzi.
SOMA; Njia Moja Ya Uhakika Ya Kuongeza Thamani Ya Kazi Yako Na Kipato Chako Pia.

Kuna kauli ambazo umekua unajiambia wewe mwenyewe mara kwa mara. Kauli hizi inawezekana umezibeba kutoka kwenye jamii au ndivyo ulivyozoea kwenye maisha yako. Kauli hizi zina nguvu kubwa ya kubadili maisha yako au kuzuia mabadiliko kwenye maisha yako. Unaweza kuweka mipango mikubwa na mizuri sana, lakini kabla hujafika mbali mazungumzo kwenye mawazo yako yanaanza. Una uhakika utaweza? Umeshashindwa mengi kwa nini hili huwezi? Acha kujidanganya, huwezi kufikia hilo unalotaka. Kauli hizi zinaendelea hivi hatimaye unashindwa kabisa kuchukua hatua.
Wanasaikolojia wanasema ya kwamba sehemu kubwa ya kauli tunazojiambia sisi wenyewe ni kauli hasi. Ni kauli za kukatisha tamaa au kujiona kwamba huwezi au haiwezekani. Kwa jambo lolote ambalo mtu atataka kufanya, ni lazima mazungumzo haya, ambayo yapo upande hasi yataingia kwenye mawazo yake. Na kama mtu hajui jinsi ya kudhibiti mazungumzo yake, hawezi kuchukua hatua.

Jinsi ya kutumia mazungumzo haya vizuri.
Kwa kuwa mazungumzo haya unayofanya na nafsi yako ndiyo mazungumzo yenye nguvu kubwa kwenye maisha yako, na kwa kuwa mara nyingi mazungumzo tunayofanya na nafsi zetu ni hasi, tunahitaji kuwa na njia bora ya kuhakikisha tunatumia mazungumzo haya kwa faida yetu. Hapa tutaangalia njia za kuweza kutumia mazungumzo haya kukuwezesha kufika popote unapotaka kufika.

Kuwa na mazungumzo chanya muda wote.
Huu ndio msingi wa kuweza kudhibiti mazungumzo yako na kuyatumia kukufikisha unakotaka kufika. Unahitaji kutengeneza mazungumzo chanya muda wote. Kuwa chanya kwa kufikiria upande chanya wa mambo yote unayokutana nayo au unayokwenda kufanya. Changamoto ya kuwa chanya ni kwamba kwa jamii tunazoishi, hili ni jambo gumu kuweza kufikia. Tumezungukwa na watu wengi ambao ni hasi na kila kitu kinachotokea kinapewa tafsiri hasi. Hivyo akili zetu zimeshajijenga kwenye msingi wa hasi. Unahitaji kujiondoa kwenye hali hii haraka sana kwa kuangalia upande chanya wa jambo lolote. Katika kila jambo linalotokea au unalotaka kufanya, angalia upande chanya wa jambo hilo. Badala ya kufikiria kwa nini ni baya au haiwezekani, jilazimishe kufikiria kwa nini ni zuri au inawezekana. Kwa mabadiliko haya ya kufikiri pekee unaanza kuona picha tofauti na uliyokuwa unaona mwanzoni.
SOMA; Epuka Adui Huyu Mkubwa Wa Mafanikio Yako Anayekurudisha Nyuma.

Usipende kulalamika na kulaumu, badala yake chukua hatua.
Hakuna kitu hasi kwenye dunia hii kama kulalamika na kulaumu wengine. Kwa kulalamika na kulaumu maana yake unajiambia wewe huwezi kufanya makubwa bali wengine. Wale unaowalalamikia ndio unawapa majukumu ya maisha yako, mara zote utakapokutana na changamoto, hutakazana kuitatua wewe mwenyewe, badala yake utatafuta nani anaweza kuhusika. Kwa njia hii kila kitu utaona ni kigumu na hakiwezekani. Kuwa mtu wa kuchukua hatua, kama kuna kitu hukipeni kibadili, na kama huwezi kukibadili basi achana nacho.
 
Jiambie kauli chanya mara kwa mara.
Kwa kuwa mawazo hasi huwa yanakuja yenyewe kutokana na mazoea ambayo umeshajijengea, siyo rahisi kuondokana na mazungumzo haya hasi. Hapa unahitaji kutumia nguvu za ziada kuhakikisha unaondokana na mazungumzo haya hasi. Na unaweza kufanya hivyo kwa kujiambia kauli chanya mara kwa mara. Tengeneza kauli chanya za kujiambia kama hizi zifuatazo; NINAWEZA KUFANYA CHOCHOTE NINACHOAMUA KUFANYA, KILA SIKU NAZIDI KUWA BORA KWNEYE KILE NINACHOFANYA, MAISHA YANGU NI JUKUMU LANGU. Tengeneza kauli itakayoendana na wewe kulingana na maisha yako na kile unachotaka kisha jiambie kauli hiyo angalau mara tatu kwa siku, unapoamka, mchana na kabla ya kulala. Jiambie kauli hiyo kwa sauti, kwa njia hii itaanza kutengeneza mazungumzo chanya kwenye mawazo yako.
 
Kuwa mtu wa kushukuru.
Katika mahusiano yetu na wengine, huwa tunaangalia zaidi upande hasi. Mtu anaweza kufanya mambo mazuri mengi sana, lakini akafanya jambo moja baya, tukasahau kabisa wema wake na kuangalia lile baya alilofanya. Hii ni njia inayotufanya tuendelee kuwa na mazungumzo hasi mara zote. Unahitaji kuwa mtu wa shukrani, mara zote tafuta jambo la kushukuru kwenye maisha yako na kwa wale wanaokuzunguka. Jilazimishe kupata kitu cha kushukuru kwenye hali yoyote unayopitia. Kwa kufanya hivi unajilazimisha kuwa na mazungumzo chanya ambayo yatakuwezesha kuziona fursa nyingi na nzuri.

Kila mmoja wetu huwa anakuwa na mazungumzo na nafsi yake, haya ni mazungumzo muhimu na yana mchango mkubwa kwenye maendeleo ya maisha yako. Yafanye mazungumzo haya kuwa chanya na mara zote utakuwa mtu wa kuziona fursa na kuzichukulia hatua. Jitengenezee kauli chanya, acha kulalamika na kuwa mtu wa shukrani. Ni mabadiliko madogo lakini yenye manufaa makubwa kwenye maisha yako.
Fanyia kazi hili ambalo umejifunza kwenye siku hii ya leo.
TUPO PAMOJA,
Rafiki na kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: