Ni rahisi sana kuona watu waliofanikiwa na kusema na wewe unataka ufanikiwe kama wao. Lakini unapoianza safari ya mafanikio ndipo unapogundua kuna mengi hukuyajua. Kuna mengi sana ambayo utayashindwa kwenye safari yako hiyo na kama utakuwa hujajiandaa vizuri hutafika mbali. Watu waliofanikiwa hawakufika walipo kwa mara moja tu, bali wamevuka vikwazo na changamoto nyingi ambavyo kwa bahati mbaya hutaviona anapokuwa ameshafanikiwa.

Ni kwa sababu hii mwandishi John Maxwell aliandika kitabu FAIL FORWAD ambacho lengo lake ni kukusaidia wewe uweze kutumia kushindwa kwako kufikia mafanikio makubwa. Kupitia kitabu hiki mwandishi ametushirikisha hatua kumi na tano ambazo unahitaji kuzipitia ili uweze kufanikiwa licha ya kupitia changamoto nyingi.

Karibu tujifunze kwa pamoja hatua hizi 15 na hatua zakuchukua ili tuweze kushinda kwa kufikia mafanikio tunayoyataka.

Hatua ya kwanza; jua kuna tofauti moja kuu kati ya watu wa kawaida na watu wanaofikia mafanikio makubwa.

Ukiyaangalia maisha ya wale ambao wanafikia mafanikio makubwa, utaona kitu kimoja ambacho wanacho ila wale wanaoshindwa hawana. Kitu hiko ni jinsi wanavyochukulia kushindwa. Wale wanaofanikiwa wanajua ya kwamba kushindwa ni sehemu ya safari yao ya mafanikio na wanatumia kushindwa kama sehemu ya kujifunza. Ila wale wanaoishia kuwa wa kawaida wanaposhindwa wanachukulia kwamba ndiyo mwisho wa safari yao.

FUNZO; Jua ya kwamba kushindwa ni sehemu ya kufikia mafanikio, na tumia kushindwa kama sehemu ya kujifunza.

Hatua ya pili; Jifunze maana mpya ya kushindwa.

Watu wengi huchukulia kushindwa kama kitu cha aibu, kwamba wanaonekana hawajui au hawapo vizuri. Kwa maana hii wengi wanaogopa kuchukua hatua na hivyo wanabaki pale walipo. Wale wanaofanikiwa wanajua maana halisi ya kushindwa ni kujifunza. Unapochukulia kila hatua ni kujifunza, unakuwa na shauku ya kuchukua hatua zaidi kwa sababu unajua unajifunza. Na kila kosa wanalofanya wanahakikisha hawalirudii tena hivyo kuwa kwenye nafasi nzuri ya kufanikiwa.

FUNZO; Kushindwa siyo aibu wala kutokujua, badala yake ni kujifunza ili kufikia mafanikio. Jua hili mara zote na kuwa tayari kujifunza zaidi.

Hatua ya tatu; jiondoe wewe kwenye kushindwa.

Watu wengi wanaposhindwa wanaona wao ndio wameshindwa. Yaani kama mtu amejaribu kufanya kitu na akashindwa, anaona yeye ndiyo ameshindwa, yeye ndiyo hawezi na hafai. Lakini wanaofanikiwa wanajua ya kwamba kushindwa kitu hakuwafanyi wao kuwa washindwa. Wanapojaribu kufanya kitu na wakashindwa hawajichukulii wao kama washindwa, bali wanajua mbinu walizotumia ndiyo zimeshindwa na hivyo kutafuta mbinu nyingine.

FUNZO; Unaposhindwa, usijichukulie wewe kama mshindwa, badala yake jua mbinu ulizotumia ndiyo zimeshindwa. Badili mbinu zako na utashinda.

Hatua ya nne; chukua hatua na punguza hofu zako.

Kitu kikubwa kinachowazuia watu kufikia mafanikio ni hofu. Kuna hofu nyingi zinazowazuia watu wasiweze kufanya makubwa. Na pale wanapojaribu na wakashindwa, ndiyo hawathubutu tena kwa sababu hofu inakuwa kubwa zaidi. Wanaofanikiwa wanajua dawa ya hofu ni moja, kuchukua hatua. Kwenye kile ambacho wanahofia kufanya wanajua wataondokana na hofu hiyo kama wataanza kukifanya, na hivyo wanafanya na hofu inapotea.

FUNZO; Jiulize ni kipi ambacho unahofia kufanya mpaka sasa halafu anza kukifanya, utashangaa ile hofu inaondoka na unaziona fursa nyingi kwako kufanikiwa.

Hatua ya tano; Kubali majukumu yako.

Pale ambapo watu wanakosea na hivyo kushindwa, huwa wanakimbilia kutafuta nani amesababisha wao washindwe. Na unajua nini, lazima wanawapata watu hao. Na hivyo kulaumu na kulalamika juu ya kushindwa kwao. Hili haliwasaidii chochote zaidi ya kuwazuia kufanikiwa. Wanaofanikiwa wanaposhindwa wanajiuliza wamesababishaje kushindwa huko, wanayaona makosa yao na kuchukua hatua. Hawalaumu wala kulalamikia wengine, wanachukua hatua.

FUNZO; Unaposhindwa usikimbilie kutafuta wa kulaumu, badala yake angalia ni makosa gani uliyofanya na jirekebishe. Anza upya ukiepuka pale ulipokosea awali.

Hatua ya sita; usiruhusu kushindwa kwa nje kuingie ndani yako.

Pamoja na kwamba utaangalia mchango wako kwenye kila hatua unayoshindwa, kuna wakati utashindwa kwa mambo ambayo yako nje ya uwezo wako. Hapa ndipo wengi wanaposhindwa kuchukua hatua kwa sababu wanaona wamekazana sana lakini mambo hayajawaendea vizuri. Wale wanaofanikiwa wanajua kwamba hata kama kushindwa kumesababishwa na mambo ambayo yapo nje ya uwezo wao, bado wanahitaji kuweka juhudi zaidi. Hawakubali mawazo yao yaangalia upande wa matatizo pekee bali wanaangalia upande chanya wa hatua gani wanaweza kuchukua.

FUNZO; Pale mambo yaliyopo nje ya uwezo wako ndiyo yanakusababisha ushindwe, usikate tamaa bali angalia ni jinsi gani unaweza kutumia hali ulizonazo au unazopitia kuweza kufikia mafanikio.

Hatua ya saba; iambie jana KWA HERI.

Watu wengi wana maumivu ya nyuma ambayo yanawazuia kufanikiwa sasa. Wanakumbuka jinsi walivyojaribu siku za nyuma ila wakashindwa. Wanakumbuka jinsi walivyoumia siku hizo za nyuma. Na kila wakipata kumbukumbu hizi wanajiapiza kwamba hawatakuja kurudia tena. Wale wanaofanikiwa nao wanapitia haya magumu, ila hawakubali magumu ya nyuma kuharibu siku za mbele. Wanakubali kile ambacho kimeshatokea na kujiandaa kupokea vile vinavyokuja. Wanajua hata kama nyuma ilikuwa mbovu kiasi gani, bado mbele ni mpya na wanaweza kufanya makubwa. Watu hawa waliofanikiwa wanajua kilichowawezesha kufanikiwa jana siyo kitakachowawezesha kufanikiwa kesho, na hivyo kuwa tayari kubadilika kila siku. Ila wale wanaoshindwa wanaendelea kufanya yale ambayo walishazoea kufanya.

FUNZO; Usitumie jana yako kuharibu kesho yako, jana imeshapita huwezi kuibadili, jifunze kupitia jana yako. leo ni siku nyingine mpya unaweza kuchukua hatua na kufikia mafanikio. Pia kuwa tayari kubadilika kadiri siku zinavyokwenda.

Hatua ya nane; jibadili wewe mwenyewe na dunia itabadilika.

Wengi wa wanaoshindwa hulalamika ni jinsi gani wale wanaowazunguka wanawafanya washindwe kufanikiwa. Watalaumu ndugu na familia kwa yale wanayofanya, watalaumu mwajiri na hata dunia kwa ujumla. Kwenye akili zao wanachofikiria ni kwamba wakiweza kuwabadili watu hao wanaowazunguka basi wataweza kufanikiwa. Lakini wanaofanikiwa wanajua siri moja, hawawezi kumbadili mtu yeyote, badala yake wanaweza kujibadili wao wenyewe. Wanajua wao wakishabadilika na dunia inayowazunguka itabadilika na kuwaletea kile ambacho wanakitaka. Na hii inawawezesha kufikia mafanikio makubwa.

FUNZO; Usijaribu kuibadili dunia, au kuwabadili wengine waende vile unavyofikiri wewe. Badala yake badilika wewe kwanza, anza kusihi vile ambavyo unataka maisha yaende na utashangaa kuona watu wanabadilika wenyewe.

Hatua ya tisa; acha kujiangalia wewe mwenyewe, angalia na wengine.

Wale wanaoshindwa wanajua kitu kimoja tu, ninapata nini, nanufaikaje, nawezaje kupata zaidi ya wengine. Hawa ni watu wabinafsi ambao wanajiangalia wao wenyewe tu. Wanachotafuta ni jinsi gani wanaweza kupata zaidi ya wengine, wanatafuta njia za kuwapa faida hata kama haziwasaidii wengine. Kwa njia hii wanajikuta hawana mahusiano mazuri na wengine na hata wao binafsi. Wanaofanikiwa wanajua mafanikio yao yanatokana na wengine. Na hivyo hutumia muda wao kufikiria ni jinsi gani wanaweza kuwanufaisha wengine. Kwa njia hii wanaziona fursa nzuri ambapo wengine wanafaidika na wao wanafaidika mara dufu. Unapotoa unapokea zaidi ya ulichotoa, hii ni sheria ya asili.

FUNZO; Usijiangalie wewe mwenyewe tu, usiangalie unanufaikaje wewe peke yako, bali ambalia wengine wananufaikaje. Jiulize ni mchango gani ambao unao kwenye maisha ya wengine. Kadiri unavyokuwa na mchango mkubwa, ndivyo unavyofanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Hatua ya kumi; tafuta faida kwenye kila hali ngumu unayopitia.

Kila mtu huwa anapitia nyakati ngumu kwenye maisha yake, kila mtu huwa anapitia changamoto na kushindwa. Lakini katika hali hizi mbaya, kuna ambao wanafanikiwa zaidi na wengine wanashindwa kabisa. Wale wanaoshindwa wanatumia muda wao kuangalia ule ugumu wanaopitia, wanaweza hata kujikumbusha mengine magumu waliyopitia huko nyuma na kuona labda wana kisirani. Hili linawafanya wazidi kushindwa. Ila wale wanaofanikiwa, kwenye kila hali ngumu wanayopitia wanajiuliza ni kipi kizuri wanaweza kukitumia kwenye hali hiyo? Kwa kujiuliza swali hili wanaziona fursa za kutumia na hatimaye kuweza kufanikiwa zaidi.

FUNZO; Unapopitia nyakati ngumu, usiangalie ule upande wa ugumu pekee, bali jiulize ni kipi kizuri unaweza kutumia kwenye hali hiyo ngumu unayopitia. Mara zote unaona kile unachotafuta, ukitafuta mazuri utayaona na ukitafuta mabaya lazima uyapate.

Hatua ya kumi na moja; unapofanikiwa, jaribu kikubwa zaidi.

Hakuna adui wa mafanikio kama kufanikiwa. Watu wengi wanapoweka malengo na kuyafikia, huona ndiyo wamefika mwisho na kujisahau. Hii haiwachukui muda mrefu kabla hawajaanguka au kubaki nyuma kulingana na dunia inavyokwenda. Wale wanaobaki kwenye kilele cha mafanikio wanajua kwamba mafanikio ni safari na siyo mwisho wa safari. Wanajua wakishafikia lengo walilokuwa wamejiwekea, wanahitaji kuenda lengo la juu zaidi. Kwa hali hii mara zote wanaweka juhudi na kubaki kwenye mafanikio.

FUNZO; Unapofikia malengo uliyojiwekea usijisahau, bali weka malengo makubwa zaidi na yafanyie kazi. Mafanikio ni safari na siyo mwisho wa safari. Endelea kuweka juhudi mara zote.

Hatua ya kumi na mbili; jifunze kwenye kila hatua unayoshindwa.

Kama hushindwi maana yake hujaribu mambo makubwa. Kama unafikia kila lengo unalojiwekea basi huweki malengo makubwa. Unafanya vile ambavyo umezoea kufanya na kwa bahati mbaya hivi havitakufikisha kwenye mafanikio. Wanaofanikiwa mara zote wanajaribu vitu vipya na vikubwa na wanaposhindwa wanajifunza ni wapi wanahitaji kuboresha zaidi.

FUNZO; Acha kufanya vile ambavyo umezoea kufanya, jiwekee malengo makubwa ambayo hujawahi kufikiria kama utafikia, yafanyie kazi na unaposhindwa jiulize ni maeneo gani unahitaji kuboresha zaidi. Ni vyema kujaribu makubwa ukashindwa, kuliko kufanya madogo na ukafanikiwa. Unajifunza zaidi kwenye kushindwa kuliko kufanikiwa.

Hatua ya kumi na tatu; fanyia kazi yale madhaifu yanayokurudisha nyuma.

Kila mtu ana udhaifu ambao unamzuia kufanikiwa. Kwa kuwa wengi hawachukui hatua ya kujijua wao wenyewe, au kupokea maoni ya wengine, hushindwa kuchukua hatua ya kujiboresha zaidi. Wanaofanikiwa wanajijua vizuri na wanajua madhaifu yao ni yapi na yanawazuiaje kufikia mafanikio. Kwa kujua madhaifu yao huchukua hatua na hivyo kuondokana na hali ya kushindwa.

FUNZO; Jijue vizuri kwa kufanya tathmini ya maisha yako na pia angalia maoni ambayo wengine wamekuwa wanakupa, jua ni madhaifu gani uliyonayo yamekuwa yanakurudisha nyuma. Yajue madhaifu hayo na angalia jinsi ya kuyafanya yasiwe kikwazo kwako kufanikiwa.

Hatua ya kumi na nne; jua hakuna tofauti kubwa kati ya kushindwa na kushinda.

Watu wengi hufikiri tofauti ya kushindwa na kushinda ni kubwa sana na hivyo wale wanaoshindwa wanaona hawawezi kufika upande wa pili. Lakini ukweli ni kwamba tofauti ya kushinda na kushindwa ni uvumilivu na ung’ang’anizi. Kama watu wawili wataanza kufanya biashara ya aina moja, katika mazingira sana, atakayeshinda siyo yule mwenye kipaji cha biashara au mwenye bahati. Bali atakayeshinda ni yule atakayeweza kuvumilia licha ya kupitia magumu. Kipaji, elimu, bahati na vingine vingi watu wanavyofikiria siyo vinavyotofautisha wanaoshinda na wanaoshindwa, bali uvumilivu.

FUNZO; Kwa jambo lolote unalofanya na unalotaka kufikia mafanikio makubwa, jiandae kuwa mvumilivu na ung’ang’ane hasa. Hata kama una elimu kubwa kiasi gani, hata kama una vipaji vingi kiasi gani, hata kama unapokea msaada mkubwa kutoka kwa wengine, kitakachokufikisha kwenye mafanikio ni uvumilivu wako. Ng’ang’ana mpaka mwisho na lazima utafanikiwa.

Hatua ya kumi na tano; Amka. Jikung’ute. Songa mbele.

Wanaofanikiwa mara zote wanaangalia sehemu moja kuu, mbele. Licha ya mengi wanayopitia, hawasahau kuangalia kule wanakokwenda. Wanapoanguka hawatumii muda mwingi kuangalia pale walipoanguka, bali wanaangalia kule wanakokwenda. Na hili linawapa hamasa ya kuamka na kusonga mbele.

FUNZO; Mafanikio hayatokani na mara ngapi umeanguka, bali umeinukaje baada ya kuanguka. Unapoanguka amka na jikung’ute kisha songa mbele. Hii safari siyo rahisi lakini uzuri ni kwamba inawezekana. Hata wewe unaweza, usikubali kubaki nyuma.

Tumia hatua hizi kumi na tano kuweza kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako. kushindwa kusiwe sababu ya wewe kurudi nyuma, bali tumia kushindwa kwako kama chachu ya kufikia mafanikio makubwa.

Kila la kheri.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz