Habari mpendwa rafiki na msomaji wa Amka Mtanzania? Natumaini unaendelea vyema katika kuboresha maisha yako. Karibu katika makala yetu ya leo ambapo leo tutajifunza chanzo cha maumivu ya ndani.
 
Maumivu ya ndani ni yale maumivu ambayo yako ndani ya nafsi na roho ni maumivu ambayo hayaonekani kwa nje ila yapo ndani ya mwili. Binadamu tunamuona mwili wake lakini roho na nafsi havionekani lakini tunaamini ni vitu ambavyo viko ndani ya mwili.
Watu wengi wamesongwa na maradhi mbalimbali, majeraha katika mioyo yao, maumivu yasiyokwisha ndani ya nafsi zao. Pia wamesongwa na mawazo na kumbukumbu mbaya zilizofichika ndani yao yote haya tunayaita maumivu ya ndani. 
 
Watu unawaona wanatembea wakiwa na nyuso za furaha lakini nafsini mwao wamebeba mizigo mizito, wengine wanateseka na maumivu ya ndani kwa sababu ya chuki, wivu, visasi na kutosamehe wengine. Watoto wadogo wanabebeshwa mizigo mizito katika nafsi zao kutoka kwa wazazi wao hata katika jamii inayomzunguka anaona vitu ambavyo viko chini ya umri wake au anafanyiwa vitu vilivyozidi umri wake.
Watu wengine walio katika maisha ya ndoa wanaishi maisha ya ujane wakati wangali hai. Kwanini wanaishi maisha ya ujane wakati bado wako hai? Baba katika familia anakuwa hatimizi wajibu wake kama baba yeye ni sauti tu ndani ya nyumba hakuna amani, furaha au upendo wala maelewano. Wanaishi maisha ya chuki ndani ya nyumba mazungumzo yao ndani ya nyumba ni ndio na hapana ndiyo yametawala. Mama naye katika familia anashindwa kutimiza wajibu wake yeye kama mama mazingira anayoishi na nyumba ni machafu, vyombo vichafu vitu vimekaa shaghalabaghala. Unakuta mama anawajibika katika mambo ya umbea na kuwajibika katika shughuli za watu na kuwa mstari wa mbele kabisa lakini nyumbani kwake hatoi thamani yake na kuwajibika kama mama.
Sasa kwa hali hii kama ni baba na mama wanaishi maisha hayo ni dhahiri kuwa ni maisha ya ujane kwani kila mmoja anakosa wajibu wa mwenzake na kutofurahia maisha kama mke na mume katika familia. Yote haya yanajaza na kusababisha chanzo cha maumivu ya ndani taratibu.

 
Sasa tuangalie chanzo na dalili ya maumivu ya ndani

Kumbukumbu Zilizofichika Ndani Ya Moyo;
Jambo lolote, mambo au tukio lililomkuta mama wakati mimba inatungwa , au wakati wowote wa ujauzito au anapojifungua tukio hilo huwa linajiandika ndani ya akili za mtoto. Hivyo, hali hii husababisha shida baadaye hata kama hujui.
Mfano; a) labda mimba ilipatikana kwa njia ya mama kubakwa.
b) labda wakati wa ujauzito mama alikuwa ni mtu wa kupigwa, kutukanwa au kusemwa na baba kila mara.
c) labda mama alikuwa mgonjwa kwa muda mrefu wakati wa ujauzito na mengine mengi. Kwa hiyo, mtoto atakayezaliwa katika matukio hayo hapo juu atazaliwa akiwa na hisia za huzuni nyingi, mtoto anaweza kuwa katika hali ya kushtuka shtuka na maradhi mbalimbali ambayo hata vipimo vya hospitalini havionyeshi.
SOMA; Mazungumzo Muhimu Yanayoweza Kubadili Maisha Yako Kabisa.

Kukosa Mahusiano Ya Karibu;
Mtoto anaweza kukosa mahusiano ya karibu labda pengine alifiwa na mzazi mmoja au wote wakati akiwa na umri mdogo. Labda mtoto alisemwa maneno yasiyostahili hasa na ndugu wa karibu, kama vile kumwita paka, mbwa, mpuuzi, mjinga n.k
Mtoto kusemwa kwa ukali na ndugu wa karibu bila kupewa nafasi ya kujieleza. Mtoto wa kike kubakwa na baba au ndugu wa karibu. Pia mtoto kulelewa na mzazi au wazazi katili sana n.k

Kukosa Mahitaji Ya Msingi ( upendo);
Mtoto kukosa kupendwa, kuthaminiwa, kutambuliwa huwa ni chanzo kingine cha maumivu ya ndani. Mfano; kutokuambiwa na wazazi au ndugu wa karibu kuwa ninakupenda.
Kutokukumbatiwa na wazazi hasa mtoto wa kiume kukosa kukumbatiwa na mama lakini pia, mtoto wa kike kukosa kukumbatiwa na baba kunawaletea watoto hao mihemko ya ajabu ya miili wanapoanza kukumbatiana hovyo na wanaodai kuwa wanawapenda.
Kuachwa bila kutiwa moyo au kupewa hongera wakati umefanya vizuri. Badala yake unalaumiwa na kutukanwa. Wazazi wa kiume kuwakataa watoto kutokana na mashaka yao kuhusu mimba ya mtoto huyo.

Kuvunjika Kwa Ndoa, Uchumba au Mkataba Mwingine Wowote Bila Kutolewa Sababu Za Msingi.
Hali hii huwa inawaathiri sana watu kisaikolojia , kukata tamaa ya maisha na kuona hawana sababu ya kuishi duniani. Vitu kama hivi huwa vinawapelekea watu kupata majeraha ya moyo na hatimaye maumivu ya ndani ambayo hayaonekani kwa nje.

Kusingiziwa Jambo;
Watu wengine husingiziwa mambo mbalimbali yanayosababisha maumivu ya ndani kama vile kusingiziwa wizi, mauaji, kuambiwa kuwa ni mchawi au amebaka n.k.

Kufanya Maamuzi Yasiyofaa.
Kuna wakati mwingine watu wanafanya maamuzi yasiyofaa lakini athari yake ni kubwa sana katika maisha yao. Mwingine anafanya maamuzi yasiyofaa kwa kuogopa jamii itamchukuliaje au ndugu au wazazi watamuonaje. Mfano kutoa mimba ni kitendo ambacho kinamwathiri mtoaji mimba kisaikolojia akikumbuka mimba au mimba alizotoa wakati kipindi ana uhitaji wa watoto halafu hawapati. Kuiba au kutaka kujiua na mengine mengi yanasababisha maumivu ya ndani.
SOMA; Mambo Kumi (10) Muhimu Ya Kuzingatia Kabla Hujafunga Ndoa Na Utajiri.

Kupewa Majina Ya Bandia;
Kupewa majina ya bandia yanasababisha maumivu ya ndani mfano wa majina ya bandia ni kama vile wasiwasi, mashaka, sikujua, shida, matatizo, masumbuko, mahangaiko n.k. Katika hali ya kawaida majina ya bandia ni maumivu makubwa sana kwa watoto na hata watu wazima. Majina hayambariki mtu na kumpa hamasa ya kusonga mbele na kujikomboa kimaendeleo.

Mwisho, ukiwa wewe ni mzazi au unatarajia kuwa mzazi epuka kumsababishia mtoto maumivu ya ndani ambayo yanamletea mzigo na majeraha ya moyo. Mazingira, sababu na mifano tuliyoona hapo yote husababisha maumivu ya ndani na wakati mwingine maumivu ya ndani hujitokeza nje ya mwili kama magonjwa lakini wakati mwingine sio rahisi magonjwa hayo kutambuliwa na vipimo vya kisayansi yaani hospitalini.
Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com au unaweza kutembelea tovuti yake www.actualizeyourdream.blogspot.com