Machaguo yanapokuwa mengi, akili inachoka na hivyo uwezo wa kufanya maamuzi sahihi unapungua. Hii ndiyo changamoto kubwa kwenye ulimwengu wa sasa ambapo machaguo ni mengi na kila siku yanazidi kuongezeka.

Leo hii ukitaka kununua kitu, utakuta vipo vitu vya aina nyingi, kujua kipi ununue ni changamoto ambayo inaweza kukuchosha kuamua kipi ununue. Hii inakufanya ushindwe kuwa na maamuzi bora.

Ili kuepuka kufanya maamuzi mabovu hakikisha una vigezo vyako binafsi ya kufanya maamuzi. Usifanye jambo lolote kama huna vigezo, kwa kukosa vigezo utaona kila kitu ni kizuri na hivyo kushindwa kujua kipi ni bora kwako. Kama ni kitu unataka kununua kuwa na vigezo vyako, kwamba kitu utakachonunua lazima kifikie vigezo hivyo. Ukikosa vigezo hivi utajikuta unasumbuka kuchagua.

Kitu kingine muhimu kufanya ni kupunguza machaguo. Hakikisha unakuwa na machaguo machache sana kwenye mambo yako binafsi. kwa mfano kama ukiamka unataka uweze kufanya shughuli zako vizuri, hakikisha kati ya kuamka mpaka kuanza shughuli zako unapunguza maamuzi mengi unayofanya. Kwa sababu kila unapofanya maamuzi unachosha akili yako na hivyo kushindwa kutekeleza majukumu yako kwa ubora. Vitu kama nivae nini, nile nini, nianze na nini, vinaweza kukuchosha kabla hata hujaanza kazi zako za siku.

Epuka machaguo mengi unayowekewa na wengine kwa kuwa na vigezo vyako mwenyewe. Na pia epuka machaguo mengi unayojiwekea mwenyewe kwa kupunguza maamuzi unayofanya.

SOMA; Usifanye Maamuzi Yako Kwa Kigezo Hiki, Utajuta Sana…

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba kadiri ninavyokuwa na machaguo mengi ndivyo ninavyokuwa na maamuzi mengi ya kufanya. Na kadiri ninavyofanya maamuzi mengi ndivyo ninavyochosha akili yangu na hivyo kushindwa kufanya maamuzi bora baadaye. Kuanzia sasa nitapunguza machaguo yangu ili niweze kufanya maamuzi machache na bora kwangu.

NENO LA LEO.

Kadiri unavyokuwa na machaguo mengi ndivyo unavyokuwa na maamuzi mengi ya kufanya. Maamuzi mengi yanapunguza uwezo wako w akufanya maamuzi bora.

Punguza machaguo yako na kuwa na maamuzi machache ya kufanya, itakuwezesha kufanya maamuzi bora kwako.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.