Habari za wakati huu rafiki yangu? Kama unasoma hapa kuna jambo moja nina uhakika nalo kuhusu wewe, umechagua safari ya kuwa na mafanikio makubwa kwenye maisha yako. najua umeshachoka kuwa kawaida na kuwashangilia wengine, sasa umeamua na wewe kufika kule ambapo wengine wamefika, hongera sana kwa hili rafiki yangu.
Safari uliyochagua kwenye maisha yako, ambayo ni safari ya kuishi maisha ya mafanikio ni safari nzuri sana kwenye maisha yako. ni safari ambayo itakuwezesha kuishi yale maisha ambayo ni ya ndoto yako, yenye maana kwako na yanayokuwezesha kuwa na mchango wako kwa watu wengine. Lakini pia safari hii siyo rahisi kama inavyoonekana kwa nje. Ni safari yenye vikwazo na changamoto nyingi. Ni safari ambayo kama una moyo mwepesi utakata tamaa haraka sana na kurudi kwenye maisha ya kawaida.
Kabla hujafikia hatua hiyo leo tutakwenda kujadili mambo muhimu ya wewe kuzingatia pale unapoelekea kukata tamaa. Kwa kuzingatia mambo haya utaweza kushinda ile hali ya kukata tamaa itakayokuwa inakunyemelea na kuweza kuendelea kuweka juhudi ili kuwa na maisha bora na ya mafanikio.
Safari hii ya mafanikio ina vikwazo na changamoto nyingi kwa sababu unahitajika kufanya vitu ambavyo hujawahi kufanya. Hapo awali ulikuwa umezoea kufanya kwa mazoea, kufanya vile ambavyo una uhakika wa kuvipata na hivyo kupata matokeo madogo sana. Lakini kwenye safari hii ya maisha ya mafanikio unalazimika kufanya vitu ambavyo hujawahi kufanya, vitu ambavyo huna uhakika kama utapata matokeo mazuri na hili linakuwa changamoto. Changamoto nyingine kwenye hili inatoka kwa wale wanaokuzunguka, kwa kuwa hawajawahi kuona mtu anafanya kwa tofauti, watakuona wewe kama unakosea na hivyo kukupinga. Bila ya kuwa na misingi ya kusimamia ni rahisi kuacha maisha haya na kurudia yale maisha ya zamani.

KUPATA KITABU HIKI BONYEZA MAANDISHI HAYA

Karibu tujifunze kwa pamoja mambo muhimu ya kuzingatia ili kuendelea na safari hii ya mafanikio bila ya kukata tamaa.

1. Jua kwamba siyo safari rahisi.
Tunapoona watu wengine wamefanikiwa, tunaona ni kitu rahisi ambacho hata sisi tunaweza kufanya. Na hivyo tunaanza kufanya na hapa ndipo tunapokutana na changamoto na kuona labda wale waliofanikiwa walikuwa na bahati ambayo wewe hujaipata. Ukweli ni kwamba watu hao hawakuwa na bahati kubwa bali waliweka juhudi, walikutana na changamoto nyingi lakini hazikuweza kuwatikisa kwa sababu walijua ni nini walikuwa wanataka na hawakuwa tayari kurudi nyuma. Kwa ung’ang’anizi wao huu waliweza kufikia mafanikio makubwa.
Na wewe pia kama unataka kufikia mafanikio unayotarajia kwenye maisha yako, ni lazima ujitoe hasa, ni lazima uwe tayari kuendelea kuweka juhudi hata pale unapokutana na changamoto kubwa. Kwa njia hii utakuwa na hamasa kubwa ya kuendelea kufanya hata mambo yanapokuwa magumu.

2. Jua kushindwa ni njia ya kufanikiwa.
Hakuna mtu aliyefanikiwa ambaye amekuwa anashinda kwenye kila jambo. Wale wanaofanikiwa wanashindwa mara nyingi kuliko wale ambao hawajafanikiwa. Kinachowafanya watu hawa wafanikiwe ni kujifunza kutokana na makosa yao na kufanya kwa ubora zaidi wakati mwingine. Safari hii ambayo umeichagua utashindwa mara nyingi, kama utakata tamaa pale unaposhindwa mara moja, hutaweza kuendelea na safari. Hivyo unaposhindwa usichukulie kama ni kushindwa, bali chukulia kama ni darasa la wewe kufanikiwa zaidi. Kila unaposhindwa jiulize ni somo gani nimejifunza hapa ambalo litaniwezesha kufanikiwa zaidi? Lijue somo hilo na litumie kwenye yale unayofanya.

3. Utawaudhi baadhi ya watu.
Nguvu kubwa inayowarudisha watu wengi nyuma ni ile jamii ambayo inawazunguka. Jamii zetu zimekuwa sumu kubwa kwenye safari hii ya mafanikio. Hii ni kwa sababu jamii imezoea kila mtu kufanya kile ambacho kila mtu anafanya. Sasa wewe unayetaka kufikia mafanikio makubwa unafanya vitu tofauti na kwa njia tofauti. Kwa hili jamii haikuelewi na watu wanaanza kuona unakosea au unapoteza muda wako. Kosa kubwa unaloweza kufanya hapa ni kuwasikiliza, au kutaka kuwaelewesha. Ukiwasikiliza wanakujaza hofu na utaacha, ukitaka kuwaelewesha kwamba upo sahihi hawapo tayari kukusikiliza na utapoteza muda wa kufanya yale ambayo ni muhimu zaidi. Unapokutana na changamoto hii ya kijamii, usiwasikilize wala usitake kuwaelewesha, badala yake fanya kwa vitendo na majibu wataona wenyewe.

4. Jua kuna gharama ambazo lazima ulipe.
Unapotaka kuwa na mafanikio makubwa, tumeona ni lazima ufanye vitu vikubwa, ambavyo hukuwahi kufanya hapo awali. Ili uweze kufanya vitu hivi ni lazima uache kufanya vitu vingine unavyofanya sasa. Kwa mfano sasa hivi una matumizi ya muda wako wote, utakapotaka kufanya jambo jipya, ni lazima uache baadhi ya mambo ya zamani ambayo ulikuwa unafanya. Hakuna safari ya mafanikio ambayo haina gharama za kulipa. Swala hili la gharama huwa linakuja pale mtu anapokutana na changamoto, anapofanya tathmini anaona jinsi gani safari hii ya mafanikio imemnyima vitu alivyokuwa navyo awali, na hivyo kuwa rahisi kukata tamaa. Wewe usifanye hivi, usiangalie ni vitu gani vizuri unakosa sasa, jua ya kwamba unaandaa vilivyo bora sana kwa baadaye.

5. Jua kwa nini unataka kufanikiwa na kwa nini mpaka sasa hujaacha.
Sababu ya wewe kufanikiwa inaweza kukupa hamasa sana pale unapokaribia kukata tamaa. Hivyo unahitaji kuwa na sababu inayokusukuma, sababu ambayo ni kubwa na siyo ya kutaka tu kuonekana kwamba na wewe umefanikiwa, au kupata tu fedha. Kadiri unavyokuwa na sababu kubwa, ndivyo inavyokupa hamasa ya kuendelea kufanya hata unapokutana na changamoto kubwa. Pale unapokuwa na sababu ambayo inawahusisha watu wengine, kwamba kile unachofanya kinafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi, unapata hamasa ya kuendelea hata unapokutana na magumu. Hii ni kwa sababu unajua ukiacha, kuna wengi wataumia kuliko hata wewe unavyoumia sasa. Zijue sababu zako kuu na mara zote jikumbushe sababu hizi.
 
Ni muhimu sana uwe na msingi sahihi pale unapochagua safari ya mafanikio, wengi wamekuwa wakianza safari hii na inawashindwa kwa sababu wanakosa msingi. Wewe msingi unao na kila siku utaendelea kujifunza, usikate tamaa wala kuacha safari hii, mafanikio yapo, yanataka kuona kama kweli umejitoa kuyapokea, ukikata tamaa unayapoteza, ukiendelea kukomaa lazima utayapata.
Nakutakia kila la kheri kwenye safari hii ya mafanikio.
TUPO PAMOJA,
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz