Kuna mtu ambaye amekuwa anasababisha wewe unashindwa kwenye mipango yako mbalimbali unayojiwekea. Mtu huyu amekuwa anavuruga furaha ya maisha yako na kuyafanya yawe magumu zaidi. Mtu huyu amekuwa kikwazo kwako kufikia yale malengo ambayo umejiwekea. Lakini uzuri ni kwamba mtu huyu unaweza kumdhibiti.
Ili uweze kumdhibiti mtu huyu unatakiwa kumjua vizuri na mtu huyu ni wewe mwenyewe. Kama umeshangazwa na hili au huelewi ni kwa namna gani umekuwa unajizuia mwenyewe usijali, tutakwenda taratibu mpaka tuelewane.
Kwa jambo lolote linalotokea kwenye maisha yako, maamuzi unayofanya wewe ndiyo yanafanya maisha yako yawe bora au yawe hovyo. Hata kama umekutana na hali ngumu kiasi gani, maamuzi unayofanya wewe mwenyewe, yanaweza kukusukuma kusonga mbele au kukurudisha nyuma.
Nguvu ya kufanikiwa au kushindwa ipo ndani yako. Kama utafanya maamuzi bora utafanikiwa na kama utafanya maamuzi mabovu utashindwa.
Umekuwa unachangia kushindwa kwako mwenyewe kwa njia mbalimbali;
Umekuwa unatafuta njia rahisi ya kupata kile unachotaka, hakuna njia hiyo na hivyo unapoteza muda.
Umekuwa unatafuta njia ya mkato ya kupata unachotaka, ukiipata inakuletea matatizo zaidi baadaye.
Umekuwa unakata tamaa unapokutana na changamoto kidogo na hivyo kujiondoa kabisa kwenye matarajio ya mafanikio.
Umekuwa unapoteza muda kwenye vitu ambavyo siyo muhimu kwako na hivyo kushindwa kuweka muda kwenye vitu ambavyo ni muhimu.
Umekuwa unaambatanisha furaha yako na vitu na hivyo unapokosa vitu hivyo unakosa furaha na kuona maisha hayana maana.
Unahitaji kufanya mabadiliko kwenye maisha yako, kuchagua maisha unayotaka kuishi na kuweka juhudi katika kufikia maisha hayo, kufanya jambo sahihi kwa wakati sahihi na kujua chanzo cha furaha ni wewe mwenyewe na siyo vitu au watu wengine.
SOMA; Kuwa Na Maisha Bora Kunaanza Na Wewe Kuweza Kusimama Mwenyewe Na Unaweza Kusimama Hivi….
TAMKO LANGU;
Najua ya kwamba mafanikio au kushindwa kunaanza na mimi mwenyewe. Hata kama yanayotokea ni mazuri au mabaya kiasi gani, mafanikio au kushindwa kwangu kunatokana na maamuzi ninayofanya. Nitaendelea kufanya maamuzi bora kwangu ambayo yatanifanya niwe na maisha bora na yenye mafanikio makubwa kwangu.
NENO LA LEO.
Mtu pekee anayekufanya wewe ushindwe ni wewe mwenyewe.
Kile kinachotokea nje yako, kiwe kizuri au kibaya, kinategemea maamuzi utakayofanya. Ukifanya maamuzi bora unaweza kugeuza hali mbaya na ikawa nzuri. Ukifanya maamuzi mabovu hata hali nzuri itageuka na kuwa mbaya.
Jua wewe ndiyo chanzo cha kila kinachotokea kwenye maisha yako, na kuwa makini na maamuzi unayofanya kwenye maisha yako.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.