Unawezaje kujua kama maisha yako ni bora kama ambavyo umekuwa unataka kuwa na maisha bora? Jibu ni rahisi, unaangalia matokeo unayopata kwenye maisha yako. Kama yanaendana na vile unavyotaka basi una uhakika maisha yako ni bora. Kama yanakwenda kinyume, kuna tatizo mahali.
Njia bora ya kupima kile unachofanya na kuangalia kule unakokwenda ni kupima matokeo unayopata. Hii ni njia ya uhakika ambayo haiwezi kukudanganya kwenye jambo lolote kuhusu maisha yako. Matokeo unayopata yatakupa mwanga kama unafanya kitu sahihi au la.
Kwa mfano kama wateja wanakuja kwenye biashara yako, halafu wanarudi tena, huku wakiwaambia watu wengine kuhusu biashara yako, haya ni matokeo kwamba unatoa huduma nzuri kupitia biashara yako. Lakini kama mteja anakuja siku moja halafu humuoni tena, ni matokeo kwamba kuna kitu hakipo sawa kwenye biashara yako.
Kama kila unapoamka asubuhi una shauku kubwa ya kuianza siku yako, ukiwa unajua kabisa ni nini unakwenda kufanya, ni matokeo kwamba una furaha na maisha yako na unaendea kile unachotaka. Lakini kama unaamka kama ugomvi, unatamani siku hiyo isingekuwepo, ni matokeo kwamba unachofanya siyo kile unachotaka.
Hakuna kitu kizuri kama kuongozwa na matokeo kwa sababu matokeo hayadanganyi. Kama unafanya kitu sahihi na unakifanya vizuri utaona matokeo mazuri, hata kama siyo kwa haraka. Na kama unafanya kitu ambacho siyo sahihi pia utayaona matokeo mabaya.
Mara zote fanya tathmini ya kila jambo unalofanya kwa kuangalia matokeo uliyopata na boresha zaidi kwa kujiuliza unawezaje kupata matokeo mazuri kuliko unayopata sasa. Hivi ndivyo waliofanikiwa wanafanya kila siku kwenye maisha yao. Ila wale walioshindwa wanafanya kwa mazoea, wanarudia kufanya kile ambacho walifanya jana, bila ya kujali kama kinaleta matokeo mazuri au mabaya. Na kwa kuwa matokeo mazuri huwa yanaonekana taratibu, huwa hawajisumbui kutafakari matokeo wanayopata.
Kuanzia sasa ongozwa na matokeo na kila jambo unalofanya litathmini kwa kuangalia matokeo uliyopata. Na mara zote jiulize ungewezaje kupata matokeo bora zaidi. Hii ndiyo njia nzuri ya kuwa bora zaidi kwenye kile unachofanya na kuwa na maisha ya furaha na mafanikio.
SOMA; NENO LA LEO; Haya Ndio Mambo Matatu Yatakayokuletea Matokeo Ya Kushangaza.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba kipimo bora cha kujua kule ninakokwenda na juhudi ninazoweka ni matokeo. Kila mara nitakuwa napima matokeo ninayopata kwa kila ninachofanya. Kupitia matokeo haya nitajiuliza ni kwa namna gani naweza kupata matokeo bora zaidi na kufanyia kazi majibu nitakayopata.
NENO LA LEO.
Kipimo bora cha kujua kule unakokwenda ni matokeo unayopata.
Kama unapata matokeo mazuri maana yake kuna vitu unafanya kwa ubora. Na kama unapata matokeo mabaya ni dhahiri kuna vitu ambavyo huvifanyi vizuri.
Tathmini kila jambo unalofanya kwa kuangalia matokeo unayopata na kisha jiulize unawezaje kupata matokeo bora zaidi wakati mwingine. Hii ni njia ya uhakika ya kuwa bora zaidi kila siku.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.