Kitu muhimu sana kwenye maisha ni kuwa na uhuru, kuweza kuyaendesha maisha yako kwa vile unavyotaka wewe bila ya kuingilia maisha ya wengine ni kitu muhimu sana. Maisha yenye uhuru ndiyo maisha yenye furaha na mafanikio.

Lakini wengi wanakosa uhuru huu na sio kwa kunyang’anywa bali kwa kuamua kuupoteza wao wenyewe. Watu wanachagua kuacha uhuru na kujiweka kwenye vifungo au utumwa wa kujitakia wao wenyewe.

Njia moja kubwa ambapo watu wanatumia kupoteza uhuru wao ni kuweka umuhimu mkubwa kwenye vitu ambavyo vipo nje yao. Pale unapoona ya kwamba kuna kitu ambacho ni muhimu sana kwenye maisha yako, kwamba bila ya kitu hiko unaona kama kaisha hayawezi kwenda basi umepoteza uhuru wako kwenye kitu hiko. Inawezekana pia ikawa mtu, kwamba umeshajiwekea mtu huyo ni muhimu sana na maisha yako hayawezi kwenda bila ya yeye, hapa umepoteza uhuru wako kwa sababu utalazimika kufanya mambo ambayo siyo bora kwako ili kumridhisha.

Unahitaji kujua ya kwamba watu na vitu vyote vinavyokuzunguka vina mchango mkubwa kwako kufanikiwa, lakini siyo kuchukulia kwamba bila ya watu au vitu hivyo maisha yako hayawezekani. Ni lazima ujue ya kwamba una nguvu kubwa ndani yako, na uwezo mkubwa wa kuweza kutengeneza au kutumia watu na mazingira mengine kupata kile unachotaka.

Hii pia haimaanishi uanze kuwadharau watu au vitu kwa sababu unataka uhuru, badala yake unavipa uzito unaostahili, kwa kujua vina mchango kwako na wewe una mchango kwa wengine. Ya kwamba kama vitaondoka au kama ni watu wataondoka unaweza kutafuta wengine au kutafuta vitu vingine.

Usipoteze uhuru wako kwa kufanya maisha yako yote yaegemee kwa watu fulani au vitu fulani. Ni lazima ujue kwamba utaendelea kusimama hata kama watu au vitu hivyo vitaondoka. Mabadiliko yanatokea kila siku, kung’ang’ana na kile ulichozoea kutakuacha nyuma wakati wenzako wanasongambele.

SOMA; Hivi Ndivyo Waajiriwa Wanavyopoteza Uhuru Wao Wenyewe, Na Jinsi Ya Kuudai Tena.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba napoteza uhuru wangu kwa kufanya maisha yangu yote yategemee watu fulani au vitu fulani. Nimejua ya kwamba uhuru unaanzia ndani yangu kwa kujua ya kwamba hata kama mabadiliko yatatokea, naweza kusimama na kuendelea. Nitaweka uzito sahihi kwa watu na vitu sahihi na kama vikiondoka bado nina uhakika nitaendelea kusimama kwa sababu najua vyote vinaanza na mimi.

NENO LA LEO.

Unapoweka mategemeo yako yote ya maisha kwa watu au vitu fulani hapo ndipo unapopoteza uhuru wako kwenye maisha.

Ni lazima ujue ya kwamba unaweza kusimama mwenyewe hata kama vile unavyotegemea vitaondoka.

Usikubali wengine ndiyo waamue utakuwa na maisha gani, au uwe na furaha au la. Haya ni maamuzi ya kufanya wewe mwenyewe, kwa kujua ya kwamba hata mambo yakibadilika bado utaendelea kusimama.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.