Kabla watu hawajanunua kile unachouza, wanakununua wewe kwanza.

Kabla watu hawajakubali kile unachowaambia, lazima wakukubali wewe kwanza.

Kwa asili binadamu tunapenda kuhusiana na wale ambao tunawajua vizuri, na tunajua wanaendana na sisi. Watu ambao wanaonekana ni wageni kwetu wanatupa wasiwasi. Hatuna hakika kama wanajali maslahi yetu au wanataka kututapeli.

Hivyo kwa chochote unachofanya, iwe ni kazi, biashara na hata mahusiano, hakikisha unauzika kwanza, hakikisha unakubalika wewe kama wewe kwanza, kabla ya vingine vyote. Ukishaweza kukubalika. Watu wakoana upo kwa maslahi yao, utajenga mahusiano bora sana na utaweza kufikia chochote unachokitaka.

Na hii ndiyo sababu watu wanapokwenda kuomba kazi wanakuwa na wasifu ambao una watu wanaoweza kuulizwa kuhusu wao (referee). Hii ni kutaka kumwondolea mwajiri mpya wasiwasi kwamba mtu huyu ni mwema au la. Kwa kuwa na mtu ambaye anakukubali inaonesha kuna kitu kikubwa unacho.

Na hata kwenye biashara, ni rahisi zaidi kununua kwa mtu ambaye ulishanunua kitu kingine kwake na ukakipata, kuliko kununua kwa mtu mpya ambaye hujawahi kumuona tena.

Mfano mzuri, ukiingia kwenye mtandao sasa hivi na ukakuta tangazo kwamba tuma elfu kumi utumiwe kitabu, na anayetoa tangazo hilo humjui, huwezi kutuma. Lakini kama ukikuta tangazo hilo limetolewa na mtu unayemfahamu kama mimi, ambapo ulishatuma fedha hapo awali na ukapata kitabu kweli, au umekuwa unanifuatilia kwa muda mrefu, itakuwa rahisi zaidi kwako kutuma.

Fanya lengo lako kubwa iwe ni kuuzika, uwe ni kukubalika kwa kuchagua watu unaotaka kujenga nao mahusiano mazuri na kisha kufanya kile ambacho kinaendana nao. Wanasema ndege wanaofanana wanaruka pamoja, na hata binadamu wenye tabia sawa ndiyo wanakubaliana na kufanya mambo ambayo ni sawa kwao.

Swali ni je unauzika kwenye kazi yako? unauzika kwenye biashara yako? unakubalika kwenye mahusiano mbalimbali uliyopo kwenye jamii. Hivi ni vitu vya kufanyia kazi kila siku. Kwa sababu kama tunavyojua, chochote unachotaka sasa hivi, utakipata kutoka kwa mtu mwingine. Kadiri unavyouzika na kukubalika kirahisi, ndivyo inavyokuwa rahisi kwako kupata kile unachokitaka.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU 52 WEEKS OF SALES SUCCESS.

TAMKO LANGU;

Nimejifunza watu hawanunui kile ninachouza bali wananinunua mimi kwanza. Pia watu hawakubaliani na kile ninachosema, bali wananikubali mimi kwanza. Nitaweka juhudi kwenye kuimarisha mahusiano yangu na watu wengine kwa sababu najua mahusiano haya ndiyo yatanipatia chochote ninachotaka kwenye maisha yangu.

NENO LA LEO.

Kabla watu hawajanunua kile ambacho unauza, wanakununua wewe kwanza.

Kabla watu hawajakikubali kile unachowaambia, wanakukubali wewe kwanza.

Unahitaji kujiweka kwenye hali ambayo watu wanakuwa rahisi kukununua na kukukubali.

Chochote unachotaka kwenye maisha yako, utakipata kutoka kwa wengine. Tengeneza mahusiano mazuri na wengine na utapata chochote unachokitaka.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.