Tunapozungumzia mafanikio, wapo wengi ambao huwa wanafikiri kwamba watafanikiwa kama watafanya kazi fulani ambazo kwa nje zinaonesha mafanikio. Labda kama akiwa daktari au rubani au injinia ndiyo ataweza kufanikiwa.
Huu sio ukweli, mafanikio tunayozungumzia hayatoki nje yako, bali yanaanzia ndani yako. Mafanikio yako yanaanza na kile ambacho unakifanya sasa, pale unapoweza kukifanya vizuri kwa viwango vya juu sana, na kuwa na mchango kwa wengine unapata thamani kubwa.
Kwa maana hii kila mtu anayo nafasi kubwa ya kufanikiwa kwa jambo lolote ambalo analifanya, hata kama itakuwa ni kufagia barabara. Barabara lazima zifagiliwe, kwa sababu wote tunahitaji kupita sehemu ambayo ni safi. Yule awezaye kufagia barabara vizuri akijua ya kwamba anatoa huduma kwa wengi, mafanikio yake yapo kwenye hiko anachofanya.
Kwa maana nyingine ni kwamba hapo ulipo sasa hivi tayari una kila unachohitaji ili ufanikiwe. Kilichobaki ni wewe kuweka juhudi kubwa, ukawa tayari kwenda hatua ya ziada na mara zote kuboresha zaidi kile ambacho unafanya. Mafanikio yanaanzia ndani yako na yanaanza na wewe mwenyewe.
Usisubiri tena, bali chukua hatua kufika pale unapotaka kufika, ukianzia hapo ulipo sasa.
SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; FAIL FORWARD (Hatua 15 Za Kufikia Mafanikio Kupitia Kushindwa).
TAMKO LANGU;
Najua ya kwamba mafanikio hayatoki nje yangu, bali yanaanzia ndani yangu. Najua mafanikio hayajatengwa kwa watu fulani wanaofanya kazi fulani. Mafanikio yapo kwa kila mtu anayechagua kuyafikia. Mimi nimeshachagua na nina uhakika wa kuyafikia. Ninaweka juhudi kubwa na ubora kila siku kwenye hiki ninachofanya ili nifanikiwe zaidi.
NENO LA LEO.
Mafanikio hayatoki nje ya mtu, bali yanaaniza ndani yake.
Mafanikio hayajatengwa kwa watu fulani wanaofanya kazi fulani.
Mafanikio yapo kwa kila anayechagua kufanikiwa, bila ya kujali anafanya nini.
Mafanikio ni zao la maarifa, juhudi na kutokukata tamaa.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.