Nachukua nafasi hii kuwakaribisha kwenye darasa la leo ambapo tutakwenda kujifunza kuhusu uwekezaji wa HATI FUNGANI kwa kiingereza BONDS.
Katika darasa la leo tutajifunza yafuatayo;
1. Maana ya uwekezaji kwenye masoko ya mitaji.
2. Maana ya uwekezaji kwenye hatifungani.
3. Mfumo wa uwekezaji wa hati fungani na faida zake.
4. Tofauti ya uwekezaji wa hati fungani na masoko mengine ya mitaji kama hisa.
1. MAANA YA UWEKEZAJI KWENYE MASOKO YA MITAJI
Uwekezaji kwenye masoko ya mitaji ni aina ya uwekezaji ambapo watu wenye mitaji ya kifedha wanaweza kuiweka kwenye shughuli mbalimbali zanuzalishaji ambapo wao hawahusiki moja kwa moja.
Badala ya kutumia fedha zako mwenyewe kuanzisha biashara au kufanya kitu kingine ambacho kitakuhusisha wewe moja kwa moja, unatoa fedha hiyo kwa wale ambao wanaweza kuitumia na wewr kupata faida kulingana na makubaliano yaliyopo.
Uwekezaji huu unafanyika kwa njia kama ununuaji wa hisa kwenye kampuni mbalimbali, ununuaji wa hati fungani na pia uwekezaji kwenye biadhara za wengine (venture capital.)
Masoko ya mitaji ni moja ya njia ambazo uwekezaji unakuwa rahisi kuugeuza kwenye fedha, yaani liguidity.
Kwa mfano unaponunua shamba kama uwekezaji, shamba hilo linaweza kuwa na thamani ya milioni kumi, ila siyo rahisi kuzipata milioni hizo kumi ndani ya muda mfupi.
Lakini uwekezaji kwenye masoko ya mitaji unaweza kupata mtaji uliowekeza ndani ya muda mfupi.
2. MAANA YA UWEKEZAJI KWENYE HATIFUNGANI.
Hatifungani au BONDS kama inavyojulikana kwa kiingereza ni moja ya mifumo ya uwekezaji kwenye masoko ya mitaji.
Kwa uwekezaji huu wewe mwekezaji unakuwa unaikesha kampuni au taasisi fedha zako, inafanyia biashara halafu inakupa wewe riba na mwisho unarudishiwa ule msingi uliowekeza.
Kwa mfano tusema kampuni inataka kufanya mradi unaohitaji milioni mia moja za fedha, lakini fedha hizo hawana. Wanaweza kutoa bonds ambapo wanakusanya mtaji huo wa milioni mia moja kutoka kwa watu, halafu watakuwa wanawalipa watu wale riba kwa kutumia fedha zao kufanya mradi wake. Na mwisho watawarudishia watu wale zile fedha walizowekeza.
Kwa ligha nyingine tunaweza kusema mfumo wa hati fungani ni kama wewe unayezinunua unaikopesha taasisi inayouza hatifungani hizo na hivyo itakulipa fedha zako pamoja na riba.
Hatifungani huwa zinatolewa na serikali, taasisi za kiserikali na baadhi ya mashirika ya umma.
Hii ni njia inayotumiwa na taasisi na mashirika haya kupata fedha wanazohitaji kwa shuguli zao za uzalishaji.
3. MFUMO WA UWEKEZAJI WA HATIFUNGANI NA FAIDA ZAKE.
Kama tulivyoona hapo juu, kwenye hatifungani wewe mwekezaji unaikopesha taasisi fedha zako, inatumia kwenye shughuli zake na wewe inakupanriba pamoja na msingi wako.
Faida inayopatikana kwenye hatifungani ni kwa kiwango vha riba ambacho taasisi hiyo inatangaza kutoa kwa wale wanaowekeza.
Kiwango hiki cha riba huwa kinatolewa kwa asilimia ya mtaji ambao umewekeza na huwa ni kwa mwaka.
Kwa mfano kama utaambiwa hatifungani ina riba ya asilimia kumi kwa mwaka, maana yake kwa ile fedha unayowekeza, ndani ya mwaka mmoja utapewa riba ya asilimia 10.
Kama utawekeza milioni moja, kwa mwaka utapewa riba ya laki moja, kwa sababu asilimia 10 ya milioni moja ni laki moja. Na hesabu zinakwenda hivyo kwa viwango mbalimbali.
Kuna taratibu mbalimbali za kulipa riba kwenye uwekezaji wa hati fungani.
Kuna utaratibu ambapo mwekezaji analipwa mara moja kwa mwaka, na utaratibu mwingine unalipwa riba mara mbili.
Kwa kutumia mfano wetu hapo juu, kama umeweka milioni moja ambayo inakupa riba ya shilingi lakinmoja kwa mwaka, kama unalipwa mara moja kwa mwaka utapewa laki yako mwaka unapoisha.
Kama inalipwa mara mbili, utaliwa elfu hamsini baada ya miezi sita, na elfu hamsini nyingine baada ya miezi sita.
Kwenye mfumo huu wa uwekezaji wa hatifungani, huwa zinatolewa kwa kipindi maalumu na zina urefu maalumu. Kuna ambazo ni za miaka miwili, nyingine miaka mitano na hata nyingine miaka kumi.
Kwa hiyo unaponunua hatifungani ambazo urefu wake ni miaka mitatu, unapoweka fedha zinapaswa kukaa kwa miaka hiyp mitatu. Hapo katikati hutazitoa badala yake utakuwa unapewa riba yako tu.
Lakini kama unataka fedha yako, basi kuta taratibu za kuweza kupewa, ikiwa ni pamoja na hatifungani yako kuuzwa kwa wengine kupitia soko la hisa.
Ule muda wa mwisho wa hati fungani huwa tunasema imekomaa (mature) hivyo kama umenunua hati fungani ya miaka mitatu, itakomaa baada ya miaka mitatu na ndo unaweza kuchukua msingi wako.
4. TOFAUTI YA UWEKEZAJI WA HATIFUNGANI NA MASOKO MENGINE YA MITAJI KAMA HISA.
Hatifungani ni tofauti kabisa na masoko mengine ya mitaji kwa mfumo wake na hata faida zake.
?Kwenye hatifungani unapata faida bila ya kujali uchumi unakwendaje. Kwa sababu unaponunua hati fungani unajua kabisa ni riba kiasi gani unapata kwa mwaka. Lakini kwenye hisa hujui ni faida kiasi gani unapata kwenye uwekezaji wako. Faida inategemea na halinya uchumi, uimara wa soko.
? Kwenye hisa unapata faida pale hisa zinapofanya vizuri na unapata hasara pale hisa zinapofanya vizuri. Kwenye hatifungani unapewa riba uliyoambiwa bila ya kujali fedha ulizowekeza zimezalisha au la.
? Kwenye hisa unaweza kupata faida kubwa sana pale uchumi unapokwenda vizuri. Kwenye hatifungani utapata riba ile ile.
? Hatifungani zina kipindi maalumu baada ya hapo zinakomaa na hivyo kurudishiwa fedha zako. Hisa hazina ukomo wa kipindi, kadiri kampuni inavyoendelea kuwepo unaweza kuendelea kumiliki hisa zake.
? Kwenye hisa unaweza kushiriki kwenye vikao mbalimbali vya kampuni, kwenye hatifungani hupati nafasi hiyo. Wewe unawekeza fedha na kuchukua riba mpaka pale inapokomaa.
Pia hatifungani inatofautiana na kuweka fedha kwenye akaunti maalumu za muda, yaani FIXED ACCOUNT kama ifuatavyo;
? Kwenye akaunti za muda riba huwa inakuwa ndogo sana lakini kwenye hayifungani riba huwa inakuwa kubwa.
? Kwenye akaunti za muda huwezi kutoa fedha zako bila ya muda kuisha, kwenye hatifungani unaweza kutoa fedha zako kabla hatifungani haijakomaa, kuna utaratibu wa kufanya hivyo.
? Kwenye akaunti ya muda fedha zako zinalimbikizwa, yaani compound interest kwa mfano ukiweka kwenye akaunti ya muda ambayo riba yake ni asilimia 5 kwa mwaka, ukiweka milioni moja kwa mwaka unapata elfu 50. Sasa unapokwenda mwaka wa pili, msingi wako unakuwa siyo milioni moja tena, bali milioni moja na elfu 50. Na hivyo riba utakayopata kwenye mwaka wa pili itakuwa zaidi ya elfu 50. Kwenye hatifungani hakuna ulimbikizaji wa riba, unapewa riba yako kila baada ya kipindi ambacho umeambiwa, kama ni mwaka mmoja au miezi sita.
Hatifungani ni moja ya aina ya uwekezaji unaofanyika kwenye masoko ya mitaji. Kwa kuwa na taarifa sahihi na kisha kuchukua hatua unaweza kunufaika na uwekezaji huu.
…..Kwa kuwa na taarifa sahihi na kuchukua hatua unaweza kunufaika na UWEKEZAJI……. Taarifa sahihi zinapatikanaje?
LikeLike
Taarifa sahihi unazipata kwa kufuatilia masoko ya mitaji na mambo ya uwekezaji.
Moja ya sehemu unazoweza kupata taarifa sahihi ni kwenye SOKO LA HISA LA DAR ES SALAAM DSE, unawesa kutembelea toviti yao http://www.dse.co.tz
Pia unaweza kupata taarifa kupitia madalali wa soko la hisa, tovuti na mawasiliano yao yapo kwenye tovutibya dse.
LikeLike
Kwa maoni yangu, CRDB ni kati ya benki zinazofanya vizuri hapa Tanzaznia. Hisa zake si za thamani kubwa ukilinganisha na hisa za mabenki mengine yanayofanya vizuri. Hii ni kwa nini?.
LikeLike