Ushauri Muhimu Kwa Waandishi Na Waendeshaji Wa Blog Za Mafunzo.

Habari za leo rafiki?
Napenda kuchukua nafasi hii kuongea na waandishi na waendeshaji wa blog za mafunzo mbalimbali. Hapa nazungumzia zile blog ambazo zinaweka makala za watu kujifunza na siyo kuripoti habari.
Kwanza kabisa nichukue nafasi hii kukupongeza kama wewe ni mwandishi au mtu unayeendesha blog ya watu kujifunza. Ni kazi kubwa sana ambayo umechagua kufanya na kazi hii haiendi bure, kuna watu ambao wanapata mwanga na wanaweza kuboresha maisha yao. Ni kazi ambayo ina mchango mkubwa sana kwenye mabadiliko ya kijamii hata kama hayaonekani kwa haraka. Nasema hongera kwa kuchagua kuwa sehemu ya mabadiliko kwenye maisha ya wengine.
Miaka mitatu iliyopita hakukuwa na blog nyingi za mafunzo kama zilivyo sasa. Blog zilikuwa zinaonekana kama sehemu ya kupashana habari na hazikupewa uzito hasa kwenye kujifunza. Lakini leo hii kumekuwa na blog nyingi ambapo watu wanaweza kutembelea na kujifunza. Hii ni hatua nzuri sana hasa kwa nchi kama yetu ambapo elimu ya utambuzi na maarifa muhimu ya kuwa na maisha bora haitolewi kwenye mifumo ya elimu au kwenye jamii zetu.

KUPATA KITABU HIKI BONYEZA MAANDISHI HAYA

Kazi bado ni kubwa.
Pamoja na juhudi kubwa tunazofanya kuwaelimisha watu kupitia maandiko yetu, kazi bado ni kubwa sana. Bado hatujaweza kuwafikia watu wengi na kuwapatia elimu hii muhimu ili wao kuweza kubadilika na kuwa na maisha mazuri huku wakipata kile wanachokitaka. Bado kuna watu wengi wanaishi maisha ya mazoea badala ya maisha yanayoendana na nyakati tulizo kwa sasa.
Hii ina maana ya kwamba bado tunahitaji waandishi wengi zaidi na bado tunahitaji blog nyingi zaidi za mafunzo. Kuna watu wamekuwa wanafikiri ya kwamba kwa sasa tumeshakuwa na blog nyingi mno hakuna tena nafasi ya blog mpya za mafunzo kuingia kwenye tasnia hii. Mimi nalikataa hili kwa sababu bado jamii zetu hazijapata elimu sawasawa.
Kila ninapoona mtu anafanya maamuzi mabovu kutokana na kukosa maarifa sahihi naona kwamba bado hatujafanya kazi zetu vizuri. Kila ninaposikia mtu anasema kwamba chuma ulete ndiyo wanamrudisha nyuma kwenye biashara yake naona bado hatujatoa elimu ya kutosha kwa watu kuhusu uendeshaji wa kisasa wa biashara. Kila ninapoona watu wakilalamika na kuwalaumu wengine kwa mambo yanayowatokea kwenye maisha, naona ni jinsi gani watu bado wanahitaji kujua majukumu ya maisha yao.
Kila ninapokutana na kundi la vijana ambao wanacheza mchezo wa kamari/kubashiri maarufu kama betting ili wapate fedha naona ni jinsi gani bado hatujaweza kutoa elimu sahihi kuhusu njia za uhakika za kujipatia kipato. Kila ninapoona watu ambao wanasubiri serikali ndiyo iwaletee yale maisha ambayo wanayataka naona jinsi ambavyo bado tuna kazi kubwa ya kufanya.
Jamii zetu zimejaa watu wa aina hii na hivyo bado kuna kazi kubwa ya kufanya. Na kazi hii inatuhitaji sisi na wengine wengi kuweza kutoa mafunzo ambayo yataleta mabadiliko kwenye jamii zetu na hatimaye tunakuwa na taifa la watu wanaojua majukumu yao na kuweza kuweka juhudi ili kupata kile wanachokitaka. Hivyo mtu anapokuambia kwamba blog za mafunzo zimekuwa nyingi, mwoneshe kazi kubwa ambayo bado haijafanywa.

Changamoto kubwa inayotukabili waandishi na wamiliki wa blog za mafunzo.
Kuna changamoto moja kubwa ambayo inatukabili waandishi na waendeshaji wa blog hizi za mafunzo. Na changamoto hii ni kufanya kitu kile kile. Imefika wakati kwamba kila tunachoandika kinafanana sana, kwa mtindo ambao unaendana. Na hii inafikia wakati msomaji akisoma blog tano zote zinaeleza kitu kimoja na hata aina ya uandishi ni moja. Hii inawachosha wasomaji na kuona hakuna kipya kwenye blog hizi.
Na hili siyo kwamba nasema tu bali limetokea kwa baadhi ya wasomaji kuwalalamikia waandishi wengine kwa kuwa na aina moja ya uandishi na hivyo kushindwa kujitofautisha. Hii ni changamoto kubwa kwa sababu inakupotezea muda wewe kama mwandishi na kushindwa kuwafikia watu wengi.

Ushauri muhimu kwa waandishi na waendeshaji wa blog za mafunzo.
Ushauri ninaotaka kukupa leo rafiki yangu ni kuhusu changamoto hiyo ya kushindwa kujitofautisha katika tasnia hii. Leo nataka nikupe ushauri wa jinsi gani ya kuweza kuboresha uandishi wako ili uweze kujitenga kwenye kundi.
Kitu kimoja ninachotaka kukushauri uanze nacho ni kuwa na sauti yako mwenyewe. Tengeneza sauti yako ya tofauti na ya kipekee ambayo wasomaji wako wataweza kuijua na kuifuata vizuri. Kwa kujitengenezea sauti yako unaweza kutengeneza hadhira ya wasomaji wako ambao wanakuelewa vizuri. Sauti ninayozungumzia hapa ni ule mtindo wako wa uandishi.
Kumekuwa na wimbi kubwa la blog zinazoanzishwa ambazo mtindo wa uandishi ni kama uliopo kwenye AMKA MTANZANIA. Watu wengi wanaochagua kuandika makala za kufundisha wamekuwa wakitumia mtindo ambao mimi natumia. Hili limekuwa linawanyima fursa ya ukuaji wa blog zao kwa sababu wasomaji wanapoanza kusoma wanaona hakuna jipya na hivyo kuacha.
Nilishaandika kitabu cha jinsi ya kuanzisha blog na kuandika makala bora ambazo zitajenga hadhira bora. Watu wengi wamekisoma kitabu hiki na kimewahamasisha sana kuwa na blog zao na kuandika makala nzuri. Lakini kitu kimoja ambacho watu wengi wanakosea ni kusahau kujitofautisha na kutengeneza sauti zao wenyewe. Wanaona kwa kuwa aina fulani ya uandishi imeshaweza kutengeneza wasomaji wengi, basi ni rahisi kwao kama wataendelea na aina hiyo ya uandishi. Lakini hapa ndipo wanapojipoteza wao wenyewe.
Huwezi kuwa mwandishi bora kama unaandika chini ya kivuli cha mtu mwingine. Unahitaji kutengeneza sauti yako mwenyewe, sauti ambayo wasomaji wako wakianza kusoma tu hata kama hakuna jina wanajua huyu ni fulani kaandika. Ili kutengeneza hili unahitaji kuwa na mtindo wako wa tofauti kabisa wa kuandika.
Kuna wakati inafika watu wanasoma makala zako siyo kwa sababu wanataka kujifunza ulichoandika, bali kwa sababu wanajua kuna vingine vingi watajifunza. Kwa mfano unaweza kuandika makala kuhusu waajiriwa, lakini wafanyabiashara wakaisoma kwa sababu wanajua ndani yake watajifunza vitu vingi hata kama makala haiwahusu moja kwa moja. Hiki ndiyo unachotakiwa kukifikia, na inawezekana kama utaacha kabisa kuangalia wengine wanaandika nini na wewe kuchagua kuandika kwa mtindo wa kipekee kwako.
Kitu kimoja unachotakiwa kupigania ni kuwa tofauti katika uandishi wako na kujitenga na kundi kubwa la waandishi ambao wanafanana kwenye mtindo wao wa uandishi. Hii siyo kazi rahisi lakini inawezekana. Siyo kazi rahisi kwa sababu mwanzoni watu wanaweza wasielewe mtindo wako, lakini kadiri unavyokwenda wataanza kukuelewa na utatengeneza wasomaji wengi na wazuri.
SOMA; JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG 

Hitimisho; choma vitabu vyote vya mwongozo.
Katika vita kuu ya pili ya dunia, Jenerali wa kivita wa marekani Douglas MacArthur alipewa ukamanda wa majeshi ya marekani kwenye ukanda wa Ufilipino. Alipopewa madaraka haya msaidizi wake alimletea kitabu ambacho kilikuwa na miongozo iliyotumiwa na watangulizi wake na ikawapa mafanikio makubwa. MacArthur alimuuliza msaidizi wake kuna nakala ngapi za kitabu hiko, akamjibu zipo nakala sita. Akamwambia sasa kachukue nakala zote sita na zichome moto, sitaki kufungwa na miongozo ya waliopita, kila mara litakapotokea tatizo nitafanya maamuzi sahihi kwa muda huo. Huyu ni kamanda ambaye alikuwa na mafanikio makubwa sana na kutunukiwa cheo cha juu kabisa kwenye jeshi cha Field Marshal.
Na mimi napenda kukuambia kitu kimoja, choma vitabu vyote ambavyo vinakufanya uwe na mtindo ambao unafanana na wengine. Kwa vitabu hapa namaanisha utaratibu wowote ambao umeshauzoea ambao uliutoa kwa watu wengine. Fanya uandishi wa kitofauti unaoendana na wewe na kile ambacho unataka watu wajifunze.
Nakutakia kila la kheri katika kufanyia kazi haya uliyojifunza na uweze kuboresha uandishi wako ili uweze kuwasaidia watu wengi zaidi.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: