Unapoendesha maisha yako ndani ya jamii kuna vitu vingi unatakiwa kuwa makini navyo. Kuna vitu ambavyo watu wamekuwa wanafanya kwa mazoea tu, huwa haiulizwi kwa nini inafanyika. Usipokuwa makini unajikuta unafanya vitu ambavyo havina manufaa yoyote kwako.

Moja ya vitu ambavyo vimekuwa vinachukuliwa kama ni kitu cha kawaida wakati siyo ni kuhusu mateso au kuteseka. Nafikiri umewahi kusikia mzazi akimwambia mtoto kwamba enzi zetu tuliishi kwa shida sana, sasa hivi mnapata raha sana. Au mwalimu akiwaambia wanafunzi sisi tulisoma kwa shida sana enzi zetu sasa hivi nyie mnasoma kwa raha.

Au mtu anamwambia mwenzake wewe hujapata shida kama ambazo nimepata mimi. Hali hii imekuwa inatengeneza picha kwamba aliyeteseka zaidi ndiyo yuko bora au anastahili huruma zaidi. Hili ni jambo ambalo unatakiwa kuliepuka haraka sana.

Mateso siyo mashindano, wala huhitaji kuonesha wengine kwamba umeteseka sana mpaka kufika ulipo. Unachotakiwa ni kuwaonesha wengine njia bora ya kufika pale ulipo wewe. Washirikishe mbinu nzuri zitakazowawezesha kutoka pale walipo na kufika mbele zaidi. Unaweza kuwaeleza kwa lengo la wao kujifunza lakini isiwe unawaeleza ili kujionesha kwamba wewe unastahili zaidi ya wengine.

Unapokutana na mtu anayejisifia ni kwa jinsi gani ameteseka kufika pale alipo ili kuonesha kwamba yeye anastahili zaidi, achana naye. Usimsikilize kwa sababu atakujengea hofu na dhana potofu kuhusu mafanikio. Kadiri muda unavyokwenda mambo yanatakiwa kuwa bora zaidi. Hivyo usikariri yale ya nyuma, hasa kwa upande wa mateso.

SOMA; UKURASA WA 357; Maumivu Na Mateso.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba kuteseka kwenye safari yangu ya mafanikio siyo sababu ya mimi kuwa bora zaidi ya wengine, au kustahili zaidi ya wengine. Mambo yanabadilika na sihitaji kuteseka kama walioteseka zamani, na wala wengine hawahitaji kuteseka kama mimi nilivyoteseka zamani. Nitawashirikisha watu mbinu bora za kuweza kufanikiwa na mimi nitajifunza mbinu bora kutoka kwa wengine.

NENO LA LEO.

Mateso siyo mashindano.

Wewe kuteseka kupata unachotaka haimaanishi kila mtu naye anatakiwa kuteseka ili kupata ulichopata wewe.

Wewe kuteseka wakati unatafuta mafanikio haikufanyi kuwa bora zaidi ya wengine wala haikufanyi ustahili kuliko wengine.

Washirikishe wengine mbinu bora za mafanikio na siyo kuwaambia ni kwa kiasi gani umeteseka ili waone unastahili zaidi.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.