Kati ya watu wengi wanaoingia kwenye biashara kila mwaka, ni wachache sana wanaoweza kuendeleza biashara zao na zikaweza kufikia ngazi kubwa ya mafanikio. Watu wengi wamekuwa wanaishia katikati na kufunga biashara zao. Na wale ambao hawazifungi, wanakuwa wanaziendesha bila ya faida au kwa faida kidogo kiasi cha kushindwa kuzikuza zaidi.

Watu wote hawa wanaingia kwenye biashara wakiwa na mipango mizuri sana. Hakuna mtu anayeanza biashara akiwa anajua ya kwamba anakwenda kushindwa. Kila mtu anajua kwamba biashara yake itakuwa ya kipekee na wateja wataipenda sana. Lakini hapo katikati baada ya biashara kuanza, kuna mambo yanakwenda tofauti na kusababisha biashara ishindwe kukua au hata kufa kabisa. Haya ndiyo mambo ambayo kila mfanyabiashara au anayetaka kuingia kwenye biashara anapaswa kuyajua ili aweze kujiandaa vyema na kuwa na biashara yenye mafanikio.

Kuna tofauti kubwa kati ya mipango ya biashara na biashara yenyewe. Kupanga ni rahisi, kila mtu anaweza kupanga. Na kwa jinsi jamii zetu zilivyojaa watu wenye maneno mengi, kila mtu anaweza kukushauri kuhusu biashara ipi inafaa kufanya. Watakuambia fuga kuku wana soko sana, au uza nafaka kwa sababu ni chakula watu lazima wale. Ni kweli kwa kufikiria hivi ni rahisi, ila hapo katikati kuna michakato na changamoto nyingi ambazo wengi wanakuwa hawajajiandaa nazo. Wanapoingia kwenye biashara wanazikuta changamoto hizo na kwa kukosa maandalizi wanayumbishwa sana.

Leo tutakwenda kujadili mambo matatu muhimu kuhusu biashara ambayo watu hawapendi kuyafikiria au kuyazungumzia kuhusu biashara. Mambo haya yanaweza kukuumiza lakini hayapaswi kukutisha, badala yake yanapaswa kukufanya ujiandae vizuri ili uweze kufanikiwa kwenye biashara unayokwenda kufanya.

Kitu cha kwanza ni ugumu wa biashara. Unapaswa kujua wazi ya kwamba hakuna biashara ambayo ni rahisi, kila biashara ina changamoto zake. Hivyo kabla hujaingia kwenye biashara yoyote jiulize changamoto za biashara hiyo ni zipi na unawezaje kukabiliana nazo. Changamoto za biashara zinatofautiana kulingana na aina ya biashara na ngazi unayoanzia biashara hiyo. Kwa mfano wale ambao wanaanza biashara kwa mtaji kidogo wana changamoto nyingi ambazo ni ndogo ndogo ambazo bila ya kuwa makini zinaweza kuwa kikwazo kwao kukuza biashara hizo. Na wale ambao wanaanza  biashara kwa mitaji mikubwa wana changamoto chache na kubwa sana ambazo kwa kufanya makosa madogo tu yanaleta hasara kubwa kwenye biashara.

Ni rahisi kuweka mipango ya mauzo faida na ukuaji wa biashara ila inapokuja kwenye utekelezaji mambo hayaendi kama ambavyo ulitegemea yaende. Ni rahisi kuona ukuaji wa biashara kwenye makaratasi lakini siyo kwenye ukuaji halisi. Unachopaswa kufanya ni kujiandaa vyema na kila changamoto ya biashara. Usikimbie pale changamoto inapojitokeza badala yake pambana nayo. Na kadiri unavyotatua changamoto nyingi ndivyo unavyozidi kukua kibiashara. Pia kuwa tayari kubadilika hasa pale mambo yanapokwenda tofauti na mipango yako ya awali.

Kitu cha pili unachotakiwa kukijua ni kwamba kuna watu wengi wanakazana kuizamisha biashara yako. Unaweza usipende hili lakini ndiyo uhalisia, na siku zote kuukataa ukweli haufanyi uwe uongo bali inafanya ukutane nao ukiwa huna maandalizi. Kama utaingia kwenye biashara ambayo kuna wengine wanafanya, basi watashindana na wewe kuhakikisha wanakuwa juu kuliko wewe. Na kama utaingia kwenye biashara ambayo umeibuni wewe mwenyewe na ikaonekana ina faida nzuri, wengine wengi watakuja kukuiga, na hivyo ushindani kutokea. Katika ushindani huu wa kibiashara kuna watu ambao wanachojali wao ni kuona biashara zao zinakua zaidi kuliko ya kwako na hivyo kuwa tayari kutumia njia zozote kukushusha chini. Watu wanaweza kutoa maneno mabaya kuhusu wewe na biashara yako na hata wakati mwingine kukuhujumu. Unaweza kutengeneza kitu kizuri na watu wakatumia sifa yako kujinufaisha wao binafsi.

Ni muhimu sana uweze kuilinda biashara yako, hakikisha unaweza ulinzi ambao utawazuia wale wanaotaka kutumia nafasi yako kufanikiwa wao zaidi. Kuwa mwangalifu na fuatilia kwa ukaribu sana biashara yako ili uweze kujua kila kinachoendelea nje na ndani ya biashara yako.

Kitu cha tatu muhimu kujua ni kwamba watu ni wasumbufu. Watu ni wasumbufu sana, na hii inaanza na washirika wako wa kibiashara, wafanyakazi wako na hata wateja wako. Lakini huwezi kuwakwepa watu kwa sababu ndio unaowahitaji ili biashara yako iweze kufanikiwa. Ni muhimu ujue kuna watu ambao watakusumbua sana kwenye biashara yako. unaweza kukubaliana na mtu muanze biashara pamoja lakini katikati mkashindwa kwenda pamoja. Unaweza kuajiri mtu wa kukusaidia kwenye biashara lakini akawa mzigo kwako, au hata akakusababishia hasara ya uzembe kabisa. Unaweza kupata mteja akawa msumbufu mpaka ukaona biashara unayofanya ni mzigo kwako.

Unachopaswa kufanya ni kujua utakutana na watu ambao ni wasumbufu na hivyo jiandae kuenda nao vizuri. Kama ni washirika kuwa na mpango mbadala pale mtu unayemtegemea inashindikana kwenda pamoja. Kama ni mfanyakazi kuwa na njia mbadala za kuifanya biashara iende hata kama wafanyakazi wanakuwa wasumbufu kwa muda. Na kama ni mteja hakikisha unakuwa na sera bora ya kutatua matatizo ya wateja ili mtu aweze kusaidia kulingana na changamoto aliyokutana nayo kupitia biashara yako.

Ni rahisi kukaa na kupanga biashara, au kusikia ushauri wa biashara kutoka kwa wengine. Lakini unapoingia kwenye biashara ndipo unauona ukweli mchungu ambao hukupata nafasi ya kuufikiria. Jiandae vizuri kwa mambo haya matatu ili biashara yako au ile unayokwenda kuanzisha iweze kudumu kama ambavyo unapanga idumu. Jua ya kwamba changamoto hazikosekani kwenye biashara yoyote ile.