Kabla hujafanya maamuzi yoyote muhimu kwenye maisha yako, hakikisha una taarifa zote muhimu kuhusu jambo hilo.

Unapokuwa na taarifa sahihi kuhusu jambo unakuwa kwenye nafasi nzuri ya kufanya maamuzi sahihi kwako ambayo yatakupatia kile unachotaka.

Changamoto kubwa ni kwamba watu wanaotaka wewe ufanye maamuzi ambayo yatawanufaisha wewe, hawakupi taarifa sahihi au hawakupi taarifa kamili. Badala yake wanakupa sehemu ya taarifa ambayo itakushawishi wewe ufanye maamuzi ambayo yanaweza yasiwe sahihi kwako. Katika zama hizi za taarifa, kuna ambao wanatumia taarifa kukuzidi wewe ujanja, hakikisha mara zote una taarifa sahihi.

Ni jukumu lako kutafuta taarifa kamili na sahihi kuhusu jambo kabla hujafanya maamuzi. Na usiishie kuridhika na kile unachosikia au kuona, bali dadisi zaidi wewe mwenyewe. Utapata taarifa nyingi ambazo zitakuwezesha kufanya maamuzi sahihi.

Lakini pia usitumie kisingizio cha kutokuwa na taarifa sahihi kuchelewa kufanya maamuzi. Kutafuta taarifa sahihi ni kitu unachotakiwa kukipa kipaumbele kikubwa ili uweze kufanya maamuzi sahihi mapema na bila ya kuchelewa. Kwa sababu kuna maamuzi mengine kadiri unavyochelewa ndiyo unavyokosa fursa nzuri.

Taarifa ni silaha nzuri itakayokuwezesha kupata fursa nzuri au kushinda changamoto unazokutana nazo. Kuwa na taarifa sahihi na kamili kuhusu jambo lolote kabla ya kufanya maamuzi.

SOMA; SIKU YA 13; Siri Ya Kufanya Maamuzi Yenye Mafanikio.

TAMKO LANGU;

Ninajua ya kwamba sasa hivi tunaishi kwenye ulimwengu wa taarifa. Wale wenye taarifa kamili na sahihi ndio wanaopata fursa nzuri na kuweza kutatua changamoto wanazokutana nazo. Kuanzia sasa nitahakikisha nakuwa na taarifa sahihi na kamili kuhusu jambo kabla sijafanya mamauzi. Kwa njia hii nitakuwa nafanya maamuzi bora kwangu.

NENO LA LEO.

Kabla hujafanya maamuzi makubwa kwenye maisha yako, hakikisha una taarifa kamili na sahihi kuhusu jambo hilo.

Taarifa ndiyo silaha muhimu kwenye ulimwengu wa sasa, mwenye taarifa sahihi anaweza kupata fursa nzuri na kutatua changamoto anazokutana nazo.

Usifanye maamuzi bila ya kuwa na taarifa kamili na sahihi.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.