Profesa mmoja aliwahi kutuambia darasani ya kwamba kwa uzoefu wake na kufanya kazi ya kufundisha kwa zaidi ya miaka 40 amejifunza kitu kimoja kuhusu maisha. Alisema ya kwamba huhitaji vitu vingi ili kuwa na maisha mazuri, bali unahitaji vitu viwili pekee.
Kitu cha kwanza ni milo miwili kwa siku. Kula ni muhimu ili uendelee kuwa na afya nzuri na kuendesha maisha yako. Na alisema kwa mtu mzima milo miwili kwa siku inatosha kabisa.
Kitu cha pili ni heshima, maisha mazuri ni yale ambayo unaheshimika kupitia mchango unaoutoa kwa wengine. Na hapa unahitaji kupenda ile kazi au biashara unayoifanya ili kuweza kuwagusa wengine na hatimaye unaheshimika.
Mwanzoni sikuwa nimemwelewa huyu profesa lakini baada ya kufikiri kwa kina niliona yupo sahihi. Mahitaji yetu ya msingi kwenye maisha ni madogo sana na tunaweza kuyafikia bila ya shida yoyote. Kinachotuumiza ni yale mahitaji ya anasa. Pale ambapo tunataka vitu ambavyo havina umuhimu wowote kwetu ila kwa sababu kila mtu anavyo vitu hivyo basi na sisi tunavitaka.
Pale tunaposukumwa kufanya vitu au kununua vitu ili na sisi tuonekane ndipo matatizo yote ya dunia yanapoanzia. Hapa ndipo ugumu wa maisha unapoanzia kwa sababu watu wanakazana kupata kile walichofikiri ni muhimu, lakini hata wanapokipata bado wanaona kuna kingine bora zaidi cha kutafuta. Na hivyo maisha yao yote yanakuwa ya kuwinda na hakuna hata siku moja wanaridhika na maisha yao.
Ukijua yale mahitaji yako ya msingi na kuweza kuyatimiza maisha yako yatakuwa mazuri. Ukiendeshwa na mahitaji ya anasa, ili kuonekana na wengine kila siku kuna kitu ambacho huna na ungetakiwa kuwa nacho ili uonekane vizuri. Hivyo utaishi maisha ya kukimbiza kitu ambacho hutaweza kukishika.
Mwigizaji wa Marekani Will Smith amewahi kunukuliwa akisema watu wengi wanatumia fedha ambazo hawajazichuma, kununua vitu ambavyo hawavihitaji ili kuwavutia watu ambao hawawapendi.
Angalia usiwe mmoja wa watu hawa. Yajue mahitaji yako ya msingi kwenye maisha na yafanyie kazi hayo, usiingie kwenye mashindani ya anasa, utapoteza maisha yako kwa mambo ambayo siyo muhimu.
SOMA; Mahitaji Matano Ya Msingi ya Kila Binadamu.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba mahitaji yangu ya msingi kwenye maisha ni machache sana na ninaweza kuyamudu. Kinachoniumiza ni mahitaji ya anasa, ambayo huwa hayatoshelezeki. Nimechagua kutokupoteza maisha yangu kukimbiza vitu ambavyo siyo muhimu kwangu.
NENO LA LEO.
Kwenye maisha kuna mahitaji ambayo ni ya msingi na mahitaji ambayo ni ya anasa.
Mahitaji ya msingi ni machache na kila mtu anaweza kuyamudu.
Mahitaji ya anasa ni mengi na kila siku yanazidi kukua, na kuja mapya zaidi.
Jua ni mahitaji yapi ya msingi kwako na yafanyie kazi, yale ya anasa yasikuumize kichwa.
Maisha bora yanaanza na wewe mwenyewe binafsi na siyo kile unachotaka kuwa nacho.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.