Habari rafiki?
Tunaishi kwenye zama ambazo mabadiliko tunayashuhudia sisi wenyewe. Ni zama ambazo tunatoka kwenye mfumo mmoja kwenda kwenye mfumo mwingine. Mfumo tunaotoka ni ule wa mapinduzi ya viwanda ambapo ajira ilikuwa ndiyo njia kuu ya kujitengenezea kipato. Na mfumo tunaokwenda ni ule ambao taarifa ndiyo nyenzo kuu ya maendeleo. Wale ambao wana taarifa sahihi na kuweza kuzitumia vizuri ndiyo ambao wananufaika sana.
Kutokana na mabadiliko haya ya kimfumo, ajira zimekosa ile nguvu ya zamani, zimekuwa chache kuliko idadi ya wataalamu na pia malipo ya ajira yamekuwa hayatoshelezi waajiriwa. Biashara zimekuwa ndiyo kimbilio la wengi ambao wamekosa ajira au ajira haziwapatii kile ambacho wanakitaka.

Katika mabadiliko haya pia kumekuwa na taarifa nyingi ambazo siyo za kweli. Watu wengi wamekuwa wakidanganywa kuhusu mabadiliko haya na mabadiliko wanayotakiwa kufanya wao ili kwenda vizuri na mambo yanavyokwenda. Wengi ambao wamekuwa wanabeba uongo huu na kuufanyia kazi wamekuwa wakiumia sana baadaye. Tutajadili uongo huu kwenye makala hii na hatua ambazo mtu anaweza kuchukua ili kuepuka kufanya maamuzi ambayo siyo bora kwake.
Kitu kimoja ambacho watu wengi wamekuwa wanadanganywa kuhusu biashara ni kwamba wanatakiwa kuachana na ajira zao na kuingia kwenye biashara. Hasa pale ambapo ajira zao haziwapatii kipato cha kutosheleza mahitaji yao. Ni ushauri mzuri pale unapoangalia upande mmoja wa jambo hili, lakini unapoamua kuangalia kwa kina unaona ni ushauri ambao unaweza kuwapoteza wengi wanaouchukua moja kwa moja.
Ukweli ni kwamba siyo kila mtu anaweza kuacha ajira na kuingia kwenye biashara na mambo yake yakawa mazuri. Siyo kila mtu anaweza kuendesha biashara na akaifurahia huku biashara hiyo ikifanikiwa sana. Haijalishi biashara zinaongelewa vizuri kiasi gani, siyo rahisi kama inavyoonekana kwa nje.

Biashara ni ngumu kufanya, biashara zina changamoto zake ambapo kwa ambaye anaingia bila ya kujipanga vizuri hawezi kuzimudu.
Kuna watu ambao wanataaluma zao na wanakuwa vizuri sana pale wanapozifanyia taaluma zao kazi. Wanakuwa na mchango mkubwa sana kupitia taaluma zao kama wakiweza kupeleka nguvu zao zote kwenye kile ambacho wanakifanya. Lakini biashara haihitaji hili, biashara haiangalii sana taaluma yako. Hata kama utaanzisha biashara ambayo inaendana na taaluma yako, ni mara chache sana utajikuta unatumia taaluma yako, mara nyingi utajikuta unafanya shughuli za kibiashara ambazo haziendani kabisa na taaluma yako.
Unapokuwa kwenye biashara unakutana na changamoto nyingi ambazo zinaweza kukukosesha hata usingizi. Kuna changamoto za wasaidizi wako kwenye biashara, labda muda wa kulipwa mishahara umefika na mzunguko wa fedha kwenye biashara haupo vizuri. Au kuna ambao wanashindwa kutekeleza majukumu yao kwa wakati na hivyo kuleta hasara kwenye biashara.
Wakati huo kuna changamoto za washindani wa kibiashara. Watu ambao wanatumia kila mbinu kuhakikisha wanawahamisha wateja kutoka kwako na kwenda kwao. Bado utakutana na changamoto za washirika ulionao kwenye biashara pale ambapo unafanya biashara na watu wengine. Kuna changamoto ya kutokuwa na uhakika wa kipato, kutokana na mabadiliko ya kila wakati yanayoendelea.
Changamoto hizi zinatosha kukukosesha usingizi usiku kucha. Siyo wote wanaoweza mkiki mkiki huu wa kukosa usingizi usiku kucha. Kuna watu ambao ni wazuri sana kwenye zile taaluma zao na wanaweza kufanya kwa ubora wa hali ya juu sana. Njia nzuri ya wao kuweza kufanya hivi ni kuweka muda wao mwingi kwenye kufanya kile ambacho wanakifanya vizuri. Na hapa wakisema waingie kwenye biashara, muda huo wanaukosa na kujikuta wanamezwa na changamoto za kibiashara.
Kwa watu wa aina hii ushauri wa acha kazi na nenda kafanye biashara siyo ushauri bora kwao. Kwa sababu ushauri huu unaangalia upande mmoja wa kipato pekee, ambao pia kwenye biashara siyo wa uhakika sana.

Hatua gani za kuchukua?
Kwa wale ambao wanafurahia kazi wanazozifanya, ambao wanaona wana mchango mkubwa kwa wengine kupitia kazi zao, hawapaswi kuacha kazi na kwenda kuanza biashara. Kwa sababu watakuwa wameamua kuacha kile kinachowaridhisha na kuwapa furaha na kwenda kufanya ambacho kitawasumbua sana.
Mafanikio ya kweli kwenye maisha yanaanza na mtu mwenyewe kuridhika na kile anachokifanya na kuona mchango mkubwa anaotoa kwenye maisha ya wengine. Hivyo kwa wale ambao ajira zao zinawapa nafasi hii, wanaweza kuendelea kuitumia vizuri.
Lakini kuna changamoto moja kubwa, ajira hazijitoshelezi, kipato ni kidogo kuliko matumizi na hapa ndipo msongo wa mawazo unapoanzia na kuwasukuma waajiriwa wengi kufanya maamuzi ambayo ni mabovu zaidi kwako. Hili halipaswi kuwa tatizo kwani kuna njia nyingi za kumwezesha mwajiriwa kuongeza kipato chake bila ya kuacha ajira yake.
Kuna uwezekano wa mtu kuanza biashara akiwa ndani ya ajira yake, au pia kuanza uwekezaji akiwa bado ameajiriwa. Kwa kufanya hivi mtu anaweza kujiongezea kipato cha ziada huku akiendelea kufanya kile ambacho anapenda kufanya.

Usibweteke.
Sijaandika makala hii kwa lengo la wewe kubweteka na kuendelea kung’ang’ania ajira ambayo haina msaada wowote kwako kifedha wala kihisia. Kama ajira ni mzigo kwako, hupati kipato kizuri na pia hufurahii kile unachokifanya, huoni kama una mchango mkubwa kwenye maisha ya wengine, kuendelea kukaa kwenye ajira hiyo hakuna manufaa yoyote kwako.
Pia kama umepata biashara ambayo ni nzuri na inakupa nafasi ya kutoa mchango bora kwenye maisha ya wengine, ni muhimu kuingia kwenye biashara hiyo. Ninachotaka uondoke nacho hapa ni wewe kuweza kufanya maamuzi ambayo ni bora kwako na siyo kufanya maamuzi kwa sababu kila mtu anafanya hivyo. Chagua kile ambacho ni muhimu na bora zaidi kwako.
Mwisho wa siku maisha ya furaha yanaanza na wewe mwenyewe, fanya kile ambacho unapenda kufanya na ambacho kinakuwezesha kutoa mchango bora kwenye maisha ya wengine.

Biashara ndani ya ajira.
Kwa wale ambao wapo kwenye ajira na wangependa kuingia kwenye biashara bila ya kuacha ajira zao mara moja, nimeandika kitabu ambacho kinawapa maarifa na mbinu zote muhimu za kuanzisha na kukuza biashara zao wakiwa bado wameajiriwa. Kitabu hiki kipo kwenye mfumo wa softcopy yaani pdf na kinatumwa kwa njia ya email. Gharama ya kitabu hiki ni tsh elfu 10. Kupata kitabu hiki tuma fedha tsh elfu 10 kwa MPESA 0755 953 887 au MPESA/AIRTEL MONEY 0717 396 253, majina ni AMANI MAKIRITA. Ukishatuma fedha tuma ujumbe wenye jina la kitabu BIAHSARA NDANI YA AJIRA pamoja na email yako na kisha utatumiwa kitabu. Karibu sana.

Nakutakia kila la kheri katika kufanya maamuzi ambayo ni bora kwako ili uweze kuwa na maisha ya furaha na mafanikio. Usibebe kila kitu ambacho wengine wanafanya, angalia kina manufaa gani kwako kabla hujaamua kuchukua hatua.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz