Sisi binadamu huwa tunaweka juhudi kubwa sana kwenye kutafuta kile ambacho tunakitaka, na kwa juhudi hizi tunakipata. Lakini tatizo linaanza baada ya kupata kitu hiko, tunakizoea na kuona hakina maana tena. Badala yake tunaanza kufikiria kingine ambacho hatuna na hivyo kutaka, tunakazana kukipata lakini tukishakipata tunakizoea na mchezo unaendelea hivyo.

Ingekuwa vizuri kama mwendelezo huu ungekuwa na mwisho au ungetuwezesha kufurahia vile ambavyo tunavipata. Lakini hali haiwi hivyo badala yake tunakosa furaha kwa sababu tunaamini kile ambacho hatuna ndiyo kitatuletea furaha kama tutakipata. Na tukishakipata ndiyo tunagundua kuna kingine ambacho bado hatujakipata mpaka sasa.

Tunahitaji kuchukua hatua tatu ili kuondokana na hali hii;

Kwanza tujizuie kuchukulia kwa mazoea kile ambacho tumeshakipata, ambacho tumeweka juhudi kubwa kukipata. Tuone ni vitu muhimu ambavyo tunahitaji kwenye maisha yetu.

Pili tujifunze kuvipenda vitu ambavyo tayari tunavyo. Ni rahisi kupenda vitu ambavyo hatuna na hivyo kutamani kuvipata. Lakini tukishavipata tunavizoea. Sasa tuanze na kupenda vile vitu ambavyo tunavyo sasa. Tupate muda wa kufikiria jinsi gani vitu tulivyonavyo vimekuwa na mchango kwetu, tufikirie jinsi ambavyo tutavikosa iwapo hatutakuwa navyo. Hapa tutaona umuhimu wa vile ambavyo tunavyo kwa sasa.

Tatu tunahitaji kujua kwamba furaha hailetwi na vitu ambavyo hatuna kwa sasa, bali furaha inaanza na sisi wenyewe. Hivyo ni muhimu tuache kuishikiza furaha yetu kwenye vitu ambavyo kwa sasa hatuna. Tutumie vile ambavyo tunavyo sasa kufanya maisha yetu kubwa bora zaidi. Na kama tutahitaji vingine tuvihitaji kwa kuwa bora zaidi na wala siyo kwa sababu hivyo ndiyo muhimu zaidi kuliko vile ambavyo tunavyo kwa sasa.

SOMA; UKURASA WA 403; Furaha Ipo Kwenye Mchakato, Sio Mwisho.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba nimekuwa napoteza furaha yangu kwenye maisha kwa kufikiria vitu ambavyo sina ndiyo muhimu kuliko vile ambavyo ninavyo. Kumbe vitu ambavyo ninavyo ni muhimu sana kwangu, nitajifunza kuvipenda na kuona mchango wake kwenye maisha yangu. Siweki furaha yangu kwenye vitu ambavyo sina.

NENO LA LEO.

Tunaweka juhudi kubwa kupata vitu ambavyo tunavitaka lakini tukishavipata tunavizoea na kuona ni vya kawaida. Tunahamishia juhudi zetu kutafuta vingine tena lakini tukishavipata tunavizoea na kuona bado havitoshi. Tunaweka furaha zetu kwenye vitu ambavyo hatuna kwa sasa.

Tujifunze kupenda vitu ambavyo tunavyo kwa sasa, tuone umuhimu wake kwenye maisha yetu na hivyo kuvitumia vizuri. Hapa ndipo furaha ya maisha yetu ilipo.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.