Moja ya vitu ambavyo vinamaliza nguvu zetu ni idadi ya maamuzi tunayofanya. Ubongo wetu ndiyo kiungo cha miili yetu ambacho kinatumia sehemu kubwa ya nguvu ya mwili. Na kwa kuwa ubongo ndio unaohusika kwenye maamuzi, kadiri unavyofanya maamuzi mengi ndivyo nguvu nyingi inavyotumika.
Miili yetu kwenye nguvu ni kama betri. Unapoamka asubuhi unakuwa na nguvu za kutosha, kama ulilala vizuri, sawa na betri ambayo imechajiwa vizuri. Kadiri siku inavyokwenda, nguvu zako zinapungua kama betri inavyopungua chaji unapoitumia.
Kama una simu ya smartphone, unajua kabisa kama umeichaji usiku kucha na asubuhi ukiamka iko na asilimia 100, ukianza kutembelea mitandao mbalimbali unashangaa baada ya muda mfupi imefika asilimia 90, mara 80 mara 70, mpaka ufike katikati ya siku ina chini ya asilimia 40. Na ndiyo maana kama unajua huwezi kuchaji katikati ya siku, utaepuka kutembelea mitandao mbalimbali, na wakati mwingine utazima kabisa muunganiko wa mtandao(data)
Mwili wako pia ndivyo ulivyo, unapoamka asubuhi unakuwa na nguvu za kutosha, unapoanza kufanya maamuzi nguvu hizi zinapungua. Ingekuwa vyema kama maamuzi haya unayofanya ni ya muhimu, lakini kwa bahati mbaya huwa yanakuwa siyo ya muhimu na hivyo kupoteza nguvu. Kwa mfano unaanza na niamke au nisiamke, hapo unaanza kujishawishi kwa nini uamke au usiamke. Ukishaamka unajiuliza nifanye kipi kati ya vile nilivyopanga kufanya, hapo pia unapoteza nguvu. Nguvu nyingi inapotea kama utaingia kwenye mitandao ya kijamii asubuhi, na nyingi zaidi inapotea kama utasikiliza au kuangalia au kusoma habari asubuhi.
Mpaka uje kufika muda wako wa kuanza kazi, akili imechoka na kila kitu kigumu unachotaka kufanya unaona ni bora uahirishe.
Linda nguvu zako kwa kuhakikisha unapoamka unafanya maamuzi machache sana na kikubwa ni kutekeleza yale majukumu muhimu kwako. Anza siku yako kwa mfumo maalumu, jua kabisa ukiamka unafanya vitu gani na unapoamka vifanye, bila ya mjadala. Chagua yale majukumu muhimu kwako na panga kuyafanya mapema siku yako inapoanza. Yale ambayo siyo muhimu unaweza kuyaweka mwisho wa siku yako.
SOMA; UKURASA WA 245; Uchovu Wa Maamuzi.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba kadiri ninavyofanya maamuzi mengi ndivyo ninavyomaliza nguvu zangu na hivyo kushindwa kutekeleza yale ambayo ni muhimu kwangu. Kuanzia sasa nitapunguza idadi ya maamuzi ninayofanya kwenye siku yangu, hasa wakati wa asubuhi ili niweze kuwa na nguvu za kutekeleza yale ambayo ni muhimu kwangu.
NENO LA LEO.
Kadiri unavyofanya maamuzi mengi kwenye siku yako, ndivyo unavyopoteza nguvu zako na hivyo kushindwa kutekeleza yale ambayo ni muhimu kwako.
Kuwa na mfumo wa kuianza siku yako kila siku, mfumo ambao utapunguza idadi ya maamuzi unayohitaji kufanya. Kwa kuwa na mfumo unajua ukiamka ni kipi unafanya na unapoamka kifanye, badala ya kuamka na kuanza kujiuliza nifanye nini, hapo unapoteza muda na nguvu zako.
Tunza nguvu zako kwa kupunguza idadi ya maamuzi unayofanya kwenye siku yako.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.