Moja ya vitu ambavyo vinawazuia watu kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yao ni kujificha. Watu wanakuwa na hamasa kubwa sana ya kufikia mafanikio, lakini wanapopiga hatua kidogo wanapata sehemu ya kujificha, na wao wanajificha.

Mtu anakuwa na mipango mizuri ya kibiashara, anaingia kwenye biashara hiyo na mwanzoni anaweza kutengeneza faida nzuri, baada ya hapo anajifunza ni kipi kinaleta faida na kipi hakileti faida. Na hapo anachagua ni vitu gani anavipa kipaumbele kufanya. Kinachotokea baada ya hapa ni mtu kuendelea kufanya kile tu ambacho kinaleta faida, na kukifanya kwa njia ile aliyozoea kufanya kila mara. Matokeo mazuri ya mwanzo yanamfanya mtu ashindwe au aogope kujaribu njia nyingine bora. Na hapa ndipo mtu anapokuwa amejificha, kila siku anafanya kile kile na kuwa kwenye hatari ya kupotezwa na wengine.

Mfano mwingine ni mtu anayeingia kwenye ajira, akiwa na hamasa kubwa ya kutoa mchango kwa wengine kupitia biashara hiyo. Lakini anapoanza kufanya kazi yake anagundua kuna yale matokeo ya kawaida tu ambayo akiweza kuyafikia hakuna anayemsumbua. Na anapojaribu kufanya mambo ya tofauti, wengine hawakubaliani naye. Kwa njia hii mtu anaamua kufanya kwa kile kiwango cha kawaida ambacho kila mtu anafanya na hasumbuliwi. Hapa mtu anakuwa amejificha kwenye kufanya viti kikawaida ili asisumbue wengine, lakini hii ina athari kubwa kwenye ujuzi na uzoefu wake wa kikazi.

Hata kwenye maisha ya kawaida watu wengi wamekuwa wakijificha kwa kuogopa kufanya vitu ambavyo havijazoeleka, wanaendelea kufanya kile ambacho kila mtu amezoea au wao wenyewe wamezoea. Hii inawaweka kwenye maisha ya kawaida na kuwa watu wa kawaida.

Watu wamekuwa wanajificha kwa sababu hawapo tayari kushindwa, hawapo tayari kukosolewa na hawapo tayari kuharibu kile ambacho wanaona kwa sasa kipo vizuri. Kila mtu anapenda kupata matokeo mazuri kwa anachofanya, hivyo kufanya kile alichozoea kuna nafasi ndogo sana ya kushindwa kuliko kufanya kitu kipya. Watu hawapendi kukosolewa, hivyo kufanya mambo mapya kunatoa nafasi kwa wengine kuwakosoa. Hivyo watu wanaamua kujificha, kwa kufanya kilichozoeleka kufanya.

Leo nakuambia usijifiche, usifanye jambo kwa sababu ndiyo umezoea kufanya hivyo au ndivyo kila mtu alivyozoea kufanya. Bali fanya jambo kwa sababu, fanya jambo ukijua unaboresha zaidi na fanya jambo ukijua utajifunza kitu kipya ambacho kitakupa njia mpya za kufanya kile unachofanya.

Kujificha kumeua uwezo mkubwa wa watu wengi, na kumekuwa kunaua uwezo wako kidogo kidogo. Anza kujiuliza ni maeneo yapi ya maisha yako ambayo umekuwa unajificha? Kwenye kazi, biashara na hata maisha ya kawaida. Angalia maeneo unayojificha na kisha amua kuacha kujificha.

TUPO PAMPJA,

KOCHA.

SOMA; Njia 30 Za Kufikia Mafanikio Makubwa Sana(World Class)