Asilimia kubwa ya mambo tunayofanya kwenye siku za maisha yetu tunafanya kwa tabia. Yaani tunafanya kwa sababu ndivyo tulivyozoea kufanya. Na mara nyingi huwa ndivyo ambavyo imezoeleka kufanyika kwenye jamii ambazo tunaishi.
Kadiri siku zinavyokwenda, mambo yanazidi kuwa magumu na hivyo tabia za watu kubadilika na kuzidi kuwa mbaya au zisizoendana na mafanikio. Na hili limefanya baadhi ya tabia kuwa na faida kubwa sana kwa sababu ni wachache wanaoweza kuwa nazo kwenye ulimwengu huu unaobadilika kwa kasi kubwa.
- Mtazamo chanya. Ni vigumu sana kuwa na mtazamo chanya kwenye dunia hii ambayo kila mtu analalamika na kutafuta wa kulaumu. Dunia ambayo vyombo vya habari vinatoa habari hasi kuliko chanya.
- Uzalishaji na ufanisi mkubwa. Kadiri teknolojia na mtandao vinavyokua, ndivyo vitu vya kupoteza muda vinazidi kuwa vingi. Simu zetu zimekuwa chanzo namba moja cha kupoteza muda. Imekuwa vigumu sana zama hizi mtu kukaa na kufanya kazi yake huku mawazo yake yote yapo kwenye kazi anayofanya.
- Kubobea kwenye kile unachofanya. Kadiri siku zinavyokwenda, na mambo ya kufanya kuongezeka, ni wachache sana wanaoweza kubobea kwenye kile wanachofanya. Wengi wanagusa juu juu na kuachia hapo.
- Utu wema. Maisha yanavyozidi kuwa magumu kila mtu anajijali yeye zaidi, hili linafanya watu kupoteza utu wema.
Jijengee tabia hizi ambazo zinapotea kwa wengi, na haitatokea hata siku moja ukakosa fursa nzuri zitakazokufikisha kwenye mafanikio. Unaweza kuona kama fursa zinachelewa, lakini nikuhakikishie zitakuja mpaka utazikimbia.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba kadiri siku zinavyokwenda watu wanazidi kuwa hasi, wanakuwa na uzalishaji mdogo, wanashindwa kubobea na wanakosa utu wema. Mimi nitajijengea tabia hizi na kuhakikisha nakuwa vizuri kwa sababu tabia hizi zitaniletea fursa kubwa za kufikia mafanikio.
NENO LA LEO.
Kadiri maisha yanavyozidi kuwa magumu, ndivyo watu wengi wanavyokuwa na mitazamo hasi, wanakuwa na uzalishaji mdogo, wanashindwa kubobea kwenye kile wanachofanya na kukosa utu wema.
Hii ni fursa kubwa kwako kujijengea tabia hizo ambazo zitakuwezesha kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako. kuwa CHANYA, ongeza UZALISHAJI wako, BOBEA na kuwa MTU MWEMA.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.