Mtoto hawezi kujua kutembea sawasawa bila ya kuanguka.
Anayejifunza kuendesha baiskeli hawezi kujua kuendesha kama hatoanguka mara kadhaa.
Watu wote ambao tunawaona leo wameweza kufanya mambo makubwa, hawakuanza kuyafanya mambo hayo tangu awali, bali walishindwa sana na kujifunza kupitia kushindwa kwao.
Hivyo basi kushindwa kwenye kile unachofanya siyo jambo baya kwenye maisha, bali ni njia ya kujifunza na kukua zaidi.
Lakini mbona sisi tunaogopa sana kushindwa? Kwa nini tunahofia kushindwa mpaka tunafikia hatua ya kuogopa hata kuanza? Kwa nini tunaogopa kushindwa mpaka tunakata tamaa ya kutorudia tena baada ya kushindwa?
Hii yote ni kwa sababu tunachukulia kushindwa kama ujinga, uzembe, uwezo mdogo na vitu vingine vya namna hiyo vinavyoonesha kushindwa ni hali ya chini. Pia hatupendi kuonekana na wengine kwamba tumeshindwa, na hivyo tunaficha kushindwa kwetu au tunaacha kabisa kufanya.
Mtoto asingekuwa tayari kuanguka asingeweza kutembea, angeendelea kukaa maisha yake yote.
Na wewe pia kama utaendelea kuogopa kushindwa, hutaweza kutoka hapo ulipo sasa. Utaendelea kuwa hapo na kufanya kile ulichozoea kufanya. Na mbaya zaidi ni kwamba hubaki hapo ulipo, bali unarudi nyuma, kwa sababu dunia inazidi kwenda mbele iwe unaenda nayo au umegoma kwenda nayo.
Kushindwa ni sehemu ya kujifunza, unajifunza ni njia ipi ambayo siyo sahihi kutumia na pia unajifunza thamani ya ushindi. Kitu chochote ambacho kinakuja kirahisi huwa kinapotea kirahisi, kama unapata kila kitu bila ya kushindwa utachukulia kushinda kama kitu kidogo. Lakini pale unaposhindwa unachukulia kushinda kama kitu chenye thamani kubwa sana kwako.
Kushindwa pia ni sehemu ya kukua zaidi. Ili utoke hapo ulipo na kufika juu zaidi, unahitaji kushindwa. Unahitaji kushindwa kwa sababu utatakiwa kufanya vitu ambavyo hujawahi kufanya, na hivi vina nafasi kubwa ya wewe kushindwa. Wengi huwa wanaogopa kufanya vitu hivyo na kujikuta wanaendelea kufanya vile walivyozoea kufanya, na hivyo hawakui. Wewe unapokuwa tayari kushindwa, unafungua milango ya ukuaji na kuwa tayari kufanya mambo makubwa.
Usichukulie kushindwa kama adui wa mafanikio yako.
Usifanye kushindwa kukupe hofu ya kuchukua hatua.
Tumia kushindwa kama hatua ya wewe kujifunza na kukua zaidi.
Anza kushindwa leo, ili kesho uwe na njia ya uhakika ya kufanikiwa.
Ni kitu gani kikubwa ambacho umekuwa unatamani kukifanya lakini hofu ya kushindwa inakuzuia kuanza? Anza kukifanya leo hii.
TUPO PAMOJA,
KOCHA MAKIRITA AMANI.
SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; FAIL FORWARD (Hatua 15 Za Kufikia Mafanikio Kupitia Kushindwa).