Kila mtu anapenda kufanikiwa, lakini siyo kila mtu yupo tayari kulipa gharama za mafanikio.

Ili kufanikiwa na kuishi maisha bora na yenye furaha, kitu cha kwanza kabisa unachohitaji kuwa nacho ni uhuru. Uhuru wa maisha yako na kuweza kufanya kile ambacho unakipenda na unajua ni muhimu kwako na kwa wanaokuzunguka.

Lakini uhuru hauji bure, unakuja na gharama zake pia. Pia uhuru huu haimaanishi kwamba uko huru kufanya unachotaka au upo kwenye jamii huru, bali inamaanisha uhuru kamili kwako.

Uhuru kamili kwako ni uhuru unaoanzia kwenye fikra zako, unaondokana na hukumu ulizokuwa unatoa kwa wengine, unaacha kuwa na upande na unakuwa tayari kujifunza na kushirikiana na yeyote. Uhuru kamili hauzuiliwi na mipaka iliyowekwa kijamii kama kabila, dini, rangi, umri.

Uhuru kamili unaufikia pale unapogundua ya kwamba kitu pekee ambacho ni wewe ni wewe mwenyewe. Pale unapojua ya kwamba wewe utabaki kuwa wewe bila ya kujali unapitia nini kwa sasa. Unajua wewe ni wewe, na wewe siyo cheo ulichopewa au sifa unazopewa na wengine. Unajua hizi zinaweza kuondoka muda wowote lakini wewe utabaki.

Kwa kuwa na uhuru kamili unakuwa na mchango bora kwa jamii inayokuzunguka na hivyo kuweza kupata matokeo bora kabisa.

Unapokuwa na uhuru kamili huhukumu wengine, kwa sababu unajua kile wanachofanya watu kwa nje ni vigumu kujua kwa ndani.

Unapokuwa na uhuru kamili hujiwekei mipaka kwamba naweza kufanya kazi na watu fulani na wengine siwezi kufanya nao kazi.

Unapokuwa na uhuru kamili unakuwa tayari kujifunza kutoka kwa kila mtu unayekutana naye, bila ya kujali umemzidi au amekuzidi.

Unapokuwa na uhuru kamili unakuwa kwenye ngazi tofauti kabisa ya uhakika wa kuyafikia mafanikio makubwa.

Tujijengee uhuru kamili ambao utaimarisha mahusiano yetu na wengine.

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

SOMA; Huu Ndiyo Uhuru Unaohitaji Kuununua Kutoka Kwenye Biashara Yako.